Mwanzo (Biblia)

kitabu cha kwanza cha Bibilia, kilicho na sura 50
(Elekezwa kutoka Kitabu cha Mwanzo)

Kitabu cha Mwanzo (pia: Kitabu cha kwanza cha Musa; kwa Kilatini na Kiingereza Genesis kutoka neno la Kigiriki Γενεσις, "Mwanzo") ni kitabu cha kwanza katika Biblia.

Safari ya Abrahamu kutoka Mesopotamia hadi Kanaani (Mchoro wa József Molnár, 1850).

Kwa asili kimeandikwa kwa Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa בְּרֵאשִׁית, Bereshit, ambalo ni neno lake la kwanza, lenye maana ya “mwanzoni”.

Pia ni kitabu cha kwanza cha Torati (au: Torah, maana yake mwongozo au sheria ya kidini ya Wayahudi), yaani vitabu vitano vya kwanza vya Agano la Kale (kwa Kigiriki Pentateuko). Wengine wanaviita vitabu vitano vya Musa kwa vile wanafikiria kuwa ndiye mwandishi wa vitabu hivyo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Utangulizi

hariri

Jina 'Mwanzo' au 'Asili' linafaa kwa kitabu cha Biblia kinachosimulia habari za asili ya ulimwengu, ya binadamu na ya taifa la Israeli, ambamo zinajitokeza dhambi za watu na njia ya Mungu ya kuwaokoa.

Kitabu cha Mwanzo kina sura hamsini. Katika sura 1 hadi 11, historia ya awali ya binadamu inasimuliwa. Sura 12 hadi 50 inahusu historia ya kale ya Waisraeli. Hasa zinataja hadithi juu ya wazee au mababu wao, kama Abrahamu, Isaka, Yakobo, halafu Yosefu na ndugu zake.

Pentateuko

hariri

Waebrania walitaja Pentateuko kuwa 'sheria' tu (2 Nya 17:9; Neh 8:1-3, 18; Mt 5:17-19; 11:13; 12:5; Lk 24:44). Kiebrania ni lugha ya taifa la Israeli na ndiyo lugha asili ya sehemu kubwa ya Agano la Kale.

Biblia ya Kiebrania iliyotafsiriwa kwanza katika lugha ya Kigiriki au Kiyunani, iliitwa Septuaginta maana yake “sabini” (ndiyo sababu kwa kifupi inaandikwa LXX), kwa vile inafikiriwa kuwa wataalamu sabini walifanya tafsiri hiyo.

Katika tafsiri hiyo, kitabu cha Mwanzo kinaitwa Genesis, maana yake “asili” na vitabu vitano vya kwanza vinaitwa Pentateuko (Kiyunani: penta = tano; teuchos = kitabu), maana yake “Vitabu Vitano”.

Katika mapokeo ya Kiebrania na ya Kikristo ya tangu zamani, Musa alitambuliwa kuwa mwandishi wa Pentateuko (Neh 8:1; 13:1; Dan 9:11; Mk 12:26; Lk 16:29-31; Mdo 15:21).

Pentateuko yenyewe haisemi kwamba Musa alikuwa mwandishi wake, hata hivyo inataja kazi yake ya uandishi. Aliandika sheria ambayo Mungu aliwapa Waisraeli (Kut 24:4; 34:27; [Kum]] 31:9, 24), aliandika historia ya Israeli (Kut 17:14; Hes 33:2) naye alitunga nyimbo na mashairi (Kut 15:1; Kum 1:22,30).

Akiwa kiongozi wa taifa, Musa alijua habari za koo za kale, nyimbo za kale na habari nyingine za mapokeo ya kale zilizokuwa zimetunzwa kwa uangalifu na kukabidhiwa kutoka kizazi hadi kizazi, kwa njia ya maneno au kwa njia ya maandiko (Mwa 5:1; 6:9; 10:1; 11:10,27).

Sawasawa na waandishi wengine, Musa aliweza kutumia habari za asili mbalimbali, hasa pale alipoandika habari za mahali au matukio asiyoweza kuyaona mwenyewe (Mwa 26:33; 35:19-20; 47:26; Hes 21:14).

Zaidi ya hayo alipokea mafunuo mengine kutoka kwa Mungu (mara nyingi alisema na Mungu moja kwa moja; Kut 3:4-6; 33:9-11; Kum 34:10), pia aliandika ripoti yake mwenyewe kuhusu matukio maalumu ya maishani mwake (Kut 17:14; 24:4; Hes 33:2; Kum 31:22-24).

Watu waliochunguza maandiko ya Biblia mara nyingine wamehisi kwamba Pentateuko ilikamilika muda mrefu baada ya Musa. Wamefikiri hivi kwa sababu hamna ulinganifu wa mambo kama vile masimulizi mengine, majina yaliyotumiwa kwa Mungu, matumizi ya maneno na habari za mipango ya dini ya Israeli.

Wengi wamefikiri kulikuwa na maandiko mbalimbali ambayo baadaye yaliunganishwa kuwa kitu kimoja.

Hivyo zamani Musa alidhaniwa kuwa mwandishi wa vitabu hivyo vyote, lakini siku hizi wataalamu wamethibitisha kuwa ndiye asili ya kiini cha sheria za Israeli, lakini vitabu hivyo viliandikwa katika kipindi kirefu hadi mwaka 400 hivi K.K.

Ndiyo sababu katika sheria za vitabu hivyo yanaonekana mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika karne hadi karne, k.mf. kuhusu Pasaka na umoja wa hekalu.

Waliohusika na uandishi ni watu wengi wa Israeli Kaskazini na Kusini. Hasa yameainishwa mapokeo manne tofauti: J (yaliyoandikwa katika karne X K.K. kwa kumuita Mungu YHWH), E (ya karne IX K.K. yanayomuita Elohim), D (yanayotawala Kumbukumbu ya Torati: ni ya karne VII K.K.) na P (yaani ya kikuhani kwa kuwa yanajali sana ibada: ni ya karne VI K.K.). Hayo ya mwisho yalitumika kama fremu ya mapokeo hayo yote ili kuunganisha Torati nzima katika karne V K.K. Hivyo Torati inatunza matukio ya msingi na imani ya taifa la Israeli jinsi ilivyozidi kukomaa baada ya Musa.

Wakati wa majadiliano hayo yote watu wengine wanasahau kwamba, jambo muhimu si jinsi Pentateuko ilivyoandikwa, bali ujumbe wake. Biblia ni kitabu ambacho umoja wake uko wazi, na ujumbe wake ni Neno la Mungu lililo hai (Neh 8:8, 14; 9:3; Yoh 5:39, 46; Mdo 28:23).

Kitabu cha Mwanzo

hariri

Watafsiri wa Septuaginta ndio waliotumia jina la 'Mwanzo' (Genesis) kwa kitabu cha kwanza katika Biblia. Waebrania walikiita kutokana na maneno yake ya kwanza yaani 'Hapo Mwanzo'. Lakini makusudi hasa ya kitabu hiki si mwanzo na asili ya kila kiumbe kadiri ya sayansi, bali ni uhusiano ambao Mungu anautaka na watu wanaoishi katika dunia yake.

Asili ya binadamu

hariri

Adamu alipoumbwa na Mungu alikuwa hana dhambi. Baadaye alianguka katika dhambi, na tangu wakati huo matokeo mabaya yalirithiwa na wanadamu wote. Mwanadamu aliyeasi alistahili na alipokea hukumu ya Mungu, lakini hata hivyo hukumu hiyo siku zote ilichanganywa na neema. Mungu hakuwaangamiza wanadamu, bali alishughulika nao, ili atengeneze njia ya wokovu itakayokuwa wazi kwa watu wote. Mpango wake ulikuwa kumchagua mtu mmoja (Ibrahimu) ambaye kutokana na wazao wake angejenga taifa kubwa la Israeli, na katika taifa hilo angeonyesha mapenzi yake kwa wanadamu, na mwisho amlete Mwokozi wa ulimwengu (Yesu).

Kitabu cha Mwanzo, licha ya kuonyesha jinsi mwanadamu alivyomwasi Mungu na kuanguka katika hukumu yake, pia kinaonyesha jinsi Mungu alivyoanza kutekeleza mpango wake mkubwa wa wokovu kwa wanadamu. Baada ya taarifa ya ahadi za Mungu alizomwahidia Ibrahimu za kumfanya kuwa taifa kubwa na kuwapa watu wa taifa hilo nchi ya urithi katika Kanaani, pia kinaonyesha jinsi ahadi hizo kuhusu taifa na nchi hiyo zilivyoanza kutimizwa.

Mwa 3 inasimulia dhambi iliyo asili ya dhambi zote (Rom 5:12). Kwa njia hiyo tunaambiwa hali yetu mbaya haitokani na Mungu, bali na uasi wetu na wa wazee wetu (Hek 2:23-24). Pia tunafundishwa kukataa toka mwanzo vishawishi vyetu tukiamini maagizo yote ya Mungu yametolewa kwa upendo mkuu. Shetani ndiye aliyeanzisha kishawishi. Eva alipaswa asimsikilize. Kosa lake la kwanza ni kumjibu: hivyo shetani akamdanganya kwamba, eti Mungu ana kijicho, hataki watu walingane naye, ndiyo sababu aliwakataza (Yoh 8:44). Tukianza kuzingatia kishawishi tunakubali shaka juu ya wema wa Mungu kwetu katika kutuelekeza. Kwa namna hiyo walianguka watu wa kwanza waliokuwa watakatifu; kwa urahisi zaidi tutaanguka sisi wenye tabia mbaya kutokana na dhambi hiyo na nyingine nyingi.

Hata baada ya dhambi Mungu anamtafuta mtu kwa upendo, ila huyo kwa aibu anamkimbia, au akijisikia analaumiwa na dhamiri, basi anatafuta visingizio hata kumlaumu Mungu kana kwamba ndiye aliyesababisha. Kwa utakatifu wake Mungu hawezi kuvumilia maovu, na kwa haki yake anataka makosa yalipwe. Ndiyo sababu tunakuta matatizo maishani, kama vile uchungu wa uzazi, kuhusiana kwa mabavu, kupata riziki kwa shida, na hasa kufa: hayo yote ni matokeo ya dhambi. Pamoja na hayo Mungu hapendi mtu yeyote apotee (2Pet 3:9), hivyo toka mwanzo aliahidi kwamba mzawa wa Eva atamponda kichwa shetani. Ndiyo habari njema ya awali kuhusu wokovu ujao.

Watu walivyoishi baada ya dhambi

hariri

Baada ya dhambi ya asili watu walianza kuzaa. Mwa 4:1-16 inatuchorea picha ya Kaini na Abeli kama wazaliwa wa kwanza waliotofautiana kiadili (1Yoh 3:11-12). Toka mwanzo mwovu na mwadilifu waliishi pamoja, wa kwanza akimdhulumu wa pili hata kumuua bila ya kujali udugu. Ikisikitishwa kufikiria mzaliwa wa kwanza kuwa muuaji wa mdogo wake, inafurahisha kwamba wa kwanza kufa alikuwa mwema, kielelezo cha Yesu aliyeuawa bila ya kosa (Eb 12:24).

Toka mwanzo hao walimuabudu Mungu kwa njia ya dini, ibada na sadaka mbalimbali. Hata hivyo Mungu akakubali zile tu zilizotolewa kwa ukarimu (Eb 11:4). Tangu hapo Biblia inatuonyesha jinsi alivyopendelea wadogo kuliko wakubwa.

Kuhusu Kaini tunaonyeshwa ustawi wa dhambi ndani mwake na uongozi wa Mungu aliyemtaka ashinde dhambi bado mlangoni. Hata baada ya dhambi hiyo ambayo ni kubwa kiasi cha kumlilia Mungu alipe kisasi, yeye alizidi kumhifadhi Kaini.

Baadaye (Mwa 4:17-24) kukawa na maendeleo ya aina mbalimbali: ujenzi, ufundi, muziki, lakini hasa dhambi. Picha yake ni Lameki, mtu wa kwanza kuwa na mitara, mkatili kama nini. Ingawa hali ilikuwa ya kukatisha tamaa, kwa baraka ya Mungu watu wakazidi kuzaa na kati ya watoto wao wakapatikana waadilifu kama Henoko aliyestahili kutwaliwa na Mungu. Hata hivyo ongezeko la dhambi likasababisha maisha ya binadamu yafupike (Mwa 6:3) kwa kuwa ni kusogea mbali na Mungu, chemchemi ya uhai.

Mwa 6:5-9:17 inatufundisha kwamba Mungu anachukizwa na dhambi, hivyo anataka kuondoa maovu duniani ili nchi impendeze kama alivyokusudia alipoiumba. Kwa ajili hiyo zamani za Nuhu alileta maji yafunike dunia na kuzamisha waovu. Lakini alisalimisha waadilifu katika safina kubwa ya kutosha, halafu akafunga nao agano thabiti (Eb 11:7). Hasa maji yanayokusudiwa kutakasa dunia yote ni yale ya ubatizo (1Pet 3:17-22), na safina ambayo iokoe watu ni Kanisa, ambalo ni la lazima kwa wokovu kama vile ubatizo unaotuingiza ndani yake.

Uso wa nchi ulipokwishatakaswa na maji njiwa akarukaruka akachuma tawi la mzeituni unaozaa matunda ya kutengenezea mafuta. Njiwa akaonekana tena juu ya maji siku ya ubatizo wa Yesu ambapo alipakwa Roho Mtakatifu na kuyatia maji nguvu ya kutakasa watu (Mk 1:9-11; Tito 3:3-7). Maji na mafuta ndiyo mwanzo mpya kwa binadamu.

Mara alipotoka safinani Nuhu alimtolea Mungu sadaka iliyompendeza hata akaahidi hataangamiza tena binadamu kila anapostahili. Sadaka hiyo ni mfano wa ile ya Yesu msalabani, inayoadhimishwa katika ekaristi, ikituondolea adhabu nyingi na kutuletea huruma ya Mungu, yaani nafasi na neema ya kutubu (Tito 2:11-14). Hatimaye kutakuwa na hukumu (Math 24:37-41).

Mwa 11:1-9 inatufundisha kwamba kiburi na dhambi kwa jumla vinatenganisha watu wasiweze kuelewana wala kuishi pamoja. Kinyume chake katika Agano Jipya tunasikia kwamba siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, aliunganisha tena watu wa makabila mbalimbali katika kutangaza sifa zake (Mdo 2:5-12). Palipo na upendo, tofauti za lugha na utamaduni si shida.

Abrahamu (1900-1800 hivi K.K.)

hariri

Mtu huyo, aliyezaliwa Mesopotamia (Iraq) baada ya watu kubuni uandishi, ndiye mwanzo wa taifa teule la Mungu na baba wa waamini wote. Aliishi kwa kuhamahama pamoja na mifugo yake: akipitia Syria alifikia nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu akashukia Misri kwa muda (Mwa 12). Lakini safari yake muhimu zaidi ni ile ya imani, kwa kuwa Abrahamu aliongozwa na Mungu siku kwa siku, katika mazuri na magumu, akisadiki ahadi zake za ajabu (Eb 11:8-19). Mchungaji huyo alikubali Mungu amchunge maisha yake yote, akamfuata bila ya wasiwasi, akituachia mfano bora wa kumshika mkono Mungu daima bila ya hofu.

Hasa Mungu alimuahidia uzao mkubwa kama nyota za mbinguni, naye akaamini ingawa alikuwa hajapata hata mtoto mmoja: ndiyo imani iliyompendeza sana Mungu (Mwa 15:1-6).

Mwa 18 inamchora kama mtu mkarimu sana kwa wageni, rafiki wa Mungu anayestahili kuambiwa yote, mwenye huruma, busara na unyenyekevu katika sala. Wageni wake watatu ambao ni kama mtu mmoja tu wanadokeza Utatu Mtakatifu. Mungu alimdai Abrahamu asadiki kwamba anaweza yote kama atakavyomdai Bikira Maria (Lk 1:17), naye alidumu kumuomba awahurumie waovu kwa ajili ya waadilifu (Yak 5:16).

Mwa 19 inatuchorea uovu wa watu ambao huko Sodoma ulizidi hata kumdai Mungu alipe kisasi. Lakini kati yao mwadilifu akaokolewa, isipokuwa mke wake akaja kuadhibiwa kwa sababu aliangalia nyuma kinyume cha agizo la Bwana (Lk 17:28-33).

Mwa 21:1-21 inatusimulia jinsi Mungu alivyotimiza ahadi yake kwa kumjalia Sara amzalie Abrahamu mtoto Isaka katika uzee na utasa. Isaka ni mtoto wa imani, si wa mwili, naye ni huru, tofauti na Ishmaeli mtoto wa mtumwa ambaye hastahili kurithi pamoja na mdogo wake. Isaka, baba wa Israeli alipata baraka kuu, naye ni mfano wa watu wa Agano Jipya. Ishmaeli, baba wa Waarabu alibarikiwa pia kwa ajili ya baba yake, naye ni mfano wa Agano la Kale ambapo watu wanategemea mambo ya kimwili (kutahiriwa, kunawa, kubagua vyakula n.k.) na hivyo ni watumwa (Gal 4:21-5:1).

Mwa 22:1-19 inatuletea habari ya kusisimua kuhusu sadaka ambayo Mungu alimdai Abrahamu, yaani kumchinja Isaka. Ni kimoja kati ya vilele vya imani ya binadamu, imani inayoonyeshwa kwa matendo ya utiifu (Yak 2:21-22). Abrahamu hakusita kumrudishia Mungu kile alichopewa, akaondoka alfajiri akasafiri mpaka mahali alipoambiwa (Wayahudi wanaamini mlima huo ndipo walipojenga hekalu la Yerusalemu). Kwa niaba ya waamini wote Abrahamu alikuwa tayari kumchinjia Mungu mwanae pekee ampendaye. Lakini atakayemtoa kweli Mwana pekee ni Mungu Baba (Yoh 3:16). Mwanae ndiye mwanakondoo aliyeuliziwa na Isaka na ambaye Mungu akajipatia juu ya mlima Kalivari alioupanda huku amejitwika sio kuni bali mti wa msalaba. Abrahamu aliamini uwezo wa Mungu juu ya mauti na hasa uaminifu wake kwa ahadi alizompa: kwa hiyo akarudishiwa mwana hai kama mfano wa ufufuko, na katika yeye, yaani katika mzawa wake, watu wote wakabarikiwa. Maisha ya imani yanadai daima sadaka, hasa ya mambo yanayopendwa zaidi (Rom 12:1-2): ndiyo njia ya kujaliwa baraka zinazopita ubinadamu wetu.

Mwa 24 inasimulia kirefu jinsi Abrahamu kabla hajafa alivyomfanyia mpango wa ndoa Isaka kufuatana na mila zao, ila alikataza kabisa asirudi kwao, bali kwa vyovyote abaki katika nchi ile aliyoahidiwa na Mungu. Hivyo imani izidi kuongoza uzao wake kama ilivyomuongoza mwenyewe.

Watoto wa Isaka: Esau na Yakobo

hariri

Kadiri ya Mwa 25:19-34, Rebeka alimzalia Isaka watoto pacha wenye sura na silika tofauti, Esau na Yakobo. Wa kwanza analaumiwa hasa kwa kupuuzia baraka ya Mungu iliyokuwa haki ya kifunguamimba: kwa sahani ya dengu alikubali kukosa neema zile zote alizojitwalia Yakobo kwa imani yake (Eb 12:16-17).

Mwa 27 inasimulia jinsi Yakobo, akifundishwa na mama yake, alivyoweza kubarikiwa na baba. Ingawa uongo wake haukubaliki (Hos 12:3-5), Mungu alithibitisha baraka ya Isaka kadiri ya desturi yake ya kumpendelea mdogo: hivyo Yakobo, aliyekimbia nchi yake ana fimbo tu, alirudi miaka ishirini baadaye ana wake 4, watoto 11 na mifugo wengi ajabu (Mwa 32). Kabla hajaingia nchi yake Mungu alishindana naye usiku kucha akalazimika kumbariki na kumtajia jina jipya, Israeli.

Yosefu na ndugu zake kushukia Misri (1700 hivi K.K.)

hariri

Kama kawaida ya mitara, kulikuwa na upendeleo na wivu. Hasa Yosefu alichukiwa na kaka zake wote, ingawa alikuwa mnyofu hata kuwasimulia ndoto zake za ajabu (Mwa 37:2-11). Kijicho na chuki vilifikia hatua ya kuwafanya watamani kumuua. Walipopata nafasi walifanya njama, ingawa si wote. Mwisho uamuzi ukawa kumuacha hai lakini kumuuza kama mtumwa kwa wafanyabiashara walioelekea Misri (Mwa 37:12-36). Lakini katika maovu ya binadamu Mungu akazidi kushughulikia taifa lake teule. Hivyo Yosefu akawa mfano wa Yesu ambaye alichukiwa bure tu akauawa msalabani kwa wokovu wa wadogo zake wakosefu.

Mwa 39 inaonyesha jinsi Yosefu alivyozidi kumtiii Mungu na kukwepa dhambi. Hivyo baada ya majaribu mbalimbali akatukuzwa kuwa liwali wa Farao kwa nchi yote, hasa kwa usimamizi wa akiba ya chakula (Mwa 41:1-49) kwa ajili ya miaka saba ya njaa aliyotabiri. Kadiri ya mpango wa Mungu njaa hiyo ikawalazimisha kaka zake waje kumuinamia, naye hakulipa kisasi; halafu, kama vile alivyotafsiri ndoto mbalimbali, aliwafafanulia maana ya matukio ya maisha yao katika mpango wa Mungu: kwamba ndiye aliyemtuma Misri kusudi awaokoe (Mwa 45:1-15).

Mwa 46:1-7 inasimulia Yakobo na wazawa wake wote, jumla wanaume 70, walivyohamia Misri. Lakini hawakusahau nchi waliyoahidiwa na Mungu: ndiyo sababu Yakobo na Yosefu walidai waapiwe kuwa watakuja kuzikwa kwao (Mwa 49:29-50:26). Kabla ya kufa Yakobo aliwabariki watoto wake 12 na kwa namna ya pekee Yuda ambaye atatawala moja kwa moja (Mwa 49:8-12).

Muhtasari

hariri
  • 1:1-2:3 Habari za uumbaji
  • 2:4-4:26 Siku za kwanza za mwanadamu
  • 5:1-32 Vizazi vya Adamu mpaka Nuhu
  • 6:1-9:29 Uovu wa mwanadamu na hukumu ya Mungu
  • 10:1-11:26 Vizazi vya Nuhu mpaka Abramu
  • 11:27-15:21 Abramu aingia nchi ya ahadi
  • 16:1-25:18 Abramu na mrithi aliyeahidiwa
  • 25:19-28:9 Isaka akabidhi urithi
  • 28:10-36:43 Yakobo aimarisha familia
  • 37:1-50:26 Kukua kwa ukoo wa Israeli na kuhama kwenda Misri

Marejeo

hariri

Vitabu vya ufafanuzi

hariri
  • Cotter, David W (2003). Genesis. Liturgical Press.
  • McKeown, James (2008). Genesis. Eerdmans.
  • Towner, Wayne Sibley (2001). Genesis. Westminster John Knox Press.
  • Wenham, Gordon (2003). "Genesis". Katika James D. G. Dunn, John William Rogerson (mhr.). Eerdmans Bible Commentary. Eerdmans.

Vingine

hariri
  • Davies, G.I (1998). "Introduction to the Pentateuch". Katika John Barton (mhr.). Oxford Bible Commentary. Oxford University Press.

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.