Dikteta (kutoka Lat. dictator yaani mwenye kutoa amri kama imla) ni neno la kumtaja mtawala asiyebanwa na sheria na kutumia nguvu ya dola kuendeleza utawala wake na kutokubali upinzani dhidi yake. Pale ambako mtu au kundi la watu hutawala kwa mbinu huu hali ya kisiasa huitwa udikteta. Mfalme anayeweza kuwa na madaraka yaleyale haitwi dikteta.

Benito Mussolini (kushoto) na Adolf Hitler (kullia) walikuwa madikteta wa Italia na Ujerumani katika karne ya 20.
Idi Amin wa Uganda pamoja na askofu Luwum aliyemwua baadaye

Asili ya cheo hariri

Kiasili "dikteta" ilikuwa cheo cha muda kwa ajili ya afisa wa jamhuri ya Roma ya kale. Kwa kawaida Waroma wa Kale waligawa madaraka makuu kati ya maafisa watendaji wawili walioitwa konsuli.

Lakini katika hali ya hatari kuu kama vita au ghasia kubwa senati ya Roma -yaani bunge- iliweza kuamua kuwa na dikteta kwa muda. Uteuzi wa dikteta ulikuwa mkononi mwa makonsuli au kama konsuli mmoja alikuwa mbali na Roma pia mkononi mwakonsuli aliyekuwepo.

Muda wa ofisi ya dikteta ilikuwa hadi miezi 6 lakini mara nyingi dikteta alirudisha madaraka yake kwa senati mara baada ya kumaliza shughuli kama kushinda vita au kugandamiza ghasia.

Dikteta alikuwa mtendaji mkuu wa serikali na amiri mkuu wa jeshi. Alishika pia madaraka ya kihakimu. Aliweza kuwaondoa maafisa wote wengine madarakani, aliweza kutoa hukumu ya mauti na kuagiza kifo cha mtu yeyote. Baada ya kumaliza kipindi chake hakuweza kuwajibika au kushtakiwa kwa maazimio na matendo yake. Kwa kawaida madiketa wa Roma walishirikiana na senati lakini hawakupaswa kufanya hivyo.

Dikteta wa kisasa hariri

Leo hii "dikteta" si cheo rasmi tena lakini namna ya kumtaja mtawala mkali anayeshika mamlaka yote mkononi mwake na kutawala kwa mabavu. Mara nyingi dikteta hakubali uchaguzi wa kisiasa au anahakikisha uchaguzi si huru. Haheshimu haki za kibinadamu kama zinamsumbua. Anatoa amri kama sheria; kama anaruhusu kuwepo kwa bunge na mawaziri ni sharti wafuate maagizo yake. Hakubali upinzani dhidi yake na matamko ya mawazo yasiyopendezwa naye.

Katika karne ya 20 madikteta mara nyingi walitumia mfumo wa chama kimoja cha kisiasa, usimamizi wa magazeti, redio na televisheni.

Kuna madikteta waliofika madarakani kwa njia ya uchaguzi lakini baadaye waliondoa upinzani na kuzuia uchaguzi huru. Mfano wake alikuwa Adolf Hitler wa Ujerumani; chama chake cha NSDAP kilipata kura nyingi kidogo katika uchaguzi wa Januari 1933 akaanzisha serikali kwa msaada wa chama kidogo akatumia mamlaka yake juu ya polisi kwa kuwakamata wapinzani wengi na kutisha mahakama pamoja na wabunge wa upinzani kwa hiyo alipewa madaraka ya kidikteta na bunge; baada ya kuwa na madaraka haya alipiga vyama vingine marufuku akatawala peke yake.

Kuna madikteta waliofika madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi; mifano yake ni Francisco Franco wa Hispania au Idi Amin wa Uganda. Wote walikuwa maafisa wa jeshi walitumia mamlaka yao juu ya wanajeshi kupindua serikali halali kwa njia ya mabavu na kujifanyia wenyewe watawala. Mara nyingi hao madikteta wa kijeshi huanza kwa vyeo kama mwenyekiti wa kamati ya kijeshi au mwakilishi mkuu wa wanajeshi lakini baada ya muda mfupi hakuna tena anayeweza kuwapinga.

Kuna madikteta wengine wanaopanda ngazi ndani ya udikteta wa kikundi au chama ambako awali kamati ilitawala kwa pamoja. Mfano ni Josef Stalin wa Urusi (Umoja wa Kisovyeti) alikuwa mwanzoni Katibu Mkuu wa chama cha kikomunisti tu na wala mkuu wa dola wala mkuu wa serikali. Alitumia nafasi yake kuondoa kwanza upinzani dhidi yake ndani ya chama na baada ya mabadiliko katika vyeo vya dola pia kuimarisha usimamizi wake wa maazimio wa vyama kuhusu maafisa wa dola. Mwishowe alishtaki wapinzani wake kuwa wasaliti na kushawishi mahakama ya kuwahukumu. Tangu miaka 1935-36 hakuwa tena na mpinzani na matakwa yake yalikuwa kama sheria.

Madikteta kadhaa wa karne ya 20 hariri

Tazama pia hariri