Italia

nchi katika Ulaya Kusini

Jamhuri ya Italia (kwa Kiitalia: Repubblica Italiana) ni nchi ya Ulaya Kusini inayoenea katika sehemu kubwa ya Rasi ya Italia na baadhi ya visiwa vya jirani kwenye Bahari ya Kati.

Repubblica Italiana
Jamhuri ya Italia
Bendera ya Italia Nembo ya Italia
Lugha rasmi Kiitalia; kijimbo pia Kijerumani, Kifaransa, Kiladino, Kislovenia, Kisardinia
Mji Mkuu Roma
Rais Sergio Mattarella
Waziri Mkuu Mario Draghi
Eneo km² 302,072.84
Wakazi 59,236,213 (31-12-2020) (23º duniani)
Wakazi kwa km² 201.7
JPT 31,022 US-$ (2008)
Pesa Euro
Wakati UTC+1
Wimbo wa Taifa Fratelli d'Italia (Ndugu wa Italia)
Sikukuu ya Jamhuri 2 Juni
Sikukuu ya Ukombozi 25 Aprili
Simu ya kimataifa +39
Italia katika Ulaya na katikati ya Bahari ya Kati.
Ramani ya Italia
Italia jinsi inavyoonekana kutoka angani

Eneo lake ni km² 302,072.84 ambalo lina wakazi 59,236,213 (31-12-2020): ni nchi ya 23 duniani kwa wingi wa watu, lakini ya 8 au 9 kwa uchumi. Mtu anayetokea katika nchi hii ya Italia kwa Kiswahili huitwa Mwitalia.

Imepakana na Ufaransa, Uswisi, Austria na Slovenia. Nchi huru mbili ndogo zinazozungukwa na eneo la Italia pande zote ni San Marino na Vatikano.

Makao makuu ni jiji la Roma, lenye umuhimu mkubwa katika historia ya dunia nzima.

Jiografia

Umbo la jamhuri, kama lile la rasi yake, linafanana na mguu linalozungukwa na maji ya Mediteraneo pande tatu.

Milima ya Appennini inaunda uti wa mgongo wake, wakati ile ya Alpi, ambayo ni mirefu zaidi, inaunda kwa kiasi kikubwa mpaka kati ya Italia na nchi nyingine za Ulaya.

Mlima mrefu zaidi, ukiwa na mita 4,810 juu ya usawa wa bahari, unaitwa Monte Bianco (Mlima Mweupe) na uko mpakani kwa Ufaransa.

Visiwa viwili vikubwa vya Sisilia na Sardinia ni sehemu za Italia pamoja na visiwa vingi vidogovidogo, vile vya Pelagie vikiwa upande wa Afrika.

Italia ina volkeno 14, ambazo 4 kati yake ziko hai: ile ndefu zaidi kuliko zote za Ulaya (mita 3,329) inaitwa Etna na iko mashariki mwa Sisilia. Italia inaongoza Ulaya kwa wingi wa matetemeko ya ardhi.

Mto mrefu zaidi unaitwa Po na una urefu wa kilomita 652. Mito mingine mirefu ni Adige, Tevere, Adda, Oglio, Tanaro, Ticino, Arno, Piave, Reno, Sarca-Mincio n.k.

Maziwa makubwa zaidi ni: Garda (km2 367.94), Ziwa Maggiore (212.51, likiingia Uswisi), Ziwa la Como (145.9), Trasimeno (124.29) na Ziwa la Bolsena (113.55).

Kutokana na urefu mkubwa wa Italia toka kaskazini hadi kusini, hali ya hewa ni tofauti sana, kuanzia baridi kali sana hadi joto kali sana.

Mikoa

Bendera Jina Makao makuu Eneo (km2) Wakazi Msongamano wa watu/km² Wilaya Miji Miji mikubwa Hali ya utawala
  Abruzzo L'Aquila 10,763 1,307,919 122 4 305 - Kawaida
  Bonde la Aosta Aosta 3,263 126,933 39 0 74 - Kujitawala
  Puglia Bari 19,358 4,045,949 209 6 258 Bari Kawaida
  Basilicata Potenza 9,995 575,902 58 2 131 - Kawaida
  Calabria Catanzaro 15,081 1,954,403 130 5 409 Reggio Calabria Kawaida
  Campania Napoli 13,590 5,761,155 424 5 551 Napoli Kawaida
Emilia-Romagna Bologna 22,446 4,354,450 194 9 348 Bologna Kawaida
  Friuli-Venezia Giulia Trieste 7,858 1,219,356 155 4 218 Trieste Kujitawala
  Lazio Rome 17,236 5,550,459 322 5 378 Rome Kawaida
  Liguria Genoa 5,422 1,565,349 289 4 235 Genoa Kawaida
  Lombardia Milan 23,861 9,749,593 409 12 1544 Milan Kawaida
  Marche Ancona 9,366 1,541,692 165 5 239 - Kawaida
  Molise Campobasso 4,438 312,394 70 2 136 - Kawaida
  Piemonte Turin 25,402 4,366,251 172 8 1206 Turin Kawaida
  Sardinia Cagliari 24,090 1,637,193 68 8 377 Cagliari Kujitawala
  Sisilia Palermo 25,711 4,994,817 194 9 390 Catania, Messina, Palermo Kujitawala
  Trentino-Alto Adige/Südtirol Trento 13,607 1,036,707 76 2 333 - Kujitawala
  Toscana Firenze 22,994 3,679,027 160 10 287 Firenze Kawaida
  Umbria Perugia 8,456 885,535 105 2 92 - Kawaida
  Veneto Venisi 18,399 4,865,380 264 7 581 Venisi Kawaida

Historia

Makala kuu: Historia ya Italia
Mji wa Venisi, uliojengwa juu ya visiwa 117.

Akiolojia imethibitisha uwepo wa Homo neanderthaliensis miaka 128,000-187,000 hivi iliyopita. Homo sapiens sapiens alifika miaka 40,000 hivi iliyopita.

Kufikia milenia ya 1 KK wakazi wengi walikuwa wa jamii ya Kizungu na kutumia lugha za Kihindi-Kiulaya.

Peninsula ya Italia iliunganishwa mara ya kwanza na Jamhuri ya Roma (509-27 KK), lakini hiyo ilipoenea Ulaya kusini na magharibi, Afrika ya Kaskazini na Asia ya Magharibi ikawa na sura ya kimataifa kama Dola la Roma.

Umoja ulipotea kuanzia uvamizi wa jiji la Roma uliofanywa na Wagermanik (476 BK) na hasa baada ya ufalme wa Karolo Mkuu aliyetawala sehemu ya kaskazini tu.

Juhudi za kuurudisha umoja zilifanywa hasa katika karne ya 19, ambapo Ufalme wa Sardinia uliteka sehemu kubwa ya Italia (hasa miaka 1860, 1866 na 1870) na kubadilika kuwa Ufalme wa Italia wenye makao makuu Roma.

Baada ya vita vikuu vya pili iligeuka Jamhuri yenye katiba inayotia mamlaka kuu mikononi mwa bunge.

Ni kati ya nchi sita zilizoanzisha Umoja wa Ulaya mwaka 1957 ikaendelea kuunga mkono ustawi wake hadi uanzishaji wa pesa ya pamoja (Euro).

Maendeleo

Italia ni kati ya nchi zilizoendelea, ikiwa na nafasi ya nane kwa nguvu ya uchumi duniani, hivyo ni mwanachama wa G7, G8 na G20.

Sanaa na utalii

 
Kuanzia kushoto kwa kufuata mzunguko wa mishale katika saa: Kanisa kuu la Florence, lenye kuba la matofali kubwa kuliko yote duniani;[1][2] Basilika la Mt. Petro, kanisa kubwa kuliko yote duniani, liko Vatikani, nchi inayozungukwa na Italia pande zote;[3] kanisa kuu la Milano, la tano duniani kwa ukubwa;[4] na Basilika la Mt. Marko, Venezia.[5]

Italia ndiyo nchi inayongoza duniani kwa kuwa na mahali pengi (51) pa kimaumbile na pa kihistoria palipoingizwa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia".

Kwa sababu hiyo pia inashika nafasi ya 5 kati ya nchi zote zilizo lengo la utalii.

Watu

Wananchi wana sifa za pekee kati ya Wazungu wote, hata upande wa DNA, kutokana na jiografia na historia ya rasi.

Ni kati ya nchi ambamo watu wanatarajiwa kuishi miaka mingi zaidi, lakini pia ni kati ya nchi ambapo uzazi ni mdogo zaidi: wanaokufa ni wengi kuliko wanaozaliwa.

Kutokana na umati wa Waitalia waliohama nchi hiyo karne za nyuma, sasa zaidi ya watu milioni 60 nje ya Italia wana asili ya nchi hiyo, mbali na raia zaidi ya milioni 4 wanaoishi nje.

Lugha rasmi ni Kiitalia, inayotegemea zaidi lahaja za Italia ya Kati, lakini siku hizi inatumiwa na wananchi walio wengi hata katika mikoa mingine, ambayo kwa jumla ni 20.

Upande wa dini, wengi wao (81.2%) ni Wakristo wa Kanisa Katoliki, wakifuatwa na Waorthodoksi (2.8%, wengi wao wakiwa wahamiaji, hasa kutoka Romania) na Waprotestanti (1.1%, wengi wao wakiwa Wapentekoste). Uhamiaji mwingi wa miaka ya mwisho wa karne ya 20 umeleta pia Uislamu (3.7%) na dini nyingine.

Dini zote zinaachiwa uhuru na, tofauti na nchi nyingi za Ulaya, waumini wake wanajitahidi kiasi kufuata ibada (29% kila wiki).

Watu maarufu

Tazama pia

Tanbihi

  1. The Duomo of Florence | Tripleman. tripleman.com. Jalada kutoka ya awali juu ya 2009-12-06. Iliwekwa mnamo 25 March 2010.
  2. Brunelleschi's Dome. Brunelleschi's Dome.com. Iliwekwa mnamo 25 March 2010.
  3. St. Peter's Basilica (Basilica di San Pietro) in Rome, Italy. reidsitaly.com.
  4. See List of largest church buildings in the world; note that the #3 entry, First Family Church building in Kansas, is now a school education complex.
  5. Basilica di San Marco. Jalada kutoka ya awali juu ya 2015-03-05. Iliwekwa mnamo 2017-01-13.

Marejeo

Viungo vya nje

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Nchi za Umoja wa Ulaya  
Austria | Bulgaria | Eire | Estonia | Hispania | Hungaria | Italia | Kroatia | Kupro | Latvia | Lituanya | Luxemburg | Malta | Polandi | Slovakia | Slovenia | Romania | Ubelgiji | Ucheki | Udeni | Ufaransa | Ufini | Ugiriki | Uholanzi | Ujerumani | Ureno | Uswidi
  Makala hii kuhusu maeneo ya Italia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Italia kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.