Aristoteli (kwa Kigiriki Αριστοτέλης, Aristotelēs; pia: Aristo; 384 KK - 7 Machi 322 KK) alikuwa mwanafalsafa muhimu wa ustaarabu wa Ugiriki ya Kale.

Aristoteli , nakala ya Kiroma ya kichwa kilichochongwa kiasili na mchongaji Mgiriki Lysippo wakati wa karne ya 4 KK

Pamoja na Plato huhesabiwa kati ya wanafalsafa muhimu zaidi katika utamaduni wa magharibi. Aristoteli alikuwa mwalimu wa Aleksander Mkuu kabla huyu hajawa mfalme.

Alichangia sehemu kubwa sana katika elimu ya sayansi na falsafa. mawazo na ugunduzi wake umewachochea watu na maandishi yake yametafsiriwa na kusomwa na watu wengi sana. [1]

Aristoteli aliandika kuhusu sanaa, nyota, biolojia, maadili, lugha, sheria. Zamani watu wa Ulaya walifuata mafundisho ya Aristoteli. Mwanateolojia mashuhuri wa Roma Thomas Aquinas alitumia sana maandishi ya Aristoteli.

Maisha

hariri

Aristoteli alizaliwa kwenye rasi ya Halkidiki katika Ugiriki ya kaskazini kama mtoto wa mganga wa mfalme Amyntas wa Masedonia.

Alipofikia umri wa miaka 17 au 18 alitumwa kusoma kwenye chuo cha Plato huko Athens alipokaa kwa miaka 20, mwanzoni kama mwanafunzi baadaye kama mwalimu.

Baada ya kifo cha Plato mwaka 347 alisafiri akatembelea mahali mbalimbali kwenye visiwa vya Bahari ya Aegei pamoja na Asia Ndogo. Akakaa kwa mfalme Hermias wa Assos akamwoa binti yake Phytias.

Mnamo 345 Hermias aliuawa na Wajemi na Aristoteli alipokea wito la kuwa mwalimu wa mfalme mteule Aleksander wa Masedonia.

Baada ya Aleksander kuwa mfalme, Aristoteli alirudi Athens 385/334 alipofundisha falsafa yake.

Mnamo 323 baada ya kifo cha Aleksander Mkuu alipaswa kuondoka Athens kwa sababu wapinzani wa Masedonia waliongezeka nguvu akahamia Halki alipoaga dunia mapema.

Maandishi

hariri

Aristoteli alitunga kamusi ya falsafa na kitabu juu ya Pythagoras na kuna sehemu tu ya maandishi yale yaliyohifadhiwa. Lakini mihtasari aliyotumia kwa masomo ilihifadhiwa ikakusanywa na wahariri wa baadaye na kutolewa kama maandishi yake.

Kati yake kuna maandishi juu ya mantiki, fizikia, falaki na metafizikia. Neno "metafizikia" limetokana na Aristoteli kwa sababu dhana zake juu ya chanzo na tabia za vitu zilipangwa baada ya maelezo juu ya "fizikia" (hivyo jina "meta-fizikia").

Mafundisho

hariri

Aristoteli alikusanya elimu ya wakati wake akajaribu kuipanga katika utaratibu.

Mwenyewe alifundishwa na Plato lakini alitofautiana na mwalimu wake katika mafundisho juu ya tabia za vitu vyenyewe. Plato aliona ya kwamba ujuzi wote tunaopata kupitia milango ya fahamu hukosa uhakika, si kamili; ujuzi wa kweli unapatikana kwa njia ya roho inayoweza kuelewa kiini cha kitu, wakati milango ya utambuzi inaona umbo la nje tu. Aristoteli alifikiri tofauti akaona utambuzi kupitia milango yetu ni muhimu zaidi na ujuzi hutegemea utazamaji wa mazingira.

Katika "metafizikia" yake kuna pia dhana juu ya "mwanzilishi" au "mwenye mwendo wa kwanza". Aliona kwamba kila kitu kina mwendo kilichosababishwa na kitu kingine. Hivyo mantiki yake ilidai kuwepo kwa chanzo cha mwendo wote akakiita "mwendeshaji asiyeendeshwa" (kwa Kigiriki proton kinoun akineton) au kwa lugha nyingine "chanzo asilia". Chanzo asili hiki kwake ni roho au dhana yenyewe (kwa Kigiriki nous). Aristoteli aliweza kukiita pia "Mungu".

Kati ya dhana zake za kudumu iko nadharia juu ya michezo tanzia inayotajwa mara nyingi kuhusu maigizo, filamu na hata michezo ya kompyuta ya leo. Kufuatana na Aristoteli mchezo tanzia huamsha maono ya watazamaji kama vile pendo au chuki, hamu au hofu, furaha au huzuni na hasira. Ilhali mtazamaji anaingizwa katika hisi hizi roho yake husafishwa wakati wa kutazama mchezo.

Tanbihi

hariri
  1. Profesa wa historia James MacLachlan aliandika hivi: Ulimwengu wa asili ulitawala fikra za watu wa Ulaya kwa miaka 2000.