Serikali ya kiraisi
Serikali ya kiraisi ni muundo wa siasa ambako serikali imo mikononi mwa rais wa nchi. Rais huyu anaunganisha nafasi za Mkuu wa Dola na pia kiongozi wa serikali.
Muundo huu ni tofauti na serikali ya kibunge ambako rais ni zaidi cheo cha heshima tofauti na kiongozi wa serikali ambaye huchaguliwa na bunge lenye madaraka ya kumwondoa tena.
Tabia za serikali ya kirais
haririTabia za utaratibu huu mara nyingi ni:
- Rais ni mkuu wa dola pia kiongozi wa serikali.
- Rais hashiriki katika bunge wala si mbunge. Katika nchi kadhaa ana haki ya kupinga sheria za bunge, kwa mfano Marekani. Hapa rais anaweza kusimamisha sheria za bunge kwa tamko la "veto" (kwa Kilatini: "Nakataa"; kwa Kiswahili "Turufu"). Kura ya pili ya theluthi mbili za wabunge linaweza kushinda tamko hili.
- Rais ana kipindi maalumu kisichoongezeka.
- Rais hawezi kuondolewa kwa tamko la bunge la kutokuwa na imani naye jinsi ilivyo kwa waziri mkuu katika serikali ya kibunge. Lakini kwa kawaida kuna utaratibu maalumu wa kumwondoa rais kwa sababu za pekee, kwa mfano akionekana amevunja sheria kwa tendo la jinai.
- Kazi ya mawaziri imo mikononi mwa rais anayewapa cheo, pia anaweza kuwaondoa; taratibu za nchi zinatofautiana kama bunge lathibitisha mawaziri au la.
Mifano
hariri- Serikali za kirais ziko kwa mfano Marekani, Meksiko, Ufilipino na nchi nyingi za Amerika Kusini, pia za Afrika.
- Kuna pia nchi za kidikteta zinazotumia muundo wa karibu na serikali ya kirais lakini kwa kawaida uwezo wa bunge ni mdogo sana.
- Cheo cha rais katika serikali ya kibunge ni tofauti sana na muundo huo wa kirais.
Faida na hasara
haririKati ya faida za utaratibu wa kirais hutajwa mara nyingi serikali imara yenye nguvu katika utendaji. Kiongozi wa taifa ana nafasi kubwa kufuata siasa anayoiona ni lazima kwa mema ya nchi, hata kama wabunge wameanza kusitasita au kuogopa hasira ya wananchi. Kazi ya serikali inategemea nia ya mtu mmoja aliyepewa na wananchi wote nafasi na muda wake. Anayeangaliwa ni haki yake na pia wajibu wake kutumia madaraka haya.
Nguvu hii ni pia udhaifu wa muundo huo: kama rais ni mtu hafifu au mtu anayekosa uelewano mwema wa matatizo yaliyopo. Pia madaraka makubwa ya rais yameonekana kurahisisha kuundwa kwa udikteta kama huyu rais akitumia madaraka yake kubadilisha mgawanyo wa madaraka kati ya matawi ya dola yaani serikali, bunge na mahakama.
Muundo wa kumbakumba ya Serikali
haririNchi mbalimbali hutumia utaratibu wa kuunganisha tabia za serikali ya kirais na serikali ya kibunge. Mfano wake ni Ufaransa ambako rais anayechaguliwa na wananchi wote hushirikiana na waziri mkuu anayetegemea bunge. Rais ana madaraka kadhaa pamoja na haki ya kuongoza mikutano ya mawaziri akitaka. Ana haki ya kutoa mwongozo juu ya siasa ya nje na pia ni mkuu wa jeshi.
Lakini anahitaji kushiriki katika kempeni za bunge na kuomba wananchi kumpa wabunge watakaoshikamana naye. Kama wananchi wanaamua tofauti anapaswa kushirikiana na waziri mkuu asiyekubaliana naye katika siasa. Hii ni njia mojawapo ya kuwapa wananchi nafasi ya kuweka mipaka kwa madaraka na uwezo wa rais wakiona asiamue kila kitu tena pekee yake.
Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |