Mbwa wawindaji (kundinyota)

Mbwa Wawindaji (kwa Kilatini na Kiingereza Canes Venatici) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakaskazi ya Dunia.

Nyota za kundinyota Mbwa Wawindaji (Canes Venatici ) katika sehemu yao ya angani
Kundinyota ya Canes Venatici - Mbwa Wavindaji katika atlasi ya nyota ya Johannes Hevelius. Nyota zinaonyeshwa "kwa macho ya Mungu", yaani kama mtazamazi angekuwa nyuma yao hivyo kinyume jinsi mtazamaji dunani anaziona.

Mahali pake

Mbwa Wawindaji linapakana na makundinyota yaa Nywele za Berenike (Coma Berenices), Bakari (Boötes) na Dubu Mkubwa (Ursa Major). Nyota angavu ya Simaki (ing. Arcturus) iko jirani.

Jina

Kundinyota hili halikujulikana kwa mabaharia Waswahili wa Kale wala kwa Waarabu au Wagiriki kwa sababu nyota zake ni hafifu sana. Katika enzi ya kale nyota hizi hazikupangwa kuwa sehemu ya makundinyota maalumu yaliyoorodheshwa na Klaudio Ptolemaio kando ya Dubu Mkubwa. Mbwa Wawindaji ni kati ya makundinyota yaliyoanzishwa na mwanaastronomia Johannes Hevelius wa Danzig (Gdansk) mnamo mwaka 1690 BK. Akiwa mpika pombe na mfanyabiashara tajiri aliyeshika kwa muda pia umeya wa mji wake alikuwa hasa maarufu kwa kuangalia, kupima na kuorodhesha nyota pamoja na mke wake Elisabeth Hevelius.

Hevelius aliyelenga kujaza mapengo kati ya kundinyota akiandika kwa Kilatini alichagua jina “Canes Venatici”. Kwa kufuata mapokeo aliona katika sehemu hii ya anga mbwa wa mwindaji Bakari (Bootes) waliomsaidia kuwinda Dubu Mkubwa. Petrus Plancius aliwahi kubuni hapa kundinyota jipya la Jordanus (mto Yordani) lakini hii haikukubaliwa na Hevelius badala yake aliona hapa Canes Venatici, Leo Minor na Lynx.

Canes Venatici - Mbwa Wawindaji iko kati ya makundinyota 88 yaliyoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kwa jina la Canes Venatici. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'CVn'.[2]

Nyota

Mbwa Wawindaji – Canes Venatici ina nyota hafifu tu. Nyota angavu zaidi ni Alfa Canum Venaticorum ambayo ni nyota maradufu yenye mag 2.9 na nyota yake ya pili ina mag 5.6. Nyota kuu ina umbali wa miakanuru 110 kutoka Dunia.[3]. Ilipewa jina la Cor Caroli ("moyo wa Carolus = Charles") huko Uingereza kwa heshima ya mfalme Charles I wa Uingereza aliyeuawa katika mapinduzi ya Oliver Cromwell huko Uingereza mwaka 1649.

  • Beta Canum Venaticorum (pia: Chara) ina mag 4.2 ikiwa umbali wa miakanuru 27 kutoka kwetu. "Chara" ni jina la Kigiriki kwa furaha.[4]

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Canes Venatici " katika lugha ya Kilatini ni "Canum Venaticorum" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Canum Venaticorum, nk.
  2. The constellations, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. Canes Venatici, tovuti ya Ian Ridpath "Star Tales", iliangaliwa Oktoba 2017
  4. linganisha Ridpath, Canes Venatici

Viungo vya Nje