Transkei ilikuwa Bantustan ya kwanza ya Afrika Kusini iliyotangazwa kuwa nchi ya pekee wakati wa siasa ya Apartheid (ubaguzi wa rangi wa kisheria).

Bendera ya Transkei (bantustan)
Ramani ya Afrika Kusini kabla ya mwaka 1994; rangi nyekundu inaonyesha Transkei.
Transkei, mwaka 1978

Eneo lake lilikuwa km² 43,800 na idadi ya wakazi takriban milioni 3.2. Mji mkuu ulikuwa Umtata (au Mthatha).

Neno Transkei lamaanisha "ng'ambo ya mto Kei". Pamoja na Bantustan nyingine ya Ciskei ("upande huu wa mto Kei") ilipangwa kuwa bantustan kwa ajili ya Waxhosa. Transkei ilikuwa na takriban nusu ya Waxhosa wote, ingawa hali halisi wengi walikaa na kufanya kazi Afrika Kusini ila hawakuwa na haki za wananchi.

Transkei ilipewa madaraka ya kujitawala mwaka 1963, ikatangazwa kuwa nchi huru tarehe 26 Oktoba 1976 lakini hakuna nchi yoyote duniani iliyoitambua kama nchi ya pekee.

Rais wa Transkei alikuwa chifu Kaizer Daliwonga Matanzima hadi 1987 alipopinduliwa na mkuu wa jeshi lake Bantu Holomisa. Kaizer Mantanzima alikuwa mpwa wake Nelson Mandela lakini hakukubaliana na siasa ya ANC. Akajaribu kwa muda kuwa na siasa mbali na Afrika Kusini lakini alishindwa kwa sababu serikali yake ilitegemea ruzuku kutoka serikali ya Pretoria.

Wakati wa mwisho wa apartheid mwaka 1994 Transkei iliunganishwa tena na Afrika Kusini mpya.

Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika Kusini bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Transkei kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.