Utawala wa Kijiji - Tanzania
Utawala wa Kijiji ni miongoni mwa tawala katika serikali za mitaa za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni utawala wa chini kabisa kimuundo ukitanguliwa na utawala wa Kitongoji.
Kuwa utawala wa chini haimaanishi kuwa na umuhimu mdogo; isipokuwa ni kupitia utawala huu ndiko ambako mambo mengi yanayoamuliwa au kupangwa na tawala za juu kama serikali, hutekelezwa.
Utawala wa kijiji huelekeza wananchi katika kutumia madaraka yao ya kidemokrasia kuamua juu ya mambo yanayowahusu kama wanakijiji moja kwa moja bila kupitia mlolongo au urasimu mrefu.
Mambo yanayohusiana na tawala za serikali za mitaa yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Utangulizi
haririKila mwananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana wajibu wa kupinga na kukataa kila aina ya uovu katika jamii vikiwemo rushwa, uonevu, wizi, ubadhirifu wa mali za umma na ya watu binafsi.
Pia ana jukumu la kudai na kupigania haki zake na za wananchi wengine, kutoa malalamiko na kuuliza maswali juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea kijijini au kwenye mtaa kupitia vyombo mbalimbali vya kijamii na kiserikali.
Wananchi wanashiriki katika serikali za mitaa kupitia vikao au mikutano mbalimbali ambapo hujadili na kutoa mapendekezo yao kuhusu mipango na matatizo yanayowakabili kwa namna moja au nyingine ili kuweza kupatiwa ufumbuzi na kurahisisha uboreshaji wa huduma za kijamii katika maeneo yao wanamoishi.
Mkutano Mkuu wa Kijiji
haririMuundo wa Mkutano Mkuu wa Kijiji
haririHiki ni chombo kikuu kabisa cha utawala wa kijiji. Kijiji kipo kwa mujibu wa sheria. Wajumbe wa mkutano wa kijijii ni wanakijiji wote waliofikia umri usiopungua miaka 18. Hakuna akidi maalum, kila kijiji hujiwekea akidi yake; inayofaa ni kati ya 20% hadi 33%. Kwa kawaida mkutano hukutana kila baada ya miezi mitatu, kikao cha dharura kinaweza kuitishwa kukiwa na haja na kufanya hivyo, hata hivyo sheria haisemi nani anaita kikao cha dharura. Taarifa ya kuitisha Mkutano Mkuu wa kijiji/mtaa hutolewa kwa siku saba.
Kila baada ya miaka mitano kinakuwa na Mkutano Mkuu Maalum wa uchaguzi wa Mwenyekiti na wajumbe wa halmshauri ya Kijiji. Mkazi wa kijiji anayegombea nafasi ya uongozi kwenye halmashauri ya kijiji au uenyekiti wa kijiji lazima awe na umri usiopungua miaka 21. Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu ni Mwenyekiti wa kijiji akisaidiwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO). Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) hupanga ratiba za vikao, kuandaa na kuitisha vikao vya Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Madaraka na Majukumu ya Mkutano Mkuu wa Kijiji
hariri- Kusimamia na kuwajibisha watendaji.
- Kuweka taratibu za namna ya kuitisha vikao vya dharura.
- Kupitia Mkutano Mkuu Maalum wa uchaguzi kuwachagua Mwenyekiti wa kijiji na wajumbe wa halmashauri ya Kijiji.
- Kujaza nafasi za viongozi wa halmashauri ya Kijiji zilizo wazi.
- Kujadili na kupokea au kukataa taarifa za utekelezaji wa shughuli za kijiji kutoka halmashauri ya kijiji.
- Kupokea, kujadili na kupitisha au kukataa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za kijiji.
- Kupokea, kujadili na kupitisha au kukataa mapendekezo ya kodi, ushuru na vyanzo vingine vya mapato ya kijiji.
- Kupokea na kujadili taarifa ya makusanyo ya fedha za kodi, ushuru na mapato mengine ya kijiji.
- Kupokea, kujadili na kufanyia maamuzi mapendekezo ya serikali ya kijiji ya kutunga sheria ndogondogo.
- Kupokeam kujadili na kuyafanyia maamuzi masuala kuhusu ugawaji wa ardhi na matumizi ya rasilimali zingine za kijiji.
- Kuhoji, kudadisi, kukosoa, kukubali au kukataa taarifa na mapendekezo ya serikali ya kijiji.
- Kuondoa madaraka serikali ya kijiji au mjumbe yeyote kabla ya muda wao.
- Kupitisha azimio la kukaripia rasmi mjumbe yoyote wa halmashauri au halmashauri kwa ujumla kwa utendaji mbovu.
Halmashauri ya Kijiji
haririMuundo wa Halmashauri ya Kijiji
haririHalmashauri ya kijiji ni chombo kikuu cha utendaji katika utawala wa kijiji. Hukutana mara moja kila mwezi, mikutano ya dharura inaweza kuitishwa. Akidi (qorum) ya vikao vya halmshauri ya kijiji ni nusu ya wajumbe wote wa halmashauri ya kijiji. Wakati Mkutano Mkuu ni kama Bunge, halmshauri ya kijiji ni kama serikali. Huchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Uchaguzi wa halmashauri wa kijiji husimamiwa na Mkurugenzi wa halmshauri ya Wilaya. Mkazi wa kijiji mwenye umri usiopungua miaka 21 ana sifa za kuchaguliwa kwenye halmshauri ya kijiji. Wajumbe wa halmashauri ya kijiji wanatakiwa wasizidi 25 na wasiopungua 15. Mkutano Mkuu kwa kushirikiana na Msimamizi wa uchaguzi idadi ya wajumbe wanayotaka kutokana na mazingira yao kutegemea na wingi wa wakazi na ukubwa wa eneo lao (idadi ya vitongoji).
Wajumbe wa halmashauri ya kijiji ni Mwenyekiti wa kijiji, wenyeviti wa vitongoji, wanawake ambao watakuwa theluthi moja ya wajumbe wote na wajumbe wengine. Mwenyekiti wa kijiji ni mwenyekiti wa halmshauri ya kijiji na mwenyekiti wa Mkutano Mkuu. Wenyeviti wa vitongoji huchaguliwa na wakazi wa vitongoji huingia kwenye halmashauri ya kijiji kwa mujibu wa nyadhifa zao.
Mamlaka na Majukumu ya Halmashauri ya Kijiji
hariri- Kutafakari maamuzi, mapendekezo na maazimio ya mkutano Mkuu wa kijiji na kubuni mbinu na njia za kutekeleza.
- Wajumbe wa halmshauri wenyewe wakiwa hawaridhiki kabisa na utendaji wa Mwenyekiti wa kijiji wana haki ya kumwondoa kwa kura theluthi mbili ya wajumbe wote na kuitisha Mkutano Mkuu wa kijiji ili kuchagua mwenyekiti mwingine.
- Kupokea taarifa za mikutano ya vitongoji na kamati zake kufanyia kazi na kupeleka Mkutano Mkuu wa kijiji.
- Kupokea, kutafakari na kufanyia kazi maagizo na mapendekezo kutoka kamati ya maendeleo ya kata (WDC) na halmshari ya wilaya.
- Kubuni na kuendekeza sera na mwelekeo wa kijiji kwa mkutano mkuu wa kijiji.
- Kuandaa na kupendekeza mipango ya maendeleo ya muda mrefu kwa Mkutano Mkuu wa kijiji.
- Kutunga sheria ndogondogo kwa kushauriana na Mkutano Mkuu wa kijiji.
- Kuwaalika wataalamu panapokuwa na haja ya kufanya hivyo ila hawatakuwa na haki ya kupiga kura.
- Kupokea, kutafakari na kupendekeza kwa Mkutano Mkuu wa kijiji maombi ya ugawaji wa ardhi zaidi ya ekari 100 hadi 500 rasilimali zingine kwa maamuzi.
- Kupokea, kutafakari na kuamua ugawaji wa ardhi chini ya ekari 100.
- Kutoa taarifa za utendaji kwa Mkutano Mkuu wa Kijiji.
- Kumiliki mali na kuingia mikataba kwa niaba ya kijiji.
Hitimisho
haririUshiriki wa wananchi ni jambo la msingi sana katika kujiletea maendeleo yao katika vijiji na mitaa. Mahali ambapo wananchi hawashiri wala hawashirikishwi kunakuwa na lawama na mizozo mingi kwa viongozi hasa pale ambapo maamuzi yaliyopitishwa yanawaumiza wananchi. Hapa ndipo wengi huona umuhimu wa kushiriki unapojitokeza zaidi.
Marejeo
hariri- Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI)(2008). Utawala bora kijijini: Ushiriki wa Wananchi katika serikali za Mitaa (Vitongoji, Vijiji na Mitaa)
Viungo vya Nje
hariri- Ofisi ya Waziri Mkuu
- Mamlaka ya Serikali za Mitaa Ilihifadhiwa 20 Juni 2009 kwenye Wayback Machine.