ʻOumuamua

(Elekezwa kutoka 'Oumuamua)

ʻOumuamua (kitaalamu: 1I/ʻOumuamua, 1I/2017 U1) ni kiolwa cha angani kilichotambuliwa mara ya kwanza katika darubini kwenye Oktoba 2017. Kutokana na tabia za njia yake na kasi kubwa ilionekana asili yake si katika mfumo wa Jua letu. Hii ni mara ya kwanza ya kwamba kiolwa kisichotoka katika mfumo wa Jua letu kilitazamwa kikipita karibu hivi nasi.

Njia ya 1I/ʻOumuamua ikipita mfumo wa Jua
Kutokana na vipimo kuna dalili ya kwamba mwendo wa 'Oumuamua ni takriban jinsi inavyoonyeshwa katika filamu hii
Umbo la 'Oumuamua jinsi gani msanii anavyoliwaza kwa kuzingatia habari za vipimo vyake

Kiolwa cha nje ya Mfumo wa Jua

Kiolwa hiki kilitazamwa na paoneaanga pa Pan-STARRS-Teleskop huko Hawaii tarehe 19 Oktoba 2017 wakati kilikuwa na umbali wa vizio astronomia 0.2 kutoka Dunia.

Kiliingia katika mfumo wa Jua kwa njia isiyolingana na bapa la sayari kwenye mfumo wa jua lakini njia yake ilifika kwa pembe la wima na bapa hili. Pia ilikuwa na kasi kubwa sana, hivyo ilionekana si sehemu ya mfumo wetu maana violwa vingi ndani ya mfumo wa Jua huzunguka kwenye bapa la pamoja tena kwa kasi ya wastani.[1]

Jina

Kilipewa jina la ʻOumuamua linalotoka kwenye lugha ya Kihawaii na kumaanisha "mtangulizi" maana ni mara ya kwanza kitu cha kigeni kutoka nje ya mfumo wa Jua kutazamwa karibu hivyo nasi. Jina kamili la kitaalamu ni 1I/ʻOumuamua. Herufi "l" kabla ya ʻOumuamua inamaanisha ni kiolwa kutoka nje ya mfumo wetu. Namba "1" inasema ni kitu cha kwanza cha aina hii kilichopewa jina. Katika mfumo wa majina ya astronomia unaotawaliwa na "Minor Planet Center" kuna pia 1I, 1I/2017 U1 na 1I/2017 U1 (ʻOumuamua) [2]

Tabia

Vipimo vinaonyesha tofauti kubwa za mwangaza wake na hii inachukuliwa kuwa dalili ya umbo lisilofanana na tufe lakini ni zaidi kama silinda (mcheduara) yaani umbo la sigara. Wavumbuzi wake kwenye darubini ya Hawaii hawana uhakika kamili lakini kuna makadirio mawili kuhusu umbo[3]:

  • kama ni silinda inayozunguka zaidi kwenye mhimili mfupi inaweza kuwa na urefu wa mita 360-800, na kipenyo cha mita 36-80
  • kama inazunguka zaidi kwenye mhimili mrefu itakuwa takriban na urefu wa mita 160-360, unene wa mita 160-180 na upana wa mita 8 - 18

Utafiti wa spektra uliopatikana kwa njia ya darubini ya William Herschel Telescope ulionyesha ya kwamba kiolwa kina rangi nyekundu nyeusi kama violwa kutoka Kanda ya Kuiper.

ʻOumuamua inazunguka haraka kwenye mhimili usio mhimili wake mkuu kwa hiyo inagaagaa, haibingirii.

Chombo cha anga?

Umbo lisilo kawaida lilileta maswali kama labda halina asili ya kawaida bali ni chombo cha angani kutoka ustaarabu wa nje.[4]. Wanaastronomia Shmuel Bialy na Abraham Loeb wa Harvard Smithsonian Center for Astrophysics mjini Cambridge, Marekani waliona uwezekano ni chombo kilichotengenezwa ("possibility that it might be a lightsail of artificial origin.") [5]

Darubini ya redio ya taasisi ya SETI ilifuata ʻOumuamua halafu pia Green Bank Telescope lakini hazikupokea alama zozote zinazodokeza habari zisizo za kiasili.[6]

Asteroidi au nyotamkia?

Kilipotazamwa mara ya kwanza wanaastronomia walihisi, kutokana na umbo la njia yake, ni nyotamkia. Lakini ʻOumuamua ilipokaribia Jua walitegemea kuona "mkia" wake yaani gesi zinazotoka wakati miale ya Jua inayeyusha sehemu ya barafu ambayo ni sehemu kubwa ya nyotamkia. Lakini haikuwa hivyo: watazamaji waliona ni asteroidi yaani gimba la mwamba.[7]

Lakini tathmini endelevu ya data ulisababisha tena watafiti wengine kuiona kama nyotamkia isiyotoa "mkia" wa gesi angavu kwa sababu kiini chake cha barafu kinafunikwa na ganda nene la mata ogania yaani kampaundi za kaboni[8] na ganda hilo linazuia kuyeyuka kwa gesi chini yake.

Marejeo

  1. Croswell, Astronomers race..
  2. JPL: Small Asteroid or Comet ‘Visits’ from Beyond
  3. Meech & alii
  4. Asteroid investigated by Stephen Hawking is ‘ALIEN probe with broken engines’, tovuti la gezeti express.co.uk/ la tarehe Thu, Dec 14, 2017
  5. Could solar radiation pressure explain ‘Oumuamua’s peculiar acceleration?, Authors:B ialy, Shmuel; Loeb, Abraham, Publication: eprint arXiv:1810.11490, Publication Date:10/2018
  6. Observation of interstellar object ‘Oumuamua shows no evidence of artificial signals, tovuti ya Techcrunch ya Dec 14, 2017
  7. Meech & alii: "Our observations reveal the object to be asteroidal, with no hint of cometary activity despite an approach within 0.25 au of the Sun."
  8. Tazama Fitzsimmons & alii

Viungo vya Nje

  • Ken Croswell: Astronomers race to learn from first interstellar asteroid ever seen, Nature News kwenye tovuti ya nature.com ya 31 Okt 2017
  • Alan Fitzsimmons, Colin Snodgrass, Ben Rozitis, Bin Yang, Méabh Hyland, Tom Seccull, Michele T. Bannister, Wesley C. Fraser, Robert Jedicke & Pedro Lacerda: Spectroscopy and thermal modelling of the first interstellar object 1I/2017 U1 ‘Oumuamua, Nature Astronomy kwenye tovuti ya nature.com ya 18 Desemba 2017 online hapa, iliangaliwa Desemba 2017
  • JPL: Small Asteroid or Comet ‘Visits’ from Beyond the Solar System. Tovuti ya jpl.nasa.gov. Jet Propulsion Laboratory California Institute of Technology, 27 Oktoba 2017, online hapa Ilihifadhiwa 18 Novemba 2017 kwenye Wayback Machine.
  • Karen J. Meech, Robert Weryk, Marco Micheli, Jan T. Kleyna, Olivier R. Hainaut, Robert Jedicke, Richard J. Wainscoat, Kenneth C. Chambers, Jacqueline V. Keane, Andreea Petric, Larry Denneau, Eugene Magnier, Travis Berger, Mark E. Huber, Heather Flewelling, Chris Waters, Eva Schunova-Lilly, Serge Chastel: A brief visit from a red and extremely elongated interstellar asteroid. In: Nature. 20. November 2017, online hapa, ilitazamiwa Desemba 2017
  • Pultarova, Teresa: Interstellar Object 'Oumuamua Could Be a Comet in Disguise , tovuti ya space.com ya December 18, 2017 online hapa