Zoraki (kwa Kilatini na Kiingereza Phoenix) [1] ni jina la kundinyota la angakaskazi ya dunia yetu.

Nyota za kundinyota Zoraki (Phoenix) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Zoraki (Phoenix)

Mahali pake

Zoraki iko karibu na nyota angavu ya Achernar (tamka a-kher-nar, kwa maana “mwisho wa mto”) katika Nahari (Eridanus) inayoitwa pia "mto wa angani".

Inapakana na makundinyota Tanuri (Fornax) na Najari ( Sculptor) upande wa kaskazini, Kuruki ( Grus), Tukani (Tucana), Nyoka Maji (Hydrus) na Nahari (Eridanus).

Jina

Zoraki ni umbo la jina lililojulikana kwa mabaharia Waswahili tangu karne na walilopokea kutoka kwa Waarabu walioona hapa boti au mashua na kuiita زورق zoraq. Boti hii ya Zoraki ilifuatana na kundinyota kubwa ya Nahari (Eridanus) ambayo ni mto wa angani. Mstari wa pinde kuanzia Ankaa kupitia κ, μ, β, ν hadi γ Phoenicis ilifanya umbo la mashua ya Zoraki.

Jina la kimataifa la Phoenix lilibuniwa na Mholanzi Pieter Dirkszoon Keyser aliyechora nyota za kusini katika safari yake katika Bahari Hindi ya miaka ya 1595-96. Inaonekana ya kwamba hakutambua nyota hizi au hakuwa na habari za kundinyota Zoraki ya Waarabu. Hapo alibuni kundinyota lililokuwa mpya kwake na kuilita kwa jina la ndege Phoenix. Phoenix au Finiksi ni mnyama wa visasili katika mitholojia ya Misri ya Kale na Ugiriki ya Kale anayekufa motoni lakini anatokea tena ama kutoka maiti au majivu yake. Baadaye Wakristo walitumia Finiksi kama mfano wa ufufuo. Wakati wa Keyser kulikuwa na wasiswasi kama ni kiumbe cha kisasili tu au labda ndege wa nchi za mbali aliyepatikana kweli. Hatuna habari zaidi lakini inawezekana ya kwamba Keyser aliamini kwamba ndege huyu alipatikana katika nchi za kusini na hapo alitumia jina lake jinsi alivyochagua pia majina ya wanyama wengine wa kusini kwa kutaja makundinyota mpya aliyobuni.

Leo Zoraki - Phoenix iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa kimataifa wa astronomia [2]. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Phe'.[3]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Ankaa au α Alfa Phoenicis yenye uangavu unaoonekana wa mag 2.37 ikiwa na umbali wa Dunia wa miakanuru 77. Hii ni nyota jitu nyekundu [4] [5]. Ni sehemu ya mfumo pamoja na nyota ya pili ndogo inayoizunguka. Jina la Ankaa ni tahajia ya Kilatini kwa kiarabu عنقاء ankaa ambayo ni tafsiri ya "Phoenix" ya Kigiriki; lakini Waarabu wenyewe kiasili hawakutumia jina hili lilitungwa na wanaastronomia wa Ulaya waliotumia majina mengi ya Kiarabu kwa kutaja nyota.

Nyota angavu ya pili ni β Beta Phoenicis ambayo ni pia nyota maradufu. Zikionekana kwa pamoja pande zake mbili zina mwangaza unaoonekana wa mag 3.31. Zinazungukana katika kipindi cha miaka 168. Umbali haikupimwa vizuri bado, makadirio ni kati ya miakanuru 165 hadi 180.[6].

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Phoenix" katika lugha ya Kilatini ni pia "Phoenicis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Phoenicis, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  4. Ankaa (Alpha Phoenicis), tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
  5. "Alpha Phoenicis". SIMBAD Astronomical Database. Centre de Données astronomiques de Strasbourg. Iliwekwa mnamo 25 Agosti 2012.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. Kaler, Jim. "Beta Phoenicis". Stars. University of Illinois. Iliwekwa mnamo 24 Agosti 2012.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Viungo vya Nje