[1] Alain Kahanga Dekula (anajulikana kama Vumbi; amezaliwa Lemera, Wilaya ya Uvira, Mkoa wa Kivu ya Kusini, 2 Aprili, 1962) ni mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - Tanzania. Alifahamika zaidi kwa kuwa miongoni mwa wapigaji gitaa la solo wakubwa wa bendi ya Marquis Original.

Dekula Kahanga
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaAlain Dekula Kahanga
Pia anajulikana kamaVumbi
Amezaliwa2 Aprili 1962 (1962-04-02) (umri 62)
Uvira, Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Kazi yakeMpiga solo
Ameshirikiana naMarquis Original

Historia hariri

Maisha na muziki hariri

 
Dekula Kahanga na Maneno Uvuruge walipokutana ndani ya jiji la Stockholm 13/04/2017. Awali walifanya kazi ote katika miaka ya 1980.

Dekula Kahanga Vumbi ni mpenzi mkubwa wa kupiga gitaa, lakini baba yake hakupenda kabisa apige gitaa, lakini bahati nzuri alikulia kwa bibi yake katika mji wa Uvira, mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako alikuwa na uhuru zaidi na akaanza kwa kutengeneza magitaa yake, ambalo lilikuwa likivunjwa kila baba yake alipokuwa akija kumtembelea bibi yake. Jirani na alipokuwa akiishi kulikuweko na bar inaitwa Sikiya sosi ambapo palikuweko na bendi ikiitwa Gramick Jazz, bendi iliyopitiwa na wanamuziki wengi waliokuja Tanzania akiwemo Dr. Remmy.

Alikuwa akisikiliza muziki ukipigwa katika hiyo bar na yeye akawa anafuatisha kwenye gitaa la kutengeza mwenyewe la nyuzi tatu, hatimaye bibi yake akamnunulia gitaa dogo la nyuzi nne ambalo alikuwa naaenda nalo mpaka shule, ambapo mwalimu wake siku nyingine alikuwa akimwita awatumbuize wanafunzi wenzie. Hatimaye akakutana na jamaa aliyekuwa akipiga katika bendi iliyokuwa ikimilikiwa na mapadri, akawa anamnunulia sigara huyu jamaa nae akaanza kumfundisha chords mbalimbali za kupiga gitaa.

Aliendelea vizuri hatimae akajiunga na bendi hiyo ya mapadri iliyoitwa Kyalalo Band akiwa mpiga rhythm. Wanamuziki wa Kyalalo hawakuruhusiwa kujiunga na bendi zilizo kuwa zinapiga muziki kwenye bar, wala bendi yenyewe kwenda kupiga kwenye bar, kulikuweko na ukumbi mkubwa wa kanisa na hapo ndipo walipofanya mazoezi na maonyesho, lakini baadae Vumbi akajiunga na bendi Bavy National tena kama mpiga rhythm, na hapo akakutana na mwimbaji Issa Nundu ambaye alikuwa anafanya hospitali na jioni kujiunga na bendi, hatimaye Kyanga Songa ambaye kazi yake ilikuwa Bwana Shamba nae alijiunga nao.

 
Wa pili toka kulia na shati jeusi Vumbi, wapili toka kushoto na suruali nyeusi Issa Nundu.

Katika kipindi hicho wakazi wa Kongo ya Mashariki, ambako kunazungumzwa Kiswahili, walikuwa wakisikiliza na kuzijua bendi nyingi kutoka Afrika ya Mashariki, bendi kama Tabora Jazz Band, Mangelepa, Simba wa Nyika, Mlimani Park zilisikilizwa sana, na nyimbo kama Kassim ilikuwa nyimbo maarufu wakati huo na hivyo ikawa ndoto ya Vumbi kuwa lazima siku moja waende huko unakotoka muziki mtamu huo ili nae aweze kushiriki.

Safari ya kwenda Tanzania, Chamwino na Marquis Original hariri

 
Orch. Maquis Original 1987 Wapiwapi Chang'ombe Bar,LR ni:Mbuya Makonga "Adios", Dekula Kahanga"Vumbi", Mpoyo Kalenga na William Maselenge. Alie chuchumaa ni Juma Choka.

[[Picha:Vumbi Kijana 1989.jpg|left|thumb|Dekula Kahanga "Vumbi" baada ya mazoezi na bendi ya Maquis Original ndani ya Lang'ata Social Hall Kinondoni Dar-Es-Salaam tarehe 10/Oktoba/1989.

Kipindi hiki ndio walirekodi nyimbo, Mashoga, Tipwatipwa, Hali Ngumu, Ossa, Marusu, Mangolibo, Kisebengo. Zote hizo alipiga gitaa la solo Vumbi.

Katika kipindi hicho Kyanga Songa na Issa Nundu waliondoka kwenye bendi yao ya Bavi National na kuelekea Tanzania. Kuondoka kwao, bendi ikatetereka sana, lakini nae wakati huo akawa anahamu sana ya kuja Afrika Mashariki. Bahati nzuri mtu mmoja Alida Shanga akamjia akiwa ametumwa na Marehemu Mzee John Luanda aliyekuwa anamiliki Chamwino Jazz kuja kutafuta wanamuziki toka Kongo, nae akawachukua na wakatua Tandale jijini Dar es Salaam, na siku waliofika tu na wakaanza mazoezi siku hiyo hiyo.

Wakiwa vijana bado yeye na wenzie watatu walikuja wakiwa na staili ya kuimba na steji show ambayo wakati huo iliitwa sarakasi, na pia wao ndo kilikuwa kikundi cha kwanza kuanza kurap katikati ya nyimbo. Waimbaji wakiwa ni Sisko Lunanga, Fanfan Bwami, na mwenzao mmoja Baposta Kilosho ambaye hatimaye alirudi Kongo. Rekodi ya kwanza ilimuacha Julius Nyaisanga akishangaa vituko vya vijana hawa. Katika bendi ya Chamwino wakati huo wapiga magitaa walikuwa Vumbi Dekula, Kazembe wa Kazembe (huyu alikuwa Msukuma ambaye aliishi kwa muda Kongo na alikuwa mpiga gitaa hodari sana), na Mzee Albert, na hatimae wakamchukua Muhidin ambae alikuwa mpiga bezi wa Dr Remmy.

 
Orch. Maquis Original 1987 Wapiwapi Chang'ombe Bar, kutoka kulia ni: Mbuya Makonga "Adios", Dekula Kahanga"Vumbi", Mpoyo Kalenga na William Maselenge. Alie chuchumaa ni Juma Choka

Siku moja walienda kuomba kupiga na Maquis Original (lifti), wakati huo wakipiga nyimbo za kopi, nyimbo kama Mario, Maze na kadhalika, hivyo wakazipiga hizo na watu wakafurahi sana na kuwatuza fedha nyingi, wakachanganyikiwa maana bendi yao ya Chamwino ilikuwa haina mshahara na si mara moja walitembea kwa miguu toka Buguruni hadi Tandale kwa kukosa mapato. Japo wakati huo walikuwa wadogo kwa umri na hata umbo walifika mahala marehemu Kasheba alikuwa anawaita ‘Vimario’, upigaji wao ulikuwa mzuri sana. Nguza aliwashauri wawe wanakuja kupiga kabla Maquis hawajaanza kupiga.

Hivyo wakaamua kuacha Chamwino, na wakawa wanasindikizana na Maquis, hili lilimuudhi aliyewaleta na siku moja wakiwa Silent Inn, maafisa wa Uhamiaji walikuja kuwachukua wakalazwa Central Police na kisha kupelekwa gereza la Keko. Wakiwa huko walimwandikia Mzee Luanda kuwa wanarudi Chamwino, basi wakaachiwa na kurudi kusuka upya Chamwino Jazz. Lakini hawakukaa muda mrefu Mzee Makassy akaja kuwaomba waingie katika bendi yake, wenzake waimbaji wakaenda yeye akabaki Chamwino, lakini muda si mrefu Nguza akamwambia aandike barua ajiunge na Maquis.

Nae akafanya hivyo na ndio kujiunga rasmi na Maquis kama mpiga gitaa la solo la pili. Aliwakuta wanamuziki kama Maneno Uvuruge, Omari Makuka, Keppy Kiombile, Ilunga Lubaba, William Maselenge na wengine wengi. Aliendelea kupiga solo la pili hadi siku moja bendi ilikuwa inapiga maeneo ya Ukonga, kwa kawaida Mzee Lubaba alikuwa anapiga kuanzia saa tatu mpaka saa sita, na kisha Nguza Viking akiingia na kuendelea . Siku hiyo Nguza hakuonekana Vumbi akaweza kupiga nyimbo zote za Nguza, na kesho yake akaambiwa afike ofisini akasainishwa rasmi mkataba wa kuwa mwanamuziki wa Maquis. Baada ya muda mfupi Nguza akaacha bendi.

Na baada ya hapo walirekodi ule wimbo maarufu wa Makumbele, solo ya wimbo huu ilikuwa awali ikipigwa na Mzee Lubaba, lakini afya ya mzee Lubaba ilianza kuzorota nae akawa anawafundisha nyimbo zake wanamuziki wengine, wimbo wa Makumbele alifundishwa Makuka na akawa anaupiga katika maonyesho mbalimbali, lakini wakati wa kutaka kurekodi kamati ya uongozi ya Maquis iliamua Vumbi aufanyie mazoezi na aurekodi. Kurekodi kwa album ya Makumbele ilitokana na safari ndefu ya bendi ambayo ilichukua miezi mitatu katika mikoa ya Ziwa, hivyo bendi iliporudi Dar ilikuta sifa ya bendi imepungua, hivyo walirekodi album ya Makumbele iliyokuwa na nyimbo kama Tipwatipwa, Ngalula na Makumbele, sifa ya bendi ikarudi juu tena kwa mara nyingine. Na ni wakati huo ambapo bendi ilihamia katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni.

Tazama pia hariri

Viungo vya Nje hariri

  Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dekula Kahanga kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Marejeo hariri

  1. "DEKULA KAHANGA ‘VUMBI’ ANAYEMILIKI BENDI YAKE SWEDEN.". michuzi2.rssing.com. Iliwekwa mnamo 2024-01-13.