Tukani (kundinyota)

Tukani (kwa Kilatini na Kiingereza Tucana) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu.

Nyota za kundinyota Tukani (Tucana) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Tukani (Tucana)
"Ndege wa Kusini" kwenye atlasi ya nyota ya Johann Bayer; Tukani iko katikati

Mahali pake

hariri

Tukani iko karibu na ncha ya anga ya kusini. Inapakana na makundinyota Nyoka Maji (Hydrus), Zoraki (Phoenix), Kuruki (Grus), Mhindi (Indus) na Thumni (Octans).

Tukani inapatikana kati ya makundinyota yaliyobuniwa tangu mabaharia Wazungu walipozunguka Dunia yote katika karne ya 16 na kuona mara ya kwanza nyota za kusini. Hazikujutajwa katika vitabu vya Wagiriki wa Kale au vya Waarabu. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na mabaharia Waholanzi Pieter Dirkszoon Keyser na Frederick de Houtman katika safari yao ya kuelekea Indonesia zikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1598 katika atlasi ya nyota ya Petrus Plancius.

Keyser alitumia jina la Kiholanzi "Den Indiaenschen Exster" alipotumia neno la kwake nyumbani kwa kutaja Hondohondo aliyoona katika nchi za Bahari ya Hindi. Ndege hii haikujulikana bado katika Ulaya lakini alifanana na Tukani ya Amerika ya Kusini na hivyo Petrus Plancius alitumia jina hili katika globu yake ya nyota aliyotengeneza baada ya kupokea taarifa ya Keyser na Houtman; jina hili lilisambazwa zaidi na Johannes Bayer katika atlasi ya nyota “Uranometria” likawa jina la kimataifa.

Leo iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2]. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Tuc'.[3]

Nyota angavu zaidi ni α Alfa Tucanae yenye mwangaza unaoonekana wa mag 2.86 ikiwa umbali wa Dunia wa miaka nuru 199[4]

Tanbihi

hariri
  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Tucana" katika lugha ya Kilatini ni "Tucanae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Tucanae, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  4. Alpha Tucanae, tovuti ya Prof. Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

hariri