Kwa maana mengine ya neno hili tazama Paa (maana)

Mapaa ya mji wa Ashdod katika Israeli penye mvua kidogo
Paa ya vigae vya ubao nchini Poland

Paa ni eneo la juu la nyumba ambalo linatumika kuziba eneo la ndani lisionekane kutoka juu na pia kuzuia jua na mvua, theluji na jua visiingie ndani.

Kuna aina nyingi za paa na hizi zinategemea mazingira ya nyumba hasa hali ya hewa na pia teknolojia inayopatikana.

Paa kufuatana na mazingira

hariri

Katika mazingira penye mvua nyingi kidesturi paa inahitaji mtelemko ili maji yasikae na kuingia ndani. Kama mazingira yana upepo mkali si vizuri kuwa na mtelemko mno maana watu waliweka mawe juu ya paa kwa kusudi la kuimarisha paa dhidi ya upepo mkubwa.

Lakini katika mazingira kavu pasipo na mvua nyingi watu hupendelea paa ambalo ni tambarare. Paa tambarare inaruhusu kuitumia kama eneo la nje. Hasa katika nchi za joto watu hupenda kulala juu ya paa wakati wa usiku kama joto ni kubwa mno ndani ya nyumba. Ni pia mahali ambako vyakula kama matunda vinaweza kukaushwa katika jua ilhali yako mbali na wanyama au wezi wanaotembea chini. Hata hivyo kwa kawaida taa tambarare huwa na mtelemko kidogo ili maji ya mvua kama inatokea inatelemka kirahisi zaidi.

Teknolojia ya kisasa inaruhusu kuwa na taa tambarare hata katika mazingira penye mvua nyingi. Hapa paa hujengwa kwa saruji iliyoimarishwa kwa feleji pamoja na kemikali zinazozuia maji na kuziba paa kabisa. Faida yake ni ya kwamba ghorofa ya juu moja kwa moja chini ya paa la nje ina nafasi kubwa inaweza kutumiwa.

Sehemu za paa

hariri

Paa huwa na sehemu mbili ambazo ni maunzi yake ya ndani halafu ganda la nje.

Maunzi ya ndani ya paa kwa kawaida hulala juu ya kuta za nyumba. Yanatengenezwa kwa kutumia bao, na tangu karne ya 19 pia kwa kutumia vyuma au feleji.

Kuna njia nyingi za kupata ganda la nje. Katika sehemu nyingi za dunia watu walitumia manyasi yanayofungwa pamoja. Kama hayatengenzwi vizuri sana kwa kutumia manyasi za pekee paa la aina hii inavuja kirahisi inahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Lakini penye manyasi yenye umbo la mrija kama gugumua kuna paa imara sana; zinaendelea kutumiwa hata katika nchi za kaskazini kama Denmark, Ujerumani au Uingereza.

Lakini kwa jumla watu wanpendelea kuwa na ganda la nje ya paa isiyoweza kuvuja. Mabati ni njia rahisi ya kufunika paa tena nyepesi; kazi ya kufunika inaenda haraka na ganda hili si nzito kwa hiyo gharama za maunzi ya ndani si kubwa. Paa la mabati ina hasara ya kwamba mabati yanashika kutu na kuharibika baada ya miaka kadhaa; pia hakuna kinga dhidi ya joto au baridi.

Vigae ni njia bora ya kufunika paa; vigae ni kama matofali vinatengenzwa kwa kutumia udongo wa ufinyanzi unaopikwa katika tanuri. Kama vimetengenezwa vizuri vinaweza kudumu karibu dekadi nyingi karibu karne. Pia vina kinga dhidi ya baridi na joto kushinda bati.

Kutegemeana na mazingira kuna pia mbinu tofauti; mlimani penye mawe ya kufaa kuna uwezekano kutumia pia bapa za mawe. hii inahitaji lakini ubao nyingi kwa ajili ya maunzi ya chini kwa sababu bapa za jiwe ni nzito sana.