Nchi lindwa

eneo ambalo linalindwa kidiplomasia au kijeshi na serikali yenye nguvu
(Elekezwa kutoka Eneo lindwa)

Nchi lindwa ni dola au eneo lililokubali kukabidhi sehemu za mamlaka yake mikononi mwa nchi kubwa na yenye nguvu. Sehemu za mamlaka zinazotekelezwa na nchi nyingine mara nyingi ni siasa ya nje au mambo ya usalama na jeshi.

Hali ya nchi lindwa wakati mwingine ilikuwa na tofauti ya jina tu na koloni, lakini mara nyingi ilikuwa na tofauti kadhaa kweli.

Kwa kawaida nchi lindwa ni nchi ndogo au nchi hafifu inayopokea ahadi ya nchi mlinzi ya kuitunza na kuitetea au kusaidia katika shughuli mbalimbali. Uhusiano huu umejulikana katika mawasiliano ya kimataifa tangu karne nyingi. Kimsingi uhusiano wa ulinzi wa aina hiyo umetambuliwa katika haki ya kimataifa.

Aina za nchi lindwa

hariri

Nchi lindwa na koloni

hariri

Zote mbili ni eneo chini ya mamlaka ya nchi ya nje. Tofauti ni kwamba koloni liko kabisa chini ya utawala wa nje. Nchi lindwa iko katika hali yake kwa sababu imekubali kulindwa ama kwa hiari yake au kwa sababu ililazimishwa kukubali. Koloni ni mali ya nchi ya nje, lakini nchi lindwa imetambuliwa kama nchi ya pekee. Kwa kawaida nchi lindwa huratibu siasa yake ya ndani na nchi mlinzi inaangalia mambo yake ya nje.

Mifano ya kinyume ni makoloni ya Ujerumani yaliyochukuliwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na mataifa washindi kama Ufalme wa Maungano (Uingereza) au Ufaransa. Nchi hizo kama Tanganyika ziliendelea kutawaliwa kama makoloni mengine lakini kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa.

Nchi lindwa za hiari kamili

hariri

Kuna mifano kadhaa ambako nchi kubwa imekubali kutunza nchi ndogo.

 • Mfano wake ni Andorra ambayo ni nchi ndogo sana katika bonde la milima ya Pirenei kati ya Hispania na Ufaransa. Inawezekana kusema nchi hii ndogo iko kwa sababu majirani makubwa wamesahau kuimeza nyakati mbalimbali katika historia na kwa jumla hawakupenda kuiachia nchi jirani. Eneo lake ni dogo mno, haliwezi kugawiwa. Tena si hatari kwa majirani. Hivyo majirani wote wakubwa wamepatana kulinda usalama wake.
 • Nchi ya Visiwa vya Cook ilikuwa nchi lindwa chini ya New Zealand na uhusiano huo umebadilika kuwa "ushirikiano wa hiari" ambao hali halisi bado ni aina ya ulinzi isipokuwa Visiwa vya Cook vina haki ya kujiondoa wakati wowote. Visiwa havina jeshi ila polisi tu. Usalama wake umetegemea New Zealand. Kinadharia Visiwa vinaweza kuwasiliana na nchi za nje lakini hali halisi vinaweza kuwa na balozi mbili pekee, moja huko New Zealand na moja kwa Umoja wa Ulaya, halafu idadi ya makonsuli. Kwa jumla kama mawasiliano na nchi za mbali ni ya lazima yanafanyika kupitia balozi za New Zealand.

Nchi lindwa wakati wa ukoloni

hariri

Wakati wa karne ya 19 ilijitokeza aina nyingine ya nchi lindwa. Wakati ule uwezo wa kijeshi na wa kiuchumi wa nchi za Ulaya uliwezesha nchi hizo kulazimisha maeneo mapana ya Asia na hasa Afrika kukubali ubwana wao. Ukoloni ulianza wakati mwingine polepole.

Nchi zenye makoloni kama Uingereza ziliona faida kama zifuatazo kuingia katika uhusiano wa ulinzi badala ya kuunda koloni moja kwa moja:

 • kupata mabandari na vituo vya kijeshi katika nchi fulani bila kugharimia utawala wa nchi yote
 • kuzuia nchi nyingine za Ulaya zisiingie katika eneo lilelile
 • kuhakikisha ya kwamba wafanyabiashara wa nyumbani watakuwa na nafasi bora kuuza bidhaa zao au kununua mazao ya nchi
 • kutumia jeshi la nchi dhidi ya majirani yasiyoshirikiana
 • kuzuia watawala wa nchi lindwa kuanza vita katika sehemu yao, hivyo kupunguza gharama za usimamizi wa eneo kubwa zaidi
 • kuwa na nafasi ya ushirikiano na nchi koloni nyingine kwa sababu nchi lindwa bado ilikuwa nchi ya pekee hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuipa hata nchi nyingine nafasi fulani kiuchumi hali iliyoweza kupungua uchungu kati ya nchi koloni.

Ngazi ya kujitawala au kutawaliwa

hariri

Hali ya nchi hizo ilikuwa na ngazi mbalimbali ya kujitawala au kutawaliwa.

 • Usultani wa Sarawak ulikuwa na mkataba na Uingereza uliosema ya kwamba usultani ulikuwa nchi huru ya pekee na Uingereza haukuwa na haki ya kujiingiza katika shughuli za ndani. Hata mawasiliano ya nje yalikuwa mikononi mwa Sultani. Wawakilishi wa mfalme wa Uingereza walitakiwa kujiandikisha katika ofisi ya sultani. Mtawala wa Sarawak hakuwa huru tena kuiachia nchi nyingine sehemu yoyote ya eneo lake. Vinginevyo alipaswa kushauriana na mwakilishi mkazi wa Uingereza lakini aliendesha siasa yake nchini.
 • Opobo katika Nigeria ilikuwa na mkataba uliokataza kila mawasiliano au mikataba na nchi za nje.
 • Sultani wa Zanzibar alikubaliwa kama mtawala mwanzoni wa ulinzi mnamo mwaka 1890. Mwaka 1896 Uingereza ulingia ndani ya utawala wa Zanzibar kwa njia ya kijeshi ikamfukuza Ali bin Said kama sultani mpya baada ya Khalifah bin Said na kumpandisha Hamad bin Thuwaini kwenye utawala. Tangu 1906 Sultani Ali bin Hamud alipaswa kumpa mwakilishi mkazi Mwingereza nafasi ya Waziri Mkuu wake na uhusiano ulikuwa zaidi wa kikoloni kwa sababu sultani hakuweza tena kufanya azimio lolote bila mwakilishi mkazi Mwingereza kuwepo na kukubali.
 • Usultani wa Witu ulikuwa nchi lindwa ya Ujerumani ikakabidhiwa na Wajerumani mikononi mwa Uingereza mwaka 1890; baadaye ilifanywa kuwa sehemu ya kawaida ya koloni la Kenya bila kujali mikataba ya awali.

Hivyo kuna mifano ambapo hali ya kuwa nchi lindwa ilikuwa kipindi kifupi tu kabla ya kumezwa kabisa na kuwa sehemu ya koloni kamili.

Lakini kuna pia mifano ambapo mapatano ya awali yaliheshimiwa, kwa mfano kwenye Falme za Kiarabu zilizorudishiwa mamlaka yote mnamo mwaka 1970.