Ufalme ni mfumo wa utawala ambapo mfalme, malkia au mtu mwingine aliyerithi cheo chake ni mkuu wa dola. Vyeo vingine vya mkuu katika ufalme ni pamoja na kaisari, shah, tenno, sultani, amiri au mtemi. Kwa kawaida mfalme amerithi cheo chake kutoka kwa baba yake au mama yake, kwa hiyo alizaliwa kama mfalme mteule na ataendelea kuwa na cheo hicho hadi kifo chake. Lakini kama mfalme aliyetangulia hakuwa na mrithi inawezekana ya kwamba mfalme mpya amechaguliwa. Mfano wa dola lenye mfumo wa ufalme ambapo mkuu anachaguliwa mara kwa mara ni Vatikani ambapo Papa ni mkuu wa dola.

Taji la mfalme Louis XV wa Ufaransa; taji ni alama za cheo cha mfalme katika nchi nyingi

Neno ufalme hutumiwa pia kwa kutaja nchi inayotawaliwa na mfalme au malkia, kwa mfano Ufalme wa Maungano, Ufalme wa Eswatini na kadhalika.

Kiwango cha madaraka cha mfalme huwa na tofauti kubwa. Leo hii wafalme wengi wako chini ya katiba ya nchi na mara nyingi wana madaraka machache; nafasi yao ni ya heshima na desturi. Lakini kuna falme kadhaa ambaPo mfalme bado ana madaraka makubwa, habanwi na katiba wala bunge wala serikali kama vile Omani au Saudia.

Tofauti ya ufalme na jamhuri hariri

Kinyume cha ufalme ni jamhuri inayoongozwa na mkuu, mara nyingi kwa cheo cha rais au katika nchi kadhaa na kamati ya watu wanaochaguliwa na kwa kawaida kwa kipindi fulani. Mara nyingi rais wa nchi huchaguliwa kwa kipindi cha miaka 4-6 na katika nchi nyingi kuna uwezekano Wa kwamba anarudi tena kwa kipindi kingine. Kuna jamhuri ambapo vongozi wanalenga kuhakikisha ya kwamba mtoto wao anaendelea na cheo cha mkuu wakiacha kutawala, lakini hii kwa kawaida si utaratibu wa kisheria katika jamhuri; mfano wa kisasa ni Korea Kaskazini ambayo ni jamhuri inayotawaliwa na familia Kim katika kizazi cha pili ilhali mtoto wa kiongozi Kim Jong Il anateuliwa kumfuata baba.

Historia hariri

Sababu za kuanzishwa kwa ufalme hariri

Ufalme ni muundo wa kale sana lakini haukuwa mfumo wa kwanza wa serikali. Wataalamu huona ya kwamba chanzo chake ni azimio la kabila au kundi dogo la watu kumruhusu mtoto wa kiongozi mwenye nguvu na uwezo kuendelea na shughuli za baba. Kuna mifano watu walioishi na viongozi wa muda tu waliamua kuwa na mfalme wakati wa vita wakiona uongozi wenye nguvu ni wa lazima. Kulitokea pia ya kwamba kiongozi aliyeteuliwa kwa kipindi cha matatizo au vita alionekana kuwa na uwezo akaendelea hadi kifo na kumpatia mtoto wake nafasi ya mrithi wakati alipokuwa bado na nguvu.

Historia ya Biblia kama mfano wa kuanzishwa kwa ufalme hariri

Biblia inasimulia jinsi gani watu wa Israeli ya Kale walioongozwa kila mahali na wazee lakini kama walipata matatizo makubwa viongozi walijitokeza walioitwa "Waamuzi" na kuwa na majukumu ya kijeshi pamoja na ya kisheria. Kitabu cha Waamuzi 8#22 kinaonyesha pia jinsi gani suala la ufalme lilivyokuwa na ugumu; mwamuzi Gideon alipoombwa na watu kuwa mfalme alikataa na kudokeza ya kwamba Mungu pekee anastahili kuwa na cheo hicho. Baadaye Sauli alijitokeza kama kiongozi dhidi ya tishio la Waamoni; alipowashinda vitani watu walimfanya Sauli mfalme wao wa kwanza. Mataifa mengi walipata ufalme kwa njia zilizofanana na Israeli ya Kale yaani wakati wa vita ambapo wengi walikubali haja ya kiongozi mwenye nguvu.

Kupinduliwa kwa wafalme au kubanwa kwa madaraka yao hariri

Mfano mashuhuri wa kinyume ni historia ya Athens au Roma ya Kale ambazo zilitawaliwa zamani na wafalme lakini viongozi wa miji hiyo walifukuza wafalme baada ya kuona tabia za kidikteta pamoja na kupuuzia haki za watu wakaanzisha jamhuri zilizoteuliwa na viongozi waliochaguliwa kwa muda tu. Lakini Roma ya Kale ilirudia mfumo wa ufalme tangu Kaisari Augusto ingawa kwa jina iliendelea kama jamhuri hadi mwisho.

Mara nyingi wafalme waliunganisha nafasi za mkuu wa serikali na kiongozi wa jeshi na jaji mkuu. Mataifa mbalimbali walimjua mfalme pia katika nafasi ya kidini kama kuhani mkuu au kama mkuu anayeshika nafasi ya Mungu duniani.

Mamlaka kubwa ya wafalme ilisababisha mara nyingi jitihada za kubana madaraka yao. Mfano mashuhuri ni Uingereza ambapo wafalme walipaswa kushauriana na bunge ya wakubwa na wawakilishi wa miji kabla ya kukusanya kodi kwa ajili ya vita au kwa shughuli maalumu. Jambo kama hilo halikutokea katika Uingereza pekee lakini katika nchi hiyo bunge lilikuwa taasisi ya kudumu isiyofutwa tena na hivyo kuwa chanzo cha muundo wa ufalme wa kikatiba ambako mamlaka ya mfalme iko chini ya sheria fulani.

Tangu uhuru wa Uholanzi, Marekani na baadaye mapinduzi ya Kifaransa nafasi ya ufalme ilianza kupungua katika Ulaya na kutoka hapo pia katika sehemu nyingine za dunia. Hasa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia falme muhimu kama Ujerumani, Austria-Hungaria, Urusi na Milki ya Osmani zilibadilisha mfumo wa utawala zikawa jamhuri.

Ukoloni na ufalme hariri

Ukoloni wa karne ya 19 ulisababisha kupotea kwa falme nyingi dunani. Mwanzoni wakoloni walitumia mara nyingi wafalme na watemi waliokuwepo kama mawakala wa utawala wao ndani ya koloni. Lakini kadiri walivyounganisha falme mbalimali za kale ndani ya maeneo mapya makubwa yaliyoendelea kuwa mataifa mapya walidhoofisha pia nafasi ya ufalme wa kieneo.

Nchi za Afrika zilipopata uhuru mara nyingi zilijitangaza kuwa jamhuri na kwa njia hiyo falme za kale za Afrika zilifutwa au kupoteza madaraka ya kiutawala na kubaki kwa jina tu kama taasisi za kiutamaduni.

 
Nchi zenye mfumo wa ufalme
nyekundu: Ufalme bila masharti ya kikatiba; chungwa: ufalme chini ya masharti kiasi ya kikatiba; kijani: ufalme wa kikatiba; kijani kibichi: nchi za Jumuiya ya Madola chini ya malkia wa Uingereza; dhambarau: ufalme wa kieneo chini ya ngazi ya jamhuri ya kitaifa

Ufalme leo hariri

Kuna nchi 44 duniani zilizoendela na mfumo wa ufalme hadi karne ya 21. (Linganisha jedwali). Ufalme wa kale ni Japani ambapo kuna wafalme tangu zaidi ya miaka 2000. Pia Ufalme wa Muungano, ambao wafalme wanaendelea karibu mfululizo tangu miaka 1,000 hivi, naDenmark tangu miaka 1,200 hivi.

Nchi

Aina ya ufalme

Cheo

Jina

Maelezo

  Japan Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge Tenno Naruhito Tenno hana madaraka ya kisiasa. Tangu 1945 ni mwakilishi wa taifa pekee. Japani ni ufalme wa kale duniani tangu zaidi ya miaka 2500. Cheo cha tenno chamaanisha „mtawala wa kimbingu“
  Antigua na Barbuda[1] Ufalme wa kikatiba - chini ya usimamizi wa bunge malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Australia[1]
  Bahamas[1]
  Bahrain Ufalme wa kikatiba Mfalme Hamad ibn Isa Al Khalifa Hadi 2002 Emirati, baadaye ufalme; tangu mageuzi ya kisiasa imekuwa ufalme wa kikatiba
  Barbados[1] Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge- Malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Ubelgiji Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge Mfalme Albert II
  Belize[1] Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Bhutan Ufalme wa kikatiba Mfalme Jigme Khesar Namgyel Wangchuck Tangu 1907 hadi 18 Julai 2008 ufalme bila masharti, baadaye ufalme wa kikatiba
  Denmark Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge malkia Margrethe II Mfalme / malkia wa Denmark ni pia mkuu wa nchi ya Greenland na ya Visiwa vya Faroe
  Grenada[1] Elizabeth II wa Uingereza
  Jamaika[1]
  Jordan Ufalme wa kikatiba Mfalme Abdullah II nchi ilianzishwa 1921 na Ufalme wa Maungano
  Kambodia Norodom Sihamoni hadi 1955 na tangu 1993 ufalme
  Kanada[1] Ufalme wa kikatiba malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Eswatini Ufalme bila masharti. Harakati ya kidemokrasia iko njiani Mfalme Mswati III
  Ufalme wa Nchi za Chini (Uholanzi) Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge Malkia Beatrix I Ufalme unajumlisha Uholanzi katika Ulaya na Aruba, Curaçao na Sint Maarten katika Amerika ya Kati
  Lesotho Ufalme wa Kikatiba Mfalme Letsie III Mfalme aliitwa hadi 1965 „Mtemi Mkuu“. Mfalme hana madaraka ya kiserikali wala hatungi sheria
  Malaysia Mizan Zainal Abidin Ufalme wa uchaguzi - Malaysia ina majimbo 13 na kati ya hizo usultani 9; mfalme huchaguliwa kila baada ya miaka 5 masultani 9 kati yao kwa njia ya kubadilishana nafasi; cheo cha mfalme ni Yang di-Pertuan Agong „mtawala mkuu“
  Moroko Ufalme wa kikatiba Mohammed VI
  New Zealand[1] Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Norwei Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge Mfalme Harald V Ufalme wa kujitegema tangu 1905
  Papua Guinea Mpya[1] Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Visiwa vya Solomon[1]
  Uarabuni wa Saudia Ufalme bila masharti Mfalme Salman Ufalme wa Kiislamu uliounganishwa 1931
  Uswidi Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge Carl XVI Gustaf
  Hispania Felipe V Ufalme hadi 1931; tena tangu 1947 bila mfalme chini ya dikteta Franco na tangu 1975 chini ya mfalme
  St. Kitts na Nevis[1] Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge malkia Elizabeth II wa Uingereza
  St. Lucia[1]
  Saint Vincent na Grenadini[1]
  Uthai Ufalme wa kikatiba Mfalme Bhumibol Adulyadej (Rama IX)
  Tonga George Tupou V
  Tuvalu[1] Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge malkia Elizabeth II wa Uingereza
  Ufalme wa Maungano Malkia wa Uingereza ni pia mkuu wa nchi wa „maeneo chini ya taji la Uingereza“ ambayo ni Guernsey, Jersey, Isle of Man halafu kwa maeneo ya ng’ambo ya Ufalme wa Maungano kama vile: Anguilla, Bermuda, Visiwa vya Virgin vya Uingereza, Eneo la Uingereza katika Bahari Hindi, Visiwa vya Cayman, Visiwa vya Falkland, Gibraltar, Montserrat, Visiwa vya Pitcairn, Saint Helena, Visiwa vya South Georgia na South Sandwich na Visiwa vya Turks-na Caicos.
Utemi
  Luxemburg Ufalme wa Kikatiba – chini ya mamlaka ya bunge Mtemi Mkubwa Henri I
  Andorra Ufalme wa kikatiba - mamlaka ya bunge Watawala wa pamoja Askofu Joan Enric Vives i Sicília na Rais Emmanuel Macron Andorra ina watawala wawili wenye madaraka na heshima ya pamoja ambayo ni askofu wa Urgel (Hispania) na Rais wa Ufaransa
  Liechtenstein Ufalme wa kikatiba Mtemi Hans Adam II
  Monaco Albert II
Usultani na Emirati
  Brunei Ufalme bila masharti Sultani Hassanal Bolkiah
  Oman Haitham bin Tariq Al Said
  Katar Ufalme bila masharti Emir Tamim bin Hamad
  Kuwait Ufalme wa kikatiba Sabah al-Ahmad al-Sabah Hadi 1991 ufalme bila masharti, tangu 1996 ina bunge
  Falme za Kiarabu Shirikisho-Ufalme wa kikatiba Rais Chalifa bin Zayid Al Nahyan Ufalme wa uchaguzi: kuna emirati 7; kila emir anaweza kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho lakini hadi sasa amechaguliwa kila safari Emir wa Abu Dhabi ambayo ni sehemu kubwa na tajiri
Eneo la Vatikani
  Vatikani Ufalme bila masharti Papa Fransisko Ufalme bila masharti wa mwisho katika Ulaya; Papa huchaguliwa na mkutano wa makardinali

Tanbihi hariri

  1. 1.00 1.01 1.02 1.03 1.04 1.05 1.06 1.07 1.08 1.09 1.10 1.11 1.12 1.13 1.14 Nchi ya Jumuiya ya Madola ambako malkia ya Uingereza ni mkuu wa dola anayewakilishwa na gavana mkuu