Simba Mdogo (kundinyota)
Simba Mdogo (kwa Kilatini na Kiingereza Leo Minor) [1] ni jina la kundinyota dogo kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia.
Mahali pake
haririSimba Mdogo inapakana na makundinyota ya Simba (zamani Asadi) (lat. Leo), Pakamwitu (Washaki) (lat. Lynx) na Dubu Mkubwa (lat. Ursa Major) ikigusana pia na Kaa (zamani Saratani) (lat. Cancer).
Nyota angavu ya Maliki Junubi (ing. Regulus) iko jirani.
Jina
haririKundinyota hii haikujulikana kwa mabaharia Waswahili wa Kale wala kwa Waarabu au Wagiriki kwa sababu nyota zake ni hafifu sana. Katika enzi ya kale nyota hizi hazikupangwa kuwa sehemu ya makundinyota maalumu yaliyorodheshwa na Klaudio Ptolemaio kando ya Asadi (Leo). Simba Mdogo ni kati ya makundinyota yaliyoanzishwa na mwanaastronomia Johannes Hevelius wa Danzig (Gdansk) mnamo mwaka 1690 BK. Akiwa mpika pombe na mfanyabiashara tajiri aliyeshika kwa muda pia umeya wa mji wake alikuwa hasa maarufu kwa kuangalia, kupima na kuorodhesha nyota pamoja na mke wake Elisabeth Hevelius.
Hevelius aliyelenga kujaza mapengo kati ya makundinyota[2] akiandika kwa Kilatini alichagua jina “Leo Minor” (Simba Mdogo) kwa kuitofautisha na Asadi au Simba Mkubwa. Petrus Plancius aliwahi kubuni hapa kundinyota jipya la Jordanus (mto Yordani) lakini hii haikuendelea na Hevelius badala yake aliona hapa Leo Minor, Leo Minor na Lynx.
Leo Minor - Simba Mdogo iko kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa kimataifa wa Astronomia kwa jina la Leo Minor. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'CVn'.[3]
Nyota
haririSimba Mdogo –Leo Minor ina nyota hafifu tu. Simba Mdogo haina nyota yenye jina la α Alfa kwa sababu Hevelius mwenyewe hakutoa majina kwa nyota zake; kazi hii ilifanywa baadaye na mwanaastronomia Mwingereza Francis Baily aliyesahau kuorodhesha nyota angavu zaidi kwa "α" akanza kutoa herufi za Kigiriki kwa β.
Nyota angavu zaidi ni Praecipua au "46 Leonis Minoris"[4] yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.83 ikiwa na umbali wa miakanuru 98 kutoka Dunia.[5]. Ilipewa jina la Praecipua lenye maana ya "mkuu" kwa sababu ni angavu zaidi.
Tanbihi
hariri- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Leo Minor " katika lugha ya Kilatini ni "Leonis Minoris" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Leonis Minoris, nk.
- ↑ Filling the gaps, tovuti ya Ian Ridpath "Star Tales", iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ The constellations, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Oktoba 2017
- ↑ 46 ni namba ya orodha ya Flaamstedt
- ↑ [1], tovuti ya Ian Ridpath "Star Tales", iliangaliwa Oktoba 2017
Viungo vya Nje
hariri- Constellation Guide: Leo Minor constellation
- Star Tales – Leo Minor
- The Deep Photographic Guide to the Constellations: Leo Minor
- Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 263 ff (online kwenye archive.org)