Tumaini Lenye Baraka

Tumaini Lenye Baraka ni diwani ya mshairi na mwandishi wa vitabu Christopher Richard Mwashinga toka nchi ya Tanzania, Afrika Mashariki ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani.

Mwashinga anaandika vitabu kwa lugha ya Kiingereza[1] na Kiswahili[2]. Tumaini Lenye Baraka ndiyo kazi yake kubwa zaidi ya mashairi kwa lugha ya Kiswahili.[3] Ameandika vitabu vitatu vya mashairi ya Kiswahili na vinne vya mashairi ya Kiingereza.[4]

Umaarufu wa Ushairi wa Christopher Richard Mwashinga unazidi kuongezeka na mashairi yake kupendwa duniani, hasa nchini Marekani[5] na katika nchi za Afrika Mashariki. [6]

Historia fupi ya Tumaini Lenye Baraka

hariri

Mashairi yaliyomo katika diwani hiyo yaliandikwa na Christopher Mwashinga kwa kipindi cha zaidi ya miaka thelathini.

Shairi la awali zaidi lililomo katika diwani hii lilitungwa siku ya Ijumaa, Desemba 27, 1985 huko Mpodoni, Siha Magharibi katika Wilaya ya Hai, mkoa wa Kilimanjaro. Shairi hilo liitwalo "Tunapomaliza Mwaka", linatokea kama shairi namba 133 katika Diwani hiyo.

Shairi namba 136 liitwalo "Nisipokuwa Kazini" ndilo shairi la mwisho kutungwa linalopatikana katika diwani hii. Shairi hili lilitungwa katika Chuo Kikuu cha Andrews, Michigan, Marekani Januari 6, 2017.

Mashairi yote 163 yanayopatikana katika diwani hii, yalitungwa katika nchi tofautitofauti duniani ikiwa ni pamoja na: Tanzania, Uingereza, Ujerumani, Israeli, Uturuki, Ugiriki, Marekani na Misri.

Toleo la kwanza la diwani hii, lijulikanalo kama toleo la Marekani (American edition), lilichapiswha nchini Marekani mara mbili na Maximum Hope Books mwezi Machi na Aprili 2017. Toleo la pili, lijulikanalo kama toleo la kimataifa (World edition), lilichapishwa na kampuni ya Maximum Hope Books, nchini China mwezi Juni mwaka 2017. [7]

Mchango katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili

hariri

Mwandishi wa diwani hiyo anaonesha jinsi lugha ya Kiswahili inavyokua kwa haraka katika Afrika na ulimwenguni kote kwa ujumla. Kukua kwa ushairi wa Kiswahili, ambao anauita "lafudhi ya asili inayoeleweka zaidi na moyo wa kila mtu anayeishi katika jamii inayohusika,"[8] ni dalili nzuri ya ukuaji wa lugha yetu adhimu. Lakini ukuaji huo lazima ufanyike kwa uwiano mzuri yaani katika nyanja zote - kijamii, kimwili, kiroho na kiakili. Anadai kwamba kuchapishwa kwa Diwani hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kukuza lugha ya Kiswahili duniani. [9]

Tungo zilizomo katika Tumaini Lenye Baraka

hariri

Tungo zilizomo katika diwani hiyo zinazungumzia nyanja kuu nne za mwanadamu - za kijamii, kiakili, kimwili na kiroho.

= Kijamii

hariri

Katika nyanja za kijamii, mtunzi anajadili masuala kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na ndoa, elimu, uonevu, n.k. Kwa upande wa ndoa shairi lijulikanalo kama "Kuvunja Ndoa Msiba" linaionya jamii juu ya madhara yanayotokana na talaka. Beti nne za shairi hilo zitasaidia kuonesha mfano wa aina ya tungo za kijamii:

Kujenga ndoa ni kazi, kupokea na kutoa,
Enzi za utandawazi, ukipewa nawe toa,
Kazana kufanya kazi, jenga, acha kubomoa,
Kuvunja uchumba giza, kuvunja ndoa msiba.

Kufunga ndoa si kazi, kuolewa na kuoa,
Msomi na mjakazi, kazi kudumisha ndoa,
Usifanye ujambazi, mtumbwi kuutoboa,
Kuvunja uchumba giza, kuvunja ndoa msiba.

Ukitoboa jahazi, la mapenzi ya kindoa,
Kwa maneno na mavazi, matendo ya kukomoa,
Maji yenye kiangazi, yataizamisha ndoa,
Kuvunja uchumba giza, kuvunja ndoa msiba.

Hata kama kwa machozi, inusuru yako ndoa,
Usifanye uchokozi, mwenzako kumdonoa,
Ukidhani vipodozi, uchungu vitaondoa,
Kuvunja uchumba giza, kuvunja ndoa msiba.[10]

Uhakiki na uchambuzi

hariri

Diwani ya Tumaini Lenye Baraka imeshapitiwa na wanazuoni kadhaa. Mmoja kati yao ni Pendo Salu Malangwa, ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Lugha na Isimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. [11]

Ushawishi wa Tumaini Lenye Baraka

hariri

Baadhi ya mashairi Christopher Mwashinga yaliyomo katika diwani hii ya Tumaini Lenye Baraka yamekuwa yakichapishwa kila juma nchini Tanzania katika gazeti la Sauti Kuu linalotoka kila Alhamisi. [12]. Mengine yamekuwa yakisomwa au kughanwa katika mikutano mbalimbli ya kijamii na kidini katika nchi mbalimbali duniani. Kwa mfano shairi lake maarufu lijulikanalo kama "Njozi Haiwezi Kufa" liliwasilishwa katika Kongamano la Kimataifa la Vijana Afrika (Pan African Youth Congress) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Baraton, nchini Kenya, Desemba 2019 [13]. Vilevile mashairi yake yamekuwa yakitumika katika mikutano mingine nchini Tanzania [14]. Miaka ya karibuni, vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini Tanzania vimekuwa vikitumia mashairi yake katika vipindi vyao ili kufikisha ujumbe wa matumaini kwa watazamaji na wasikilizaji wao. Kwa mfano kituo kikubwa cha televisheni cha Hope Channel Tanzania katika kipindi chao cha Mbiu ya Kusini na Morning Star Radio kinachorushwa kila siku ya Jumapili [15].

Tanbihi

hariri
  1. Christopher Mwashinga, Beeches of Golden Sand: Inspirational Poems (Berrien Springs, MI: Marejeo Books, 2009)
  2. Christopher R. Mwashinga, Sauti Toka Ughaibuni (Berrien Springs, MI: Maximum Hope Books, 2014)
  3. Vitabu vyake vingine vya mashairi ni pamoja na Kilele cha Tumaini (2016) na Sauti Toka Ughaibuni (2014)
  4. Maximum Hope Newsletter, Volume 1 Number 1 Winter, 2015, p. 16.
  5. The League of American Poets' Anthology: A Treasury of American Poetry Vol. III, published in 2007
  6. A. Lavender Great Poems of the Western World, 2010.
  7. Journal of Adventist Mission Studies Vol. 13, No. 1,pp.23-32 (Spring 2017
  8. Tumaini Lenye Baraka, uk. 13-14.
  9. Tumaini Lenye Baraka, uk. 21
  10. Tumaini Lenye Baraka, shairi namba 121 uk. 230-231
  11. Katika dibaji ya diwani hii, Malangwa aliandika: "Diwani ya Tumaini Lenye Baraka ni kitabu cha aina yake katika ushairi wa Kiswahili, na pengine pia katika vitabu vya mafundisho ya dini tulivyozoea kuviona, ukiachilia mbali Nyimbo za Kikristo. Imezoeleka sana kuona vitabu vya mafundisho ya dini vikiwa vimeandikwa kinathari. Diwani hii imekuja na mtindo mpya wa kuielezea imani ya Kikristo katika vionjo na mguso wa kishairi, na tena ushairi wa kimapokeo unaozingatia kanuni na taratibu zote za uandishi wa mashairi. Mtu wa kwanza kabisa kuthubutu kuandika mafundisho ya Kibiblia (Vitabu vya Injili na Matendo ya Mitume) katika mtindo wa ushairi kwa lugha ya Kiswahili alikuwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mkabala huu umekuwa wa kipekee sana na haujazoeleka katika maandiko ya dini, na kimsingi unasaidia sana kuwafikia watu wengi ambao hawajapata nafasi ya kusoma Biblia. Mashairi ya Diwani hii yamewasilishwa kwa namna tofauti tofauti na hivyo kuzidi kumfanya msomaji aendelee kufurahia ujumi na umbuji wa kisanaa. Kwa mfano, katika Diwani hii kuna mashairi yaliyoandikwa kwa mtindo wa utenzi na mengine yameandikwa kwa mtindo wa masimulizi. Aidha, katika Diwani hii kuna mashairi ambayo ni Tathilitha (yenye mistari 3), Tarbia (mistari minne) na Takhmisa (mistari 5). Karibu mashairi yote yana mkarara au kibwagizo, yaani mstari mmoja unaojirudia rudia na machache sana yametumia kimalizio kwenye beti zake. Mtindo na ubunifu uliotumika vimefanya Diwani hii ivutie sana kusoma. Mwandishi wa Diwani hii ameonesha namna dini na mafundisho yake inavyosaidia katika suala zima la ujenzi wa jamii. Kwa maneno mengine, mwandishi ameonesha uhusiano mkubwa uliopo baina ya mafundisho ya kidini na maendeleo ya jamii. Kwa mfano, Mwandishi ametoa mausia mbalimbali kuhusu ndoa, kuishi kwa malengo au kuweka malengo katika maisha, umuhimu wa kutunza na kutumia wakati vizuri (muda ni mali), upendo kwa wazazi na ndugu wengine, umuhimu wa elimu, kuwajali wengine, kuridhika na ulivyonavyo na anawatia moyo wanajamii wasiogope uzee, kwamba uzee ni hekima na suala muhimu tu ni kutumia ujana vizuri. Maudhui mengine ya kijamii ambayo Mwandishi amejishughulisha nayo katika Diwani hii ya Tumaini lenye baraka ni maonyo kuhusu ubaya wa chuki, kuwa makini katika kuchagua marafiki, ameonya wenye madaraka juu ya unyanyasaji wa wanyonge, kutenda haki na kumheshimu Mungu wa mbinguni. Aidha, falsafa ya Mwandishi, Christopher Mwashinga, kuhusu suala zima la muda imejipambanua kwa uwazi sana. Mwandishi anasisitiza kwamba muda ni mali na kwamba wanadamu wanapaswa kuishi kwa malengo; na waweke malengo makubwa makubwa, hata kwenye maombi wasiombe mambo madogo madogo, waombe makubwa. Mwandishi pia amekuja na mtazamo mpya kuhusu sikukuu za mwanadamu; siku ya kutoka tumboni mwa mama, siku ya kuzaliwa upya (kubatizwa) na siku ya kutambua kwa nini upo duniani. Hizi ni siku ambazo mwanadamu hapaswi kuzisahau. Katika Diwani hii, Mwandishi Mchungaji Christopher Mwashinga, ametumia muda mwingi sana kuibua na kufundisha masuala mbalimbali ya kidini, na hasa dini ya Kikristo. Diwani hii inamtambulisha Yesu Kristo kwa namna ya pekee sana na kwa namna anavyoelezwa katika Maandiko Matakatifu, Biblia. Anamweleza Yesu kama Tumaini la Vizazi vyote, Yesu ndiye Neema, Nuru ya Ulimwengu, Tumaini lenye Baraka, Mkombozi wa Dunia, Mwokozi, Rafiki anayetupenda na tunayempenda, Yeye ni Ufufuo, Kuhani Mkuu, Jaji, na kadhalika. Amesisitiza na kutoa wito mara kadhaa watu wamwamini Yesu, ndiye suluhisho la mambo yote. Ameeleza na kusisitiza kwamba Biblia ni Mfalme wa vitabu vyote duniani kwani kinafunua kila kitu kuhusu maisha haya na yajayo. Amesisitiza kwamba Mungu ndiye asili ya vitu vyote. Ametoa wito kwa Wakristo wote pamoja na wachungaji au wahubiri kuishi sawa sawa na injili inavyofundisha na siyo kuwa watu wa maneno tu. Kitabu hiki kinafaa kusomwa na watu wote. Kulingana na lugha rahisi na ya wazi iliyotumika, kitabu hiki kinafaa kusomwa na mzungumzaji yeyote wa lugha ya Kiswahili. Pili, Diwani hii inafaa kusomwa na wanafunzi wa lugha na fasihi ya Kiswahili katika ngazi ya sekondari na vyuo, kwani imesukwa kwa namna ambayo imesheheni ujumi na umbuji wa kisanaa unaoibua masuala muhimu kisanaa na hivyo, inafaa kufanyiwa uchambuzi kama kazi nyingine za kifasihi. Mwandishi amejitahidi sana kuzingatia kanuni na taratibu za ushairi, ikiwamo umakini katika kuwianisha vina na mizani, matumizi ya lugha ya kisanaa—tamathali za semi, methali, nahau, na kadhalika. Aidha, Diwani hii inaweza kughanwa katika mikutano ya Kikristo na ikawaelimisha waumini kuhusu masuala mbalimbali ya kiroho. Ama kwa hakika ukibahatika kusoma Diwani hii mpaka mwisho, hutabaki kama ulivyo." Pendo Salu Malangwa ‘Dibaji’ “Tumaini Lenye Baraka: Diwani ya Christopher Mwashinga” Berrien Springs, MI: Maximum Hope Books, 2017) uk. i-iii
  12. Ona kwa mfano Sauti Kuu Toleo Na. 13 Alhamisi Aprili 16-Jumatano Aprili 22, 2020
  13. https://www.youtube.com/watch?v=Ss7plu-z7J0&t=2070s
  14. https://www.youtube.com/channel/UC-y7pHWONOjy_Qw5o_zr8zw
  15. https://www.youtube.com/watch?v=Ueqo7aNoGJA&t=948s