Anzwani
Anzwani[1] (Kikomori: Ndzuani, Ndzuwani au Nzwani[2]) ni moja kati ya visiwa vinne vya funguvisiwa vya Komori. Eneo lake ni 424 km² na jumla kuna wakazi 240,000. Ni jimbo la kujitawala ndani ya jamhuri ya Komori. Mji mkuu unaitwa Mutsamudu.
Anzwani | |||
| |||
Mahali pa Anzwani ndani Komori | |||
Ramani ya Anzwani | |||
Nchi | Komori | ||
---|---|---|---|
Mji mkuu | Mutsamudu |
Historia
haririAsili
haririWakazi asilia walikuwa walowezi kutoka visiwa vya Indonesia ya leo waliofika kwa jahazi katika karne za kale. Mabaki ya makazi ya kale yametambuliwa na wana akiolojia na kukadiriwa kuwa wa karne ya 9.[3]: 6 Baadaye wafanyabiashara Waarabu, Waajemi na Waswahili walifika kwenye Komori na kuingiza visiwa pamoja na Anzwani katika nyavu ya biahara ya Bahari Hindi.[3]: 55
Usultani hadi koloni
haririMnamo mwaka 1500 Usultani wa Anzwani ukaundwa ukaendelea kuwa dola lenye nguvu kwenye Komori.[3]: 44 Mwaka 1816 Sultani Alawi bin Husein aliona hatari ya kushambuliwa na Usultani wa Zanzibar akaomba usaidizi wa Ufaransa. Mwaka 1886 Wafaransa walitangaza Anzwani kuwa eneo lindwa na 1912 wakaitwaa kabisa pamoja na visiwa vyote vya Komori kama sehemu ya koloni yao ya Madagaska.[3]: 101–112
Uhuru na mapigano
haririWakati wa uhuru 1975 Anzwani ikajiunga na jamhuri ya Komori.[3]: 152
Tangu 1997 uhusiano kati ya Anzwani na Komori ulikuwa na mabadaliko mbalimbali kutokana na mipango ya wanasiasa wale. Mwaka 1997 Anzwani pamoja na Mwali ikajitenga na Komori na kutangaza uhuru wake kama Dola la Anzwani (État d’Anjouan) chini ya rais Fundi Abdallah Ibrahim. Kisiwa kiliomba kuunganishwa tena na Ufaransa kama Mayotte lakini serikali ya Ufaransa ilikataa. Mwaka 1999 rais mzee Fundi Abdallah Ibrahim akajiuzulu na serikali iliyomfuata ikapinduliwa mwaka 2001 na kamati ya kijeshi. Chini ya kiongozi wa kijeshi Mohamed Bacar kisiwa kikajiunga tena na Komori iliyokuwa na katiba na muundo mpya kama "Umoja wa Komori" tangu 2002. Anzwani sasa ilikuwa jamhuri au jimbo la kujitawala ndani ya Umoja wa Komori. Bacar alichaguliwa kuwa rais wa Umoja kwa miaka 5 chini ya katiba ya Umoja.[3]: 178–185
Baada ya mwisho wa kipindi chake mwaka 2007 mwenyekiti wa bunge kama rais mtendaji alikuwa na jukumu ya kuandaa uchaguzi lakini wanajeshi walimpindua na kumrudisha Bacar. Bacar aliandaa uchaguzi ulioshatkiwa kuwa bandia akatangaza ushindi wake kwa 90% za kura. Serikali ya umoja haukutambua tokeo hili. Bacar alijibu kwa kutangaza tena uhuru wa Anzwani.[3]: 187
Serikali ya Komori iliomba msaada wa Umoja wa Afrika na tarehe 25 Machi 2008 jeshi la Komori pamoja na kikosi cha Umoja wa Afrika chenye askari kutoka Tanzania, Senegal, Sudan na Libya kikisaidiwa na Ufaransa likavamia kisiwa. Bacar alikimbialia Mayotte akaomba kimbilio; Ufaransa umekataa kumkubali kama mkimbizi wa kisiasa lakini vilevile haikumrudisha Komori kwa hofu anaweza kuuawa. Tarehe 15 Juni 2008 uchaguzi mpya chini ya usimamizi wa serikali ya Komori ulifanywa. Rais mpya wa Anzwani ni muhandisi Moussa Toybou.[3]: 187, 188
Marejeo
hariri- ↑ Mandan, A. C. (1903). Swahili-English Dictionary (PDF). The Clarendon Press. uk. 14.
- ↑ Philip Raworth (2010). "The Autonomous Island of Anjouan (Ndzuwani): Introductory Note" (kwa Kiingereza). Oxford University Press.
- ↑ 3.0 3.1 3.2 3.3 3.4 3.5 3.6 3.7 Walker, Ian (2019). Islands in a Cosmopolitan Sea: A History of the Comoros (kwa Kiingereza). Oxford University Press. ISBN 9780190071301.
Viungo vya Nje
hariri- Anjouan.net (tovuti kwa Kiingereza na Kifaransa)
- Tovuti ya Benki Kuu ya Komori Ilihifadhiwa 29 Aprili 2011 kwenye Wayback Machine.