Aiskilos

(Elekezwa kutoka Aeschylus)

Aiskilos (kwa Kigiriki: Αἰσχύλος aiskhilos; kwa Kiingereza Aeschylus; 525 KK - 456 KK) alikuwa mshairi na mwandishi wa Ugiriki ya Kale. Alitunga takriban tamthiliya 70-90, na 6 kati ya hizo zimehifadhiwa hadi leo. Aiskilos alikuwa wa kwanza kati ya waandishi watatu wakuu wa tamthiliya za tanzia katika Ugiriki wa Kale. Wengine wawili walikuwa Sophocles na Euripides. [1]

Sanamu ya Aiskilos, enzi za Kiroma

Kati ya tanzia zake ni hasa "Waajemi" na "Orestia" zinazoendelea kuonyeshwa.

Aristoteli alisema kuwa Aeschylus alimwongezea mchezaji wa pili kwenye maigizo yake. Wachezaji wake waliongea kati yao, sio kwa kwaya pekee jinsi ilivyokuwa kawaida kabla yake ambako tamthilia za Kigiriki zilionyeshwa kwa mchezaji mmoja na kwaya tu. Mbinu huu uliongeza mvuto wa tamthilia zake kwa watazamaji.

Familia na ujana

hariri

Aiskilos alizaliwa mnamo mwaka 525 KK katika mji mdogo uitwao Eleusis, ambao upo kilomita 27  kaskazini magharibi mwa Athens . Tarehe hiyo inapatikana kwa kuhesabu nyuma miaka arobaini kutoka kwa ushindi wake wa kwanza kwenye mashindano ya Dionisia. Familia yake ilikuwa tajiri, na baba yake Euphorion alihesabiwa kati ya familia za wakubwa wa Attika. Pausanias aliandika kwamba Aeschylus alifanya kazi katika shamba la mizabibu hadi alipopata ndoto kuwa mungu Dioniso alipomtembelea katika usingizi wake na kumwabia atunge tamthilia. Tanzia yake ya kwanza ilionyeshwa alipokuwa na umri wa miaka 26 tu.

Vita ya Uajemi

hariri

Mnamo 490 KK jeshi la Uajemi (Iran), likiongozwa na Dario, lilitua Ugiriki na kujaribu kuliteka. Aiskilos na kaka yake Sinegeiros walijiunga na jeshi la Athens na kupigana dhidi ya Waajemi kwenye Mapigano ya Marathon . Kakaye Syiegeiros aliuawa vitani. Waathens waliweza kushinda jeshi kubwa zaidi la Uajemi. Ushindi huu ulisherehekewa kote katika miji ya Ugiriki. Mnamo mwaka 480 KK mfalme Xerxes I wa Uajemi alijaribu tena kuvamia Ugiriki. Aiskilos alishiriki kwenye Mapigano ya Salamis akiwa mwanabaharia na baadaye kama jeshi la miguu kwenye Mapigano ya Plataia mnamo 479 KK. Tanzia yake ya kale zaidi iliyohifadhiwa inayoitwa "Waajemi" huonyesha maarifa yake katika vita hiyo. Ilionyeshwa mara ya kwanza mwaka 472 KK katika mashindano ya maigizo ya Dionisia ikashinda.

Maisha ya baadaye

hariri

Aiskilos alisafiri mara mbili hadi kisiwa cha Sisilia mnamo miaka ya 470 KK. Alialikwa na Hieron, mtawala wa Siracusa, jiji kubwa la Kigiriki upande wa mashariki wa kisiwa hicho. Kwenye moja ya safari hizi aliandika Wanawake wa Aetna, kwa heshima ya mji ulioanzishwa na Hieron. Alionyesha pia tena Waajemi

Kuanzia mwaka 473 KK Aiskilos alianza kushinda mashindano ya Dionisia ya kila mwaka, akishinda tuzo ya kwanza karibu kila mashindano. Mnamo 458 KK, alirudi Sisila kwa mara ya mwisho, akitembelea mji wa Gela ambapo alikufa mnamo 456 au 455 KK. Inasemekana aliuawa na kobe aliyeanguka kutoka angani baada ya kudondoshwa na tai . Hadithi hii labda ni hadithi tu. [2]

Kazi ya Aeschylus iliheshimiwa sana na Waathens kiasi kwamba baada ya kifo chake, tanzia zake ndizo pekee zalizoruhusiwa kurejeshwa katika mashindano yajayo. Wanawe Euphorion na Euaion, na mpwa wake Philocles, wote waliandika michezo pia.

 
Picha ya kisasa ya uwanja wa tamthilia wa Dionisos huko Athens, ambapo tanzia nyingi za Aiskilos ilichezwa

Tanbihi

hariri
  1. Schlegel, August Wilhelm von. Lectures on dramatic art and literature. uk. 121.
  2. See (e.g.) Lefkowitz 1981, 67ff. Cf. Sommerstein 2002, 33, who does not tell this story when giving a biographical sketch of the poet.

Marejeo

hariri
  Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Aiskilos kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.