Uumbaji
Uumbaji ni tendo linalosadikika analiweza Mwenyezi Mungu tu kwa sababu ni kusababisha kitu kuwepo kutoka utovu wa vyote.
Hivyo vitu vyote vimeanza kuwepo kwa uwezo wake tu, ingawa kwa kawaida vinatokana na vile vilivyotangulia (k.mf. wazazi).
Kwamba kiumbe kimeweza kikatokana na vingine namna hiyo haifuti ukweli kwamba kimeanza na kinaendelea kuwepo kwa uwezo wa Muumba aliyesababisha viumbe hivyo viwepo na kuzaa au kubadilika.
Kwa msingi huo, si lazima dhana ya mageuko ya spishi ipingane na imani katika uumbaji.
Uumbaji katika Biblia
Uumbaji unasimuliwa katika sura mbili za kwanza za Kitabu cha Mwanzo. Kama vile sehemu mbalimbali za Biblia, kitabu hicho kilitungwa kwa kushona pamoja maandishi tofauti. Ndiyo sababu tunakuta masimulizi mawili juu ya Mungu kuumba ulimwengu na watu.
Simulizi la Kwanza
La kwanza (1:1-2:4a) linamchora Mungu akifanya kazi kama binadamu kwa siku sita halafu kustarehe. Aliumba kila kitu kwa Neno lake (Eb 11:3; ndiye Mwanae pekee: Yoh 1:1-18). Wengine wanaona humo hata kidokezo cha kwanza cha Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, katika upepo uliovuma juu ya wingi wa maji.
Mungu aliona kila alichokiumba ni chema tu, lakini alipoumba mtu katika jinsia mbili akaona ni mwema sana, ni bora kuliko vingine, akamweka kuvitawala kwa niaba yake.
Mwanamume na mwanamke wana hadhi sawa kwa kuwa wote wawili ni sura na mfano wake, si upande wa mwili, bali hasa kwa roho yenye uwezo wa kuelewa na kupenda kwahiari.
Muumba anataka watu washirikiane na kusaidiana, kilele cha uhusiano wowote kati yao ni ndoa inayowafanya kuwa mwili mmoja kama Kristo na Kanisa (Ef 5:31-32).
Simulizi la Pili
Simulizi linalofuata (Mwa 2:2b-25) ni la zamani zaidi, nalo pia lina mafundisho makuu juu ya Mungu na mtu, hasa kwamba huyo ndiye kiumbe bora anayeweza kushirikiana na Mungu, tofauti na vingine.
Hali yake asili ilikuwa ya kupendeza kabisa kwa usafi wa moyo na uhai usio na mwisho, naye alitakiwa akubali kazi za Mungu na kufuata maneno yake, bila ya kujiamulia nini jema, nini baya.
Kumbe, alifanya tofauti akaharibika na kuathiri ulimwengu mzima.