Kitabu cha Alfu Lela U Lela au Usiku Elfu na Moja (كتاب ألف ليلة وليلة kwa Kiarabu au هزار و یک شب kwa Kiajemi) ni mkusanyiko wa fasihi katika muundo wa visa kutoka Mashariki ya Kati.

Alfu Lela u Lela kwa maandishi ya Kiarabu

Maandishi na historia yake

Visa hivi vinatokana na kitabu cha zamani cha Kiajemi kiitwacho Hazâr Afsâna (Visa vya Ngano Elfu Moja). Inaaminika kuwa mtu aliyekusanya visa hivi na kutafsiri kwa Kiarabu ni mtambaji hadithi maarufu Abu abd-Allah Muhammed el-Gahshigar katika karne ya 14. Tafsiri ya kwanza ya Kiarabu ya kisasa ilichapwa Cairo, Misri mwaka 1835.

Inasadikika kuwa visa hivi vilianza kukusanywa wakati Baghdad ilipokuwa kitovu cha biashara na siasa Mashariki ya Kati. Wafanyabiashara toka Uajemi (Persia), China, India, Afrika, na Ulaya walikuwa wakitembelea Baghdad kwa ajili ya biashara.

Masimulizi makuu ya Alfu Lela: Mfalme na Shahrazad

Mwanzo wa visa hivi ni kuudhiwa kwa mfalme Shahryar wa "kisiwa kilichoko kati ya India na China," na kitendo cha mke wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa. Shahryar aliamua kumuua mke wake. Kwa kuamini kuwa wanawake wote wako kama mke wake aliyemuua (yaani sio waaminifu) anamwamuru mtumishi wake awe anampatia mke kila usiku. Baada ya kulala na mke wake mpya usiku, kunapokucha anaamuru mke huyo auawe.

Hali hii inaendelea hadi pale binti wa huyo mtumishi wake anapounda mbinu maalum na kuamua kujitolea kuwa mke wa mfalme. Binti huyo jina lake ni Shahrazad (Scheherazade au Shahrastini katika vitabu vya Kiingereza). Kila usiku baada ya ndoa yao, binti huyo anatumia masaa na masaa kumsimulia mfalme visa vitamu na vya kusisimua ambapo utamu wake unakuwa umekolea inapofika alfajiri (ule wakati wa kuuawa kwa mke wa mfalme). Kwa nia ya kujua mwisho wa kisa, mfalme alikuwa akiahirisha mauaji ya Shahrazad. Aliendelea kuahirisha kuuawa kwa mke wake hadi akapata naye watoto watatu! Ulipofika wakati huo aliamini kuwa mke wake huyo ni mwaminifu hivyo akabadili uamuzi wa kuua wake zake.

Mchanganyiko wa hadithi

Visa vyenyewe ni mchanganyiko wa mapenzi, misiba, ucheshi, mashairi, na visa vya dini ya Kiislamu. Visa hivi vinajumuisha pia wanamazingaombwe na majini.Visa maarufu ni pamoja na Taa ya Alladin, Baharia Sindbad, Ali Baba na Wezi Arobaini. Kati ya majina mengi inayotajwa kuna pia majina ya Khalifa Harun ar-Rashid na mshairi Abu Nuwas. Inaaminika kuwa visa vya Alladin na Ali Baba viliingizwa katika mkusanyiko huo karne ya 18 na Antoine Galland ambaye alisikia visa hivyo toka kwa mtambaji hadithi wa Kimaroni tokea nchini Syria.


Viungo vya Nje


Viungo vya Filamu na Luninga