Nyoka Maji (kundinyota)

Nyoka Maji (kwa Kilatini na Kiingereza Hydrus) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu.

Nyota za kundinyota Nyoka Maji (Hydrus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Nyoka Maji (Hydrus)

Mahali pake

hariri

Nyoka Maji lipo karibu ncha ya anga ya kusini. Inapakana na kundinyota la Meza (Mesa), Nahari (Eridanus), Saa (Horologium), Nyavu (Reticulum), Zoraki (Phoenix), Tukani (Tucana), Thumni (Octans).

Nyoka Maji ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa tangu mabaharia Wazungu walizunguka Dunia yote yaani karne ya 16. Hazikutajwa katika vitabu vya Wagiriki wa Kale au vya Waarabu. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na mabaharia Waholanzi Pieter Dirkszoon Keyser na Frederick de Houtman katika safari yao ya kuelekea Indonesia iliyoonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1598 katika globu ya nyota ya Petrus Plancius na kuingizwa baadaye katika ramani ya nyota ya Johann Bayer iliyokuwa muhimu kwa elimu ya nyota[2].

Keyser alitumia jina la Kiholanzi “Waterslang” (nyoka maji) liliyotajwa baadaye kwa jina la Kigiriki "Hydrus“ ambalo kisarufi ni umbo la kiume la jina Hydra (Shuja), kundinyota kubwa ya nusutufe ya kaskazini.

Leo ipo pia katika orodha ya makundinyota 88 yaliyoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3]. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Hyi'.[4]

Nyota angavu zaidi ni α Beta Hydri yenye uangavu unaoonekana wa mag 2.8 ikiwa na umbali wa Dunia wa miaka nuru 24.3[5]

Wingu Kubwa la Magellan linaingia kwa kiasi kidogo ndani ya Nyoka Maji.

Tanbihi

hariri
  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Hydrus" katika lugha ya Kilatini ni "Hydri" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Hydri, nk.
  2. Johann Bayer’s southern star chart , tovuti "Star Tales" ya Ian Ridpath, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  5. Beta Hydri, tovuti ya Prof. Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

hariri