Bendera ya Senegal
Bendera ya Senegal ina milia tatu za wima pamoja na nyota ya pembetatu katikati.
Milia ni za rangi nyekundu, njano na kijani kibichi. Nyota ni ya kijani.
Maana ya rangi ni kama zifuatazo:
- Nyekundu hudokeza mapambano ya uhuru, damu iliyomwagika na matumaini ya ujamaa
- Njano ni rangi ya dhahabu na utajiri unaotokana na kazi ya pamoja
- kijani ni rangi ya tumaini na maendeleo, pia hukumbusha dini ya raia wengi ambayo ni Uislamu.
Asili ni bendera ya Shirikisho la Mali ya mwaka 1959. Wakati ule Senegal na Sudan ya Kifaransa zilikuwa pamoja katika Shirikisho hadi mwaka 1960. Bendera ya shirikisho ilikuwa ileile, isipokuwa ilionyesha umbo jeusi la mwanadamu katikati. Senegal iliendelea na bendera lakini umbo la mtu lilibadilishwa kuwa nyota.
Rangi ni zilezile zinazopatikana katika bendera nyingi za kiafrika kutokana na athari ya Ethiopia kama nchi ya Afrika iliyofaulu kujitetea dhidi ya majaribio ya kuitawala kikoloni.