'

hannes Hevelius
Johannes Hevelius jinsi alivyochorwa na Daniel Schulz wa Danzig
Amezaliwa16111687
Kazi yakemwanaastronomia na mfanyabiashara Mjerumani


Kifaa cha robo-duara (quadrant) kilichoboreshwa na Hevelius kwa upimaji wa nyota

Johannes Hevelius (kwa Kijerumani pia: Hevel; kwa Kipolandi Jan Heweliusz; (16111687) alikuwa mwanaastronomia na mfanyabiashara Mjerumani[1] wa dola-mji Danzig (Gdansk) katika ufalme wa Poland.

Maisha

Alizaliwa katika familia ya wafanyabiashara kwa jina la Johann Hewelcke akatumia kwa maandiko ya kitaalamu umbo la Kilatini la jina lake. Kwa Kipoland jina lake linatajwa kama Jan Heweliusz.

Akiwa mrithi wa biashara ya familia yake kupika bia aliendesha utafiti wa astronomia uliojenga sifa yake katika Ulaya wa wakati wake.

Alipata elimu ya hisabati na nyota kwake nyumbani akaendelea kusoma sheria na hisabati kwenye Chuo Kikuu cha Leyden (Uholanzi).

Baada ya kurudi aliendesha biashara ya bia ya familia yake na kujenga kituo cha kutazama nyota juu ya nyumba yake mjini Danzig. Vifaa vya upimaji vya nyota alivitengeneza mwenyewe. Alinoa lenzi kwa mkono wake na kutengeneza darubini. Lakini alisisitiza kufanya vipimo vya nyota bila matumizi ya darubini kwa sababu alikuwa na mashaka juu ya ubora wa lenzi zilizopatikana[2]

Alichora atlasi ya Mwezi ("Selenographia" ya mwaka 1647) alipotunga ramani za kuonyesha sehemu nyingi za uso wa Mwezi. Majina kadhaa alizobuni yanatumiwa hadi leo, kwa mfano “Alpi za Mwezi”. Kasoko ya Hevelius ilipokea jina lake katika matumizi ya kimataifa.

Mwaka 1679 mwanaastronomia Mwingereza Edmond Halley alimtembelea Danzig akiangalia nyota pamoja na Hevelius na kulinganisha vipimo. Halley alishangaa jinsi gani vipimo vya Hevelius aliyekataa matumizi ya darubini kwa vipimo vyake vililingana kabisa na vyake mwenyewe alivyochukua kwa njia ya kifaa hiki.

Baada ya kifo cha mke wake wa kwanza aliendelea na kazi ya nyota pamoja na mke wake wa pili Elisabeth Hevelius akatunga orodha ya nyota 1,564 iliyokuwa orodha kubwa ya wakati wake. Humo alibuni kundinyota mpya na saba kati ya hizi zinaendelea kutumiwa kati ya orodha ya kundinyota 88 za kisasa za UKIA. Hizi ni: Mbwa wawindaji (Canes Venatici), Mjusi (Lacerta), Simba Mdogo (Leo Minor), Pakamwitu (Lynx), Ngao (Scutum), Sudusi (Sextans) na Mbweha (Vulpecula).

Orodha hii pamoja na atlasi ya nyota (Prodromus Astronomiae) zilitolewa mwaka 1690 na mke wake anayetazamwa kuwa mwanastronomia wa kike wa kwanza anayejulikana.

Tanbihi

  1. Hevelius anatajwa mara nyingi kuwa Mpoland; alitoka katika familia wa raia Wajerumani wa mji wa Danzig iliyokuwa sehemu ya kujitawala wa Milki ya Poland-Lithuania. Idadi kubwa wa wakazi walikuwa Wajerumani kiutamaduni katika kipindi kile kabla ya kuanzishwa kwa utaifa wa baadaye. Linganisha tovuti ya Galileo Project
  2. Hevelius and the Firmamentum Sobiescianum, tovuti ya Ian Ridpath "Star Tales", iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu mwanasayansi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Johannes Hevelius kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.