Ushairi wa Christopher Richard Mwashinga

Ushairi wa Christopher Richard Mwashinga unapatikana katika vitabu vingi alivyoviandika kwa Kiingereza[1] na Kiswahili[2].

Makala hii inatoa historia fupi ya ushairi wake wa Kiswahili.

Historia ya ushairi

hariri

Christopher Mwashinga, aliyezaliwa tarehe 9 Januari 1965, ni mshairi kutoka nchi ya Tanzania, Afrika Mashariki. Amekuwa akiandika na kughani mashairi ya Kiswahili tangu mwaka 1978 alipokuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya msingi ya Ngare-Nairobi iliyoko Siha Magharibi, katika wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, nchini Tanzania.

Uandishi wake wa mashairi ya Kiswahili umegawanyika katika vipindi vinne vikubwa: 1978-1984; 1985-1991; 1999-2018, 2018 hadi leo.

Kipindi cha kwanza: 1978-1984

hariri

Kipindi cha kwanza kinaanzia mwaka 1978 na kutambaa hadi mwaka 1984. Ingawa Mshairi alihitimu masomo yake ya elimu ya msingi mwaka 1981 katika Shule ya Msingi Ngare-Nairobi iliyoko Siha Magharibi, mkoani Kilimanjaro, bado aliendelea kuandika mashairi hata baada ya kumaliza masomo yake. Alianza kuandika mashairi ya Kiswahili akiwa na umri wa miaka kumi na mitatu hivi, wakati huo akiwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule hiyo ya Msingi ya Ngare-Nairobi. Wakati huo aliandika mashairi mengi, lakini kwa kuwa hakuwa na njia bora ya kuyahifadhi, yote yalipotea. Yeye mwenyewe anakumbuka sehemu tu ya beti za baadhi ya mashairi ya kipindi hiki cha kwanza. Mfano mzuri ni shairi moja refu lililozungumzia habari za kijana mmoja wa kufikirika aliyeitwa Hasani ambaye alichaguliwa kwenda masomoni Songea, Tanzania ya kusini na baadaye akapatiwa nafasi ya kuendela na masomo ya elimu ya juu nchini Japan. Mistati miwili ya ubeti mmojawapo anaoukumbuka ulikuwa na maneno yafuatayo:

Mambo yakawa ni mambo, sijui apewe nini
Akachaguliwa ng’ambo, miaka miwili Japani.

Mashairi yote aliyoyatunga wakati huo yalihadithia mambo ya kijamii au kujadili masuala ya kisiasa. Hakuandika shairi lolote la kidini.

Kipindi cha pili: 1985-1991

hariri

Kipindi cha pili cha utunzi wa mashairi ya Christopher Mwashinga kilianza rasmi mwezi Desemba mwaka 1985 wakati akiwa bado anaishi Kilimanjaro Magharibi. Mwezi Aprili mwaka huo wa 1985 alipokuwa nyumbani kwao Uyole, Mbeya akitembelea wazazi na ndugu zake, alisikia kwa mara ya kwanza ujumbe wa Kiadventista na kuupokea. Aliporudi mkoani Kilimanjaro, alibatizwa katika Kanisa la Waadventista wa Sabato, Majengo, Moshi mnamo tarehe 18 Mei, 1985. Baada ya kubatizwa aliendelea kuishi katika eneo la Mpodoni huko huko Siha Magharibi. Akitokea Mpodoni, aliendelea kuhudhuria ibada katika kundi la Matadi SDA lililokuwa chini ya kanisa la Majengo Moshi wakati huo.

Kama miezi saba tangu alipojiunga na kundi hili la Matadi SDA, idara ya vijana ya kundi iliandaa tamasha la vijana kama sehemu ya programu maalumu za kufungia mwaka. Hapo ndipo kiongozi wa vijana wakati huo, Bw. Yohana Jackson, alipomwomba Christopher Mwashinga aandike shairi litakaloimbwa wakati wa tamasha hilo, naye akakubali. Kwa hiyo siku ya Ijumaa, Desemba 27, 1985 Christopher Mwashinga, wakati huo akiwa na umri wa miaka ishirini, alitunga shairi la beti nane aliloliita,”Tunapomaliza Mwaka.” Shairi hili liliimbwa kesho yake, Jumamosi, Desemba 28, 1985 wakati wa tamasha lililofana sana la vijana wa kundi hilo. Hilo ndilo lililokuwa shairi lake la kwanza alilotunga lenye maudhui ya kidini. Ubeti wa saba wa shairi hilo una maneno yafwatayo:

Katika yetu maombi, Mungu ulitusikia,
Na tulipotenda dhambi, ulitusamehe pia,
Mkutano wa makambi, ulitufanikishia
Tunapomaliza mwaka, Mungu tunakushukuru.

Kuandikwa kwa shairi hili la kwanza la kiroho ndiko kulikopiga kipenga cha kuanzisha rasmi enzi mpya ya utunzi wa mashairi ya Kikristo ambayo Mwashinga ameidumisha kwa kipindi cha zaidi ya miaka thelathini iliyofuata. Baada ya mwanzo huu wa enzi mpya uliotokea kama ajali, akiwa bado anaishi Kilimanjaro Magharibi, Mwshinga aliendelea kutunga mashairi ya Kikristo ambayo mengine aliwapa rafiki zake kama zawadi. Kwa bahati mbaya mashairi hayo yote yalipotea na huenda hayatapatikana tena. Mwaka uliofuata, siku ya Jumapili, Machi 10. 1986, Christopher Mwashinga alisafiri toka Kilimanjaro Magharibi kulekea nyumbani kwao Uyole, Mbeya ambako aliwasili kesho yake Machi 11, 1986. Aliamua kuhamishia makao yake makuu Mbeya kwa minajili ya kuendelea na masomo yake ya sekondari. Akiwa Mbeya, aliendelea kutunga mashairi ya Kikristo kwa lugha ya Kiswahili. Kwa mfano Julai 14, 1986 alitunga shairi aliloliita, “Kazi Ilo Mbele Yetu.” Shairi hili liliimbwa katika mkutano wa makambi ya Waadventista wa Sabato uliofanyika mwezi Agosti katika eneo la Iganzo, Mbeya. Shairi hili, ambalo ni moja ya mashairi yake machache ya awali yaliyosalia, liliimbwa na akina dada watatu, yaani Eva, Ellen na Jane ambao ni mabinti wa mzee Rupia, aliyekuwa Mwinjilisti maarufu wa Vitabu nchini Tanzania wakati huo.

Baada ya kuhitimu masomo yake ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Igawilo, Mbeya mwaka 1988, Mwashinga alifaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea mwezi Julai 1989. Akiwa shuleni Songea, aliandika mashairi kadha wa kadha ya Kikristo ikiwa ni pamoja na shairi lake liitwalo, "Yesu Rafiki wa Watoto,” lililoimbwa katika mkutano wa makambi ya Songea mjini Agosti 25, 1989. Mwezi mmoja tu kabla ya mwisho wa mwaka huo, yaani siku ya Alhamisi, Novemba 30, 1989, ndipo alipoandika shairi lake linalojulikana na wengi nchini Tanzania. Shairi hili la beti 44, aliliita, ”Nimeguswa na Upendo wa Yesu.” Shairi la mwisho kabisa alilotunga akiwa Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea, ni shairi fupi la beti tatu aliloliita, ”Yapendeza Kuonana,” Shairi hili aliliambatisha na barua yake ya mwisho kwa wazazi na ndugu zake waliokuwa nyumbani kwao Uyole, Mbeya wakimsubiri awasili nyumbani baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha sita. Shairi hili lilitungwa Jumapili, Mei 5, 1991.

Kufuatia kuhitimu masomo yake ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea, Mwashinga aliondoka na kurudi nyumbani kwao Uyole, Mbeya. Kwa muda wote uliobaki wa mwaka 1991, hakuandika shairi lolote la Kiswahili. Sababu inaweza kuwa kwamba wakati huu akiwa Mbeya, alielekeza nguvu zake nyingi katika kuandika na kuchapisha mashairi ya Kikristo kwa lugha ya Kiingereza. Kwa mfano mwezi Oktoba mwaka huo huo aliandika shairi lake la kwanza la Kiingereza liitwalo ”The Glorious Deliverance,” ambalo lilichapishwa katika gazeti lililokuwa likitoka kila Jumapili liitwalo Sunday News la Oktoba 6, 1991. Mashairi yake mengine mawili ya Kiingereza yalifuata haraka, yaani ”To the Pilgrims,” lililochapishwa Januari 19,1992 na "Our Doomed World" lililochapishwa Mei 10,1992. Hadi Januari 8, 1993 Mwashinga alipoondoka Mbeya kwenda Arusha kujiunga na Chuo cha Kiadventista Tanzania (Tanzania Adventsit College) kusomea masomo ya uchungaji na theolojia, hakuna ushahidi kwamba aliandika shairi lolote jingine la Kiswahili ambalo linafahamika. Hata hivyo, kuanzia mwaka 1993 alipoanza masomo hapo Tanzania Adventist College hadi mwezi Julai 1997 alipohitimu masomo yake ya shahada ya kwanza katika theolojia kutoka katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Baraton, nchini Kenya, alikuwa ameshachapisha mashairi ya Kikristo zaidi ya kumi, yote kwa lugha ya Kiingereza. Mashairi hayo yalichapishwa na Sunday Nation,Kenya,[3] nchini Kenya na Literature Evangelist nchini Marekani [4] Ni jambo la kushangaza kwamba kwa muda huo wote hakuandika shairi lolote la Kiswahili ingawa kuna ushahidi kwamba mapenzi yake kwa mashairi ya Kiswahili hayakuzima. Mara kwa mara pale alipoalikwa kuhubiri au kuhutubia makundi ya vijana wa Kikristo, alizoea kughani mashairi yake ya zamani na hasa shairi liitwalo ”Nimeguswa na Upendo wa Yesu.” Kwa mfano, baada ya kurudi Tanzania mwaka 1997 na kuanza kazi yake kama Mkurugenzi wa Chaplansia wa Jimbo la Mashariki mwa Tanzania katika Kanisa la Waadventista wa Sabato bado aliendelea kughani mashairi yake mara kwa mara.

Kipindi cha tatu: 1999-2018

hariri

Kipindi cha tatu cha ushairi wa Christopher Mwashinga kilianza mwaka 1999 na kuimarika zaidi miaka kadhaa baadaye pale alipojiunga na Chuo Kikuu cha Andrews, nchini Marekani mwaka 2005. Kabla ya mwaka 2009, ukiacha mashairi yake ya Kiingereza yaliyochapishwa katika magazeti mbalimbali pamoja na diwani kadhaa zilizochapishwa nchini Marekani, [5] kazi zake nyingi hazikuwa zimechapishwa. Jambo hili lilionesha uwezekano wa kazi zake kupotea kabisa. Kwa hiyo, ilipofika mwaka 2009, Christopher Mwashinga mwenyewe aliamua kuanza mradi mkubwa na wa muda mrefu wa kuchapisha maandiko yake ya awali ya Kiingereza na Kiswahili. Huu ulikuwa ni mkakati maalumu wa kuyahifadhi maandiko yake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Wakati huu ndipo alipoamua pia kuchapisha mashairi yake ya Kiswahili kwa malengo hayo hayo. Kwa hiyo, mwezi Februari mwaka 2013 wakati kitabu chake cha kwanza cha Kiswahili kiitwacho Barua na Mashairi kilipochapishwa nchini Marekani, mashairi yake ya Kiswahili yapatayo arobaini na sita yalichapishwa kwa mara ya kwanza kabisa. Kazi hii ilifuatiwa na kitabu kingine kiitwacho Sauti Toka Ughaibuni: Mashairi ya Matumaini (2014) ambacho kilihusisha mashairi yote yaliyotokea katika Barua na Mashairi pamoja na nyongeza ya mashairi mengine mapya ambayo yalichapishwa kwa mara ya kwanza. Sauti Toka Ughaibuni kilifuatiwa na kitabu kingine cha mashairi yake kiitwacho Kilele cha Tumaini (2016) ambacho kilihusisha mashairi mapya ambayo hayakuwahi kuchapishwa mahali popote na wakati wowote kabla ya wakati huo. Kuchapishwa kwa vitabu hivi kulifungua pazia la enzi angavu ya mashairi ya Kikristo kwa lugha ya Kiswahili. Katika kipindi cha miaka ya karibuni kumekuwa na mrejesho chanya kutoka kwa wapenzi wa tungo za Mshairi huyu katika nchi mbalimbali, hasa Marekani na Tanzania. Diwani yake iitwayo Tumaini Lenye Baraka ambayo inajumuisha mashairi yake yote ya Kiswahili aliyoyaandika katika kipindi cha miongo mitatu, 1985-2016 ilichapishwa mwaka 2017. Hii ilifuatiwa na diwani nyingine iitwayo Sauti ya Faraja na Matumaini iliyochapishwa mwaka 2018. Mashairi yake mengine yamechapishwa katika gazeti la Sauti Kuu chini Tanzania. [6]. Mengine somwa au kughanwa katika mikutano mbalimbli ya kijamii na kidini katika nchi mbalimbali duniani. Kwa mfano shairi lake maarufu lijulikanalo kama "Njozi Haiwezi Kufa" liliwasilishwa katika Kongamano la Kimataifa la Vijana Afrika (Pan African Youth Congress) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Baraton, nchini Kenya, Desemba 2019 [7]. Vilevile mashairi yake yametumika katika mikutano mingine nchini Tanzania [8]. Miaka ya karibuni, vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini Tanzania vimekuwa vikitumia mashairi yake katika vipindi vyao ili kufikisha ujumbe wa matumaini kwa watazamaji na wasikilizaji wao. Kwa mfano kituo kikubwa cha televisheni cha Hope Channel Tanzania katika kipindi chao cha Mbiu ya Kusini na Morning Star Radio [9].

Kipindi cha Nne: 2018 hadi sasa

hariri

Kipindi cha nne. Kipindi cha nne cha ushairi wa Christopher Mwashinga kinaanzia mwaka 2018 na kuendelea hadi sasa. Ingawa kwa namna moja au nyingine kipindi hiki kinaweza kuonekana kama ni mwendelezo wa kipindi cha tatu, hata hivyo kuna mambo makubwa matatu yaliyojitokeza kuanzia mwaka huo yanakifanya kipindi hicho kuwa tofauti na vipindi vilivyotangulia.

(1) Mashairi ya watoto. Mwashinga alianza rasmi kuandika mashairi ya watoto mwezi Januari mwaka 2018. Wakati wa safari yake ya ndege kati ya London, Uingereza na Chicago, Marekani, akiwa angani aliandika mashairi mawili ya Watoto ambayo ni: “Kipepeo” na “Miguu Midogo.” Mashairi haya yalitokea katika kitabu chake cha kwanza cha mashairi ya watoto kiitwacho Mdomo Mmoja, Masikio Mawili kilichochapishwa nchini Marekani mwaka 2019. Lifuatalo ni shairi liitwalo “Kipepeo,” ambalo lilikuwa shairi la kwanza aliloliandika wakati wa safari hiyo.

Mtazame kipepeo, jinsi anavyopepea,
Kazaliwa leoleo, lakini anatembea,
Nampenda kipepeo, kwa Mungu namuombea,
Haya njoo kipepeo, njoo tucheze pamoja [10]

(2) Mashairi ya mtindo randuu. Katika kipindi hiki cha nne, kwa mara ya kwanza Mwashinga alianza kuandika mashairi ya Kiswahili kwa mtindo wa Kifaransa ujulikanao kama Rondeau. Kwa Kiswahili bahari hii anaiita bahari ya randuu. Randuu ni shairi lenye beti tatu na mishororo kumi na tano. Lina vina vya kati na vya mwisho. Katika shairi hilo kipande cha kwanza cha mshororo wa kwanza (yaani ukwapi) kinatumika kama mshororo wa mwisho katika ubeti wa pili na wa tatu kama inavyoonekana katika shairi hili hapa chini:

 JIJI LINALOPENDEZA         

Jiji linalopendeza, Mungu katuandalia,
Ni zuri lakushangaza, mwangaza umetulia,
    Mwokozi mwenye uweza, ndiye aliyelijenga,
    Umilele waangaza, chozi sitolengelenga,
Matamu yake machenza, hilo nimelisikia,

Ninashindwa kueleza, jinsi navyojisikia,
Mungu atupe uweza, faraja kutupatia,
   Nimekwishapeleleza, jiji halina kimbunga,
           Jiji linalopendeza.

Watoto wachezacheza, maisha wafurahia,
Ajali na majeneza, hayo hayataingia,
    Mungu ameshaeleza, huzuni ataipinga,
    Daima tutapendeza, tutaishi kwenye mwanga,
Tutaimba na kucheza, machozi yatakimbia,
         Jiji linalopendeza.

(3) Mashairi ya bahari ya Ukawafi na Mavue. Katika kipindi hiki cha nne Mwashinga pia alianza kuandika mashairi katika bahari za Ukawafi na Mavue. Ukawafi ni shairi la vipande vitatu (ukwapi, utao, na mwandamo) na mavue ni shairi la vipande vinne (ukwapi, utao, mwandamo, na ukingo) katika kila mshororo. Ndani ya kipindi hiki cha nne, mashairi yake ya ukawafi na mauve yamechapishwa katika vitabu vyake na katika magazeti pia. Ubeti wa nne wa shairi lililoandikwa katika bahari ya Ukawafi liitwalo “Msimu wa Machipuko” unasema:

 Msimu wa machipuko, nje ukiangalia, ni kama vile mkeka,
Popote huku na huko, unaliona zulia, kijani kisichochoka,
Hata bila ya mbeleko, watoto wanatulia, wakaliapo ukoka,
Msimu wa machipuko, wengi waufurahia, wazazi, dada na kaka.[11].

Mfano wa mashairi yake yaliyoandikwa katika bahari ya Mavue ni pamoja na shairi linaloitwa “Hasi Imekuwa Chanya,” lilochapishwa katika gazeti la Sauti Kuu.

 Sauti ya baragumu, katika tufani, upepo wa hari, chini ninakaa,
Niipokeapo simu, sauti moyoni, yatangaza shwari, usoni nang’aa,
Umeiondoa ndimu, mwangu mdomoni, sasa ni tayari, chungwa kulitwaa,
Sauti yako ni tamu, katika tufani, wanipa habari, njema kama taa.[12].


Vitabu vya mashairi ya Kiswahili

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Christopher Mwashinga, Beeches of Golden Sand: Inspirational Poems (Berrien Springs, MI: Marejeo Books, 2009)
  2. Christopher R. Mwashinga, Sauti Toka Ughaibuni (Berrien Springs, MI: Maximum Hope Books, 2014)
  3. Kenya's Sunday Nation of 18 June 1995; 13 August 1995.
  4. Literature Evangelist Magazine published by the General Conference of Seventh-day Adventists, June 1996.
  5. The League of American Poets' Anthology: A Treasury of American Poetry Vol. III, 2007 and Great Poems of the Western World, 2010.
  6. Ona kwa mfano Sauti Kuu Toleo Na. 13 Alhamisi Aprili 16-Jumatano Aprili 22, 2020
  7. https://www.youtube.com/watch?v=Ss7plu-z7J0&t=2070s
  8. https://www.youtube.com/channel/UC-y7pHWONOjy_Qw5o_zr8zw
  9. https://www.youtube.com/watch?v=Ueqo7aNoGJA&t=948s
  10. Christopher Mwashinga, ‘’Mdomo Mmoja, Masikio Mawili: Mashairi ya Watoto’’ (Berrien Springs, MI: Maximum Hope Books, 2019), 17
  11. Njia ya Matumaini (Berrien Springs, MI: Maximum Hope Books, 2021)
  12. Gazetii la Sauti Kuu, Alhamisi, Februari 24-Machi2, 2022