Erasto B. Mpemba
Erasto Bartholomeo Mpemba (1944 - 2023) alikuwa mwanasayansi kutoka nchi ya Tanzania aliyegundua tabia ya pekee ya maji inayojulikana leo kwa jina la athari ya Mpemba (kwa Kiingereza Mpemba effect). Jina hili linaeleza tabia ya maji kuganda kwa haraka zaidi yakiwa ya moto kuliko maji ya baridi.
Maisha
Mpemba alizaliwa tarehe 1 Februari 1944 katika kijiji cha Bumbuli, wilaya ya Lushoto mkoani Tanga. Alikua mtoto wa mwisho kwenye familia yenye watoto nane ya Foibe na mchngaji Bathoromeo Mpemba.
Alifunga ndoa na Bi. Naomi Vuhahula mwaka 1986 na alikua na watoto 6.
Elimu
Mpemba alipata elimu ya Msingi katika shule ya Msingi Bumbuli na baadae kuendelea na shule ya kati Lwandai. Baada ya hapo, aliendelea na elimu ya sekondari katika shule ya sekondari Magamba iliyopo mkoani Tanga. Elimu ya kidato cha tano na sita ("A level") alipata shule ya sekondari Mkwawa.
Mwaka 1969, Mpemba alipata stashahada ya elimu ya wanyamapori kutoka chuo cha Mweka kilichopo Kilimanjaro, Tanzania. Baadae mwaka 1977 alipata shahada ya sayansi kutoka chuo kikuu cha Canbera kilichopo nchini Australia. Alijiendeleza kwa mafunzo ya uda mfupi katika nyakati mbalimbali, mwaka 1980 kutoka chuo cha Kivukoni na mwaka 1984 kutoka Michigan, Marekani.
Jinsi alivyogundua athari ya Mpemba
Mnamo mwaka 1963 Mpemba alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu kwenye shule ya sekondari ya Magamba (Tanga)[1]. Vijana walikuwa na kawaida ya kutengeneza aiskrimu yao wenyewe jikoni mwa shule. Kwa kawaida walichemsha maziwa wakakoroga sukari ndani yake, wakaiacha kupoa halafu kuiweka kwenye friza.
Siku moja Mpemba alichelewa kazi hii akaogopa ya kwamba mwanafunzi mwingine angechukua chombo cha mwisho kilichopatikana kwa aiskrimu kwa hiyo alimwaga maziwa ya moto katika chombo kile cha mwisho na kuiweka vile kwenye friza pamoja na chombo cha mwenzake aliyewahi kuchemsha na kupoza maziwa tayari. Alipofungua friji baada ya saa moja na nusu alikuta aiskrimu yake ilikuwa tayari ilhali ile ya mwenzake (aliyeweka maziwa iliyopoa) haikuganda bado ilikuwa katika hali ya ujiuji.
Siku iliyofuata akamwuliza mwalimu wa fizikia kwa nini maziwa ya moto iliganda haraka kuliko ile ya kupoa. Mwalimu akajibu hii haiwezekani lazima alikosa.
Katika likizo zilizofuata Mpemba alikutana na rafiki aliyefanya kazi ya upishi mjini Tanga akitengeneza aiskrimu. Huyu rafiki alimweleza ya kwamba hata yeye na wapishi wengine wa aiskrimu huko Tanga waliweka mchanganyiko wa aiskrimu kwenye friza ilhali ni moto kwa sababu inaganda haraka zaidi. Habari hii ilimkumbusha kuhusa maarifa yake shuleni.
Baada ya kumaliza Kidato cha Nne Mpemba aliendelea kusoma A-level kwenye Mkwawa High School huko Iringa. Hapa alifundishwa kuhusu sheria ya kupoza ya Newton. Akamwuliza tena mwalimu wa fizikia kuhusu siri ya maziwa ya moto kuganda haraka kuliko maziwa ya kupoa. Hata mwalimu huyo alikataa akasema haiwezekani na hii ni "fizikia ya Mpemba si fizikia ya kawaida". Tangu siku hiyo utani wa "fizikia ya Mpemba" uliendelea shuleni.
Mpemba aliamua siku moja kurudia jaribio la kuweka vyombo viwili vya maji ya moto na maji baridi ndani ya friza akaona matokeo ni yaleyale. Siku moja shule ilitembelewa na profesa Denis Osborne wa chuo kikuu cha Dar es Salaam. Mpemba alishika moyo akasimama na kumwuliza Dr Osborne kwa nini maji ya moto yanaganda haraka kuliko maji baridi. Osborne alishtuka kidogo lakini aliona ni muhimu kuwahamasisha wanafunzi, kwa hiyo hakutaka kumkatisha tamaa, hivyo akajibu kwa upole kuwa hajasikia habari kama hii, pia hailingani na fizikia jinsi anavyoijua, lakini labda inaweza kutokana na athari isiyojulikana alimwahidi kurudia jaribio akifika tena Dar es Salaam. Wiki iliyofuata Osborn alifanya jaribio na matokeo yalikuwa yaleyale. [2]
Baadaye, wakati Mpemba aliposoma kwenye Chuo cha utawala wanyama pori huko Moshi alitunga muswada pamoja na Dr Osborne walipoeleza pamoja majaribio yao wakijaribu kutoa maelezo ya athari.[3]
Katika maisha ya baadaye Mpemba alikuwa mtumishi kwenye wizara ya maliasili hadi kustaafu.[4]
Mpemba hakuwa mtu wa kwanza wa kugundua athari hii, lakini alikuwa mtu aliyefaulu kuitambulisha mara ya kwanza katika jamii ya wanasayansi. Anastahili sifa kwa ujasiri wake wa kutetea hoja yake mbele ya walimu na wanafunzi waliomcheka. Vilevile utambuzi wake uliweza kuzaa matunda baada ya kukutana na mwanasayansi Dr Osborne aliyekuwa tayari kusikia hoja ya ajabu na baadaye kumpa sifa mwanafunzi badala ya kutangaza athari kama kazi yake mwenyewe tu.
Kazi
Mpemba alianza kazi kama afisa wa wanyamapori wa mkoa wa Mara mwaka 1969. Mwaka 1970 mpaka 1972 alifanya kazi kama afisa habari wa makao makuu ya wizara na baadae kurudi kua afisa wanyamapori wa mkoa wa Shinyanga kati ya mwaka 1972 na 1974. Pia aliwahi kufanya kazi kama afisa maliasili wa mkoa wa Iringa kati ya mwaka 1981 - 1989. Mpemba alifanya kazi wizara ya maliasili kati ya mwaka 1989 hadi mwaka 2005 akisimamia kitengo cha maendeleo na usimamizi ambapo alistaafu mwaka 2005 kama afisa maliasili mwandamizi.
Marejeo
- ↑ Habari zifuatazo zinarejea taarifa ya Mpemba hapa: Cool? A paper by Erasto Mpemba and Denis Osborne, 1969
- ↑ Monwhea Jeng (Novemba 1998). "Can hot water freeze faster than cold water?". University of California. Iliwekwa mnamo 2010-09-15.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Mpemba, Erasto B.; Osborne, Denis G. (1969). "Cool?". Physics Education. 4. Institute of Physics: 172–175. doi:10.1088/0031-9120/4/3/312. republished as Mpemba, E B; Osborne, D G (1979). "The Mpemba effect" (PDF). Physics Education. 14. Institute of Physics: 410–412. doi:10.1088/0031-9120/14/7/312.
- ↑ "Speaker Erasto B Mpemba in 1963". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-10-26. Iliwekwa mnamo 2016-03-03.