Tshimanga Kalala Assosa (4 Aprili, 1949) ni mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- Tanzania. Alifahamika zaidi kwa kuwa miongoni mwa waimbaji wakubwa wa bendi ya Marquis Original na bendi yake binafsi Orchestra Mambo Bado.

Tshimanga Assosa
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaTshimanga Kalala Assosa
Pia anajulikana kamaMtoto mzuri
Amezaliwa4 Aprili 1949 (1949-04-04) (umri 74)
Uvira, Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Kazi yakeMpiga solo
Ameshirikiana naMarquis Original

Historia hariri

Wasifu hariri

Tshimanga Kalala Assosa ni mwanamuziki maarufu aliyewahi kupiga muziki katika bendi kubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za Negro Success, ]Les Kamalee, Lipua Lipua na Fuka Fuka. Assosa ni mwenye kipaji cha kutunga na kuimba nyimbo za muziki wa dansi pia ni kiongozi wa bendi ya Bana Maquis iliyopo jijini Dar es Salaam. Kwa hali isiyokuwa ya kawaida, Tshimanga Assosa amekuwa akikataa ofa lukuki za kwenda ‘kula maisha’ Ulaya na Marekani na kuamua kuishi katika Jijini la Dar es Salaam nchini Tanzania. Akiwa katika bendi hizo alishirikiana wanamuziki nguli akina Bavon Marie Marie, Nyboma Mwandido, Pepe Kalle na Kiamuangana Mateta Wazola Mbongo ‘ Verckies’.

Kuzaliwa, elimu na muziki hariri

Assossa alizaliwa katika mji wa Kamina uliopo Jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo tarehe 4 Aprili, 1949. Alipata elimu ya Sekondari katika Shule iliyojulikana kama Charles Ruangwa hapo Kamina. Assosa alianza kuimba akiwa bado mdogo na kwamba aliyejipeleka mwenyewe katika kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Baram huko Kamina ambako Mapadri walimsaidia kumfundisha muziki. Pamoja na juhudi zake hizo, Baba yake mzazi kamwe hakutaka mwanaye ajitumbukize katika muziki na kumtaka afuate masomo yake shuleni.

Baada kumaliza kidato cha nne, Baba yake alimpeleka Chuo cha Ufundi cha Kamina. Assosa Muziki ulikuwa ndani ya damu yake, hivyo kila siku baada ya kutoka Chuoni alikuwa akienda kuangalia mazoezi ya bendi iliyokuwepo hapo Kamina ya Super Gabby. Mazoezi hayo yalimtia hamasa kubwa ya kupenda muziki. Siku moja aliomba apewe nafasi kujaribiwa kuimba katika bendi hiyo. Assosa alikubaliwa akaingia stejini kuimba, lakini kabla hajamaliza kuimba ghafla Baba yake alitokea ukumbini humo na kumcharaza viboko. Pamoja na makatazo yote hayo, hatimaye baba yake mwisho wake alikubali ombi la mwanaye baada ya kubaini kuwa hashikiki wala habadiliki kitabia, akamruhusu afanye muziki aupendao.

Safari kamili ya muziki hariri

 
Assossa enzi za Mambo Bado (mtoto mzuri).

Mwaka 1969 Tshimanga alikwenda Kinshasa kutafuta maisha. Kwa bahati nzuri alikutana na mwanamuziki Bavon Marie Marie na akampeleka kwa mmiliki wa bendi moja katika jiji hilo aliyejulikana kama Didi Kalombo. Assosa aliitumia vyema nafasi hiyo ya kujaribiwa sauti. Mmiliki huyo alimkubali, hapo ikawa chanzo kuanza kutimiza ndoto zake kwa kupata ajira katika bendi hiyo. Assosa anazikumbuka changamoto alizokutana nazo za kuwakuta wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa watanashati kuliko yeye, mavazi mazuri zikiwemo suti na wote walikuwa wang’aavu usoni wakitumia vipodozi (mkorogo). Pamoja na hayo, sauti yake ndiyo iliyomuokoa na kupewa heshima kama wanamuziki wengine.

Baadaye Negro Success kiongozi wake kufariki Bavon Marie Marie kwa ajali ya gari, bendi hiyo iliteteleka na hatimaye ikafa. Mwaka 1974 Assosa alikutana na Nyboma Mwandido na kumueleza kwamba anatakiwa na mmiliki wa Bendi ya Lipua Lipua, aliyejulikana kwa jina Kiamuangana Mateta Wazo la Mbongo "Verckies". Alipofika huko alitakiwa kujaribu kuimba sauti ya Pepe Kalle, ambaye alikuwa amekwisha ondoka. Hata hivyo, hakujua ujasiri aliupata wapi siku hiyo pale alipomtamkia mmiliki huyo kwamba hayuko tayari kuimba sauti ya mtu, bali aachiwe aimbe sauti yake halisi ambayo baadaye uongozi ulimkubali.

Akiwa huko, aliungana na wanamuziki wengine wakali akina Chizunga Ricks (Solo), Mutembu Chibau, Basikita na Kayembe waliokuwa wamemtangulia katika bendi hiyo. Wakiwa na Lipua Lipua waliibuka na vibao vikali vilivyotisa jiji la Kinshasa vya Mombasa, Nikibwe na Amba. Mwaka 1975 bendi hiyo iliingia katika mgogoro kati ya mmiliki wa Bendi hiyo na wanamuziki. Aliamua kuondoka na kwenda kujiunga na Bendi ya Les Kamalee. Akiwa na Les Kamalee walitoka na nyimbo ambazo hadi hivi sasa bado zinatamba katika ulimwengu wa muziki za Abisina, Masuwa, Aigi na nyingine nyingi.

Wanamuziki wa Bendi hiyo baada ya mafanikio yao ya ghafla, walilewa sifa na kujiamini kupita kiasi. Walilipwa maslahi murua, walinunua vyombo vyao vya muziki na magari ya kubebea vyombo hivyo. Mbwembwe zikazidi na kusababisha kusahau wajibu wao katika kazi. Bendi ya hiyo kufa mwishoni mwaka 1975. Mwenye bahati habahatishi, Assosa alikaribishwa katika Bendi ya Fuka Fuka iliyokuwa ikiongozwa na Mule Chibauma. Akiwa na Bendi hiyo mwaka 1978 ilifanya ziara hapa nchini Tannzania. Fuka Fuka ilipoingia Dar es Salaam ilikuwa na nyimbo zake mpya za Bitota, Lomeka, Baba Isaya, Papii na Funga Funga ambazo anazielezea kwamba zailiwaduwaza wapenzi wa muziki wa jiji la Dar es Salaam wakati huo.

Bendi hiyo baadaye iliingia mkataba wa kupiga muziki kwa miezi sita na Chama cha mateksi Dereva cha Tanzania Transport, Tax and Services (TTTS) ambacho pia kilikuwa kikimiliki ukumbi wa Mlimani Park. Baada ya kumaliza mkataba Fuka Fuka waliondoka kurejea kwao wakipitia Nairobi nchi Kenya na Kampala huko Uganda. Wakiwa Kampala kwa bahati mbaya nchi hiyo ilikuwa imeingia vitani, ikipigana na Tanzania mwaka 1979. Vita hivyo viliiwaathiri kwa kiasi kikubwa kwani wakiwa Uwanja wa ndege wa Entebbe wakisubiri kurejea kwao, vurugu za vita ziliwakaribia, wao wakakimbia wakiviacha vyombo vyote vya muziki uwanjani humo ilihali kila mmoja akitafuta njia ya kunusuru maisha yake.

Mwaka 1981 akiwa kwao Kongo, Assosa alifuatwa na mfanyabiashara toka Tanzania aliyemtaja kwa jina la Joseph Mwakasala ili kuja Tanzania kupiga muziki katika bendi ya Mlimani Park Orchestra kwa mkataba wa miezi sita. Akiwa Mlimani Park Orchestra alikutana na wakali wa muziki wa Tanzania, akina Muhidini Maalim Gurumo, Michael Enoch, Abel Balthazar, Joseph Bartholomew Mulenga na Cosmas Tobias Chidumule. Baada ya kumaliza mkataba mwaka 1982, Tshimanga Kalala Assosa alichukuliwa na mzee Kitenzogu Makassy katika bendi yake ya Orchestra Makassy alikodumu hadi mwaka 1986.

Akiwa hapo alitoa wimbo ulioshika chati wa Athumani. Mwaka huo huo aliamua kuanzisha bendi yake ya Orchestra Mambo Bado, akatoka na wimbo wa ‘ Bomoa Tutajenga kesho’ Wimbo huo ulitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu kwamba haukuwa na maadili mema. Bendi hiyo ilijengewa mizengwe na kusababisha kasambaratika baada ya muda mfupi. Assosa alichukuliwa na bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa na Chinyama Chiyaza kwa wakati huo mwaka 1987. Alipigia bendi ya Maquis hadi ilipo sambaratika ikipiga kayika ukumbu wa Lang’ata, Kinondoni miaka ya 1990. Akiwa hapo wapenzi wa Maquis Original walimpa jina la ‘mtoto mzuri’ kufuatia utanashati wake.

Baadaye alichukuliwa na mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Paul Kyala kuimarisha bendi ya Legho Stars. Akiwa na bendi hiyo alifyatua vibao vya Francisca, Afra, Moseka na vingine vingi. Baada ya kumaliza mkataba aliungana na wanamuziki aliokuwa nao Maquis du Zaire ambao walikuwa wameanzisha bendi ya Bana Maquis. Anawataja akina Kasongo Mpinda ‘Cryton’, Mukumbule Lulembo ‘Parashi’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’. Hadi sasa bado yuko na bendi hiyo ya Bana Maquis.

Tazama pia hariri

Viungo vya Nje hariri


  Makala hii kuhusu mwanamuziki fulani wa Afrika bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tshimanga Assosa kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.