Nyotabadilifu

(Elekezwa kutoka Nyota geugeu)

Nyotabadilifu (kwa Kiingereza: variable star) ni nyota ambayo inaonekana huku mwangaza wake unabadilika-badilika; yaani kuna mabadiliko ya kurudiarudia jinsi mwangaza wake unavyoonekana na mtazamaji.

Nyotabadilifu za kupatwa: nyota maradufu zinazozungukana na kufunikana hivyo kuleta mabadiliko ya mwangaza

Mabadiliko hayo ya mwangaza yanaweza kutokea katika muda wa saa, siku, miaka hadi karne kadhaa. Tofauti zinaweza kuwa ndogo tu au kubwa.

Kimsingi kuna hali mbili zinazosababisha nyota kuwa badilifu:

  • sababu za ndani ya nyota, kwa mfano nyota inapanuka na kuwa angavu zaidi halafu kunywea tena
  • sababu za nje ya nyota, kwa mfano kuna kitu kinachopita mbele yake na kupunguza kiwango cha nuru kinachofika kwetu.

Nyota nyingi huwa na kiwango cha badilifu, hata Jua letu lina kiwango kidogo cha mabadiliko ya mwangaza wake kwa asilimia 0.1 yanayorudia baada ya miaka 11[1].

Historia ya kutazama nyotabadilifu

hariri

Nyota badilifu zilitambuliwa tayari zamani, pale ambako watu waliangalia nyota kwa utaratibu na kutunza kumbukumbu. Maandiko ya Misri ya Kale yaliyotungwa mnamo mwaka 1200 KK ina habari za vipindi vya siku za bahati nzuri au bahati mbaya. Vipindi hivi vinalingana na vipindi vya badilifu vya nyota ya Rasi Madusa (Algol) wakati ule.[2].

Kuna pia habari katika maandiko ya China ya Kale zinazotaja mabadiliko kati ya nyota, ingawa haieleweki kama hii ilihusu nyotamkia, nyota nova au badilifu.

Lakini falsafa ya nyakati za kale iliamini ya kwamba anga halibadiliki,hivyo matukio kama nyotamkia yaliaminiwa kutokea katika angahewa, si angani kwenyewe.

Nyota badilifu ya kwanza iliyotambuliwa katika kipindi cha kisasa kwenye mwaka 1596 ilikuwa Mira (Omikron Ceti) katika kundinyota ya Ketusi. Inabadilika katika kipindi cha miezi 11; wakati wa kuwaka inafikia mag 2 lakini baadaye inafifia hadi mag 11 haionekani tena kwa macho matupu. Hivyo mgunduzi wake David Fabricius aliamini mwanzoni ni nyota nova hadi alipotambua ni kitu kipya na cha ajabu angani.

Mwingereza John Goodricke alikuwa wa kwanza kutoa maelezo ya hali ya kibadilifu baada ya kutazama Rasi Madusa (Algol) akahisi ya kwamba kuna sayari kubwa inayopita mbele yake na hivyo kunpunguza mwangaza wake. Leo hii tunajua hii ni nyota maradufu na kuna nyota dhaifu inayozunguka nyota angavu na hivyo kupunguza nuru yake.

Idadi ya nyota badilifu iliongezeka sana tangu kupatikana kwa kamera za kupiga picha za nyota katika karne ya 19. Picha zinarahisisha ulinganifu wa anga kwa nyakati mbalimbali na kutambua tofauti za mwangaza.

Toleo la mwisho la Orodha ya Nyota Badilifu (General Catalogue of Variable Stars)[3] (2008) linataja nyota badilifu zaidi ya 46,000 katika Njia Nyeupe pamoja na 10,000 katika galaksi nyingine na zaidi ya 10,000 zinazodhaniwa kuwa badilifu bila kuthibitishwa.

Aina za nyotabadilifu

hariri
 
Mpito wa sayari mbele ya uso wa nyota unapunguza mwanga wake kwa muda; ukipimwa unaleta habari juu ya obiti na ukubwa wake

Nyota zinaweza kuonekana badilifu kwa sababu tofauti.

  • Nyotabadilifu ya kupwita (pulsating variable stars)
Nyota hizi zinapanuka na kunywea; wakati wa kupanuka mwangaza unaongezeka, wakati wa kunywea mwangaza unapungua.
  • Nyotabadilifu za kufoka (eruptive variable stars)
Kila baada ya muda zinarusha mata kwenye anga kama sufuria ya kuchemsha maji ambapo maji yanatolewa nje ya sufuria. Hapa mwangaza unaongezeka.
  • Nyotabadilifu za kulipuka (cataclysmic or explosive variable stars)
Hasa ni nyota nova yaani nyota ambazo zimenywea sana na kuporomoka ndani yake; hatua hii inafuatwa na mlipuko; hapo nyota inatoa nishati nyingi sana kwa muda mfupi.
  • Nyotabadilifu kiviringi (Rotating variable stars)
Kama nyota ina doa kubwa upande moja doa hili litaonekana au kutoonekana kutegemeana na mviringio wa nyota(linganisha Madoa ya Jua) vilevile kama umbo la nyota si kama tufe itaonyesha mara upande mpana, mara upande mwembamba na hiyvo kutoa viwango tofauti vya nuru
  • Nyotabadilifu za kupatwa (eclipsing binaries)
Kwa kawaida hizi ni nyota maradufu. Mfano wake mashuhuri ni Rasi Madusa (Algol) ambayo ni nyota mbili za karibu zinazoonekana kama nyota moja tu. Hizi mbili zinabiringiana. Kama ziko kandokando tunapata nuru ya pande zote mbili, kama nyota yenye mwangaza mdogo inafika mbele ya nyota yenye mwangaza mkubwa nuru inafifia.
  • Nyotabadilifu kutokana na mipito ya sayari (planetary transits)
Zinafanana na nyota zinazopatwa. Kama nyota ina sayari inayopita mbele ya uso wake mwangaza wake hupungua kiasi

Marejeo

hariri
  1. Fröhlich, C. (2006). "Solar Irradiance Variability Since 1978". Space Science Reviews. 125: 53
  2. Jetsu, L.; Porceddu, S. (2015). "Shifting Milestones of Natural Sciences: The Ancient Egyptian Discovery of Algol's Period Confirmed". PLoS ONE. 10 (12): e.0144140 (23pp). online hapa
  3. Samus, N. N.; Kazarovets, E. V.; Durlevich, O. V. (2001). "General Catalogue of Variable Stars". Odessa Astronomical Publications. 14: 266. Bibcode:2001OAP....14..266S.

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: