Sukari (kutoka Kar. سكر‎ sukkar, iliyotoka kwenye Sanskrit sharkara) ni dutu tamu inayoungwa katika chakula na vinywaji kwa kusudi la kuzinogesha.

Aina nne za sukari.
Fuwele za sukari jinsi zinavyoonekana kwa hadubini.

Sukari kama chakula hariri

Sukari ya chakula inapatikana kwa umbo la fuwele zenye rangi nyeupe na aina za kahawia mbalimbali kutegemeana na kiwango cha kusafishwa wakati wa kuitengeneza. Sukari inayopatikana madukani imetengenezwa kutokana na miwa au bitiruti ya sukari.

Watu hutia sukari katika vyakula na vinywaji vingi.

Sukari hupokewa haraka na mwili na ni chanzo muhimu cha nishati. Wakati huohuo matumizi ya sukari nyingi huleta hatari ya ugonjwa wa kisukari na ugonjwa huo umeenea duniani tangu kupatikana kwa sukari kwa bei nafuu kutoka viwanda vikubwa. Hatari nyingine, inayotokana na kula sukari nyingi, ni kuoza kwa meno[1].

Kikemia sukari ni aina ya kabohidrati yaani wanga. Tukila vitu vya wanga (kwa mfano ugali, viazi, mkate) mwili wetu huvunja molekyuli za wanga kuwa molekyuli ndogo zaidi za sukari. Hii ni sababu ya sisi kupenda sukari sana kwa sababu sukari ndiyo ile mwili wetu unayotafuta na kula sukari inapunguza kazi ya mwili ya kuvunja kabohidrati kuwa sukari mwilini.

Sukari kikemia hariri

Aina zote za sukari ni sehemu ya dutu zinazoitwa kabohidrati. Wanakemia hujua aina mbalimbali za sukari. Sukari tunayotumia kama chakula huitwa sukrosi na fomula yake ni C12H22O11. Kuna pia sukari ndani ya matunda ambayo ni tofauti kikemia huitwa fruktosi (C6H12O6) inayosababisha utamu wa matunda.

Sukari jinsi inavyopatikana dukani huvunjwa tena mwilini. Kemia hutofautisha sukari aina za monosakaridi na disakaridi. Disakaridi ni molyekuli kubwa zaidi inayounganisha monosakaridi mbili. Monosakaridi ni sukari ya kimsingi inayoingia kwenye damu mara moja kwa mfano fruktosi. Hii ni sababu ya kwamba wanamichezo hula vidonge vya fruktosi au deksitrosi wakihitaji kuongeza nguvu haraka.

Historia hariri

 
Miwa iliyokatwa.

Miwa na asali hariri

Kabla ya kupatikana kwa sukari watu walitumia matunda na hasa asali kwa kutia utamu kwenye vyakula vyao. Miwa ililimwa katika Asia ya Kusini tangu miaka elfu kadhaa na maji matamu ya miwa yalitumiwa mahali pengi.

Sukari fuwele ya Wahindi hariri

Wahindi walikuwa watu wa kwanza wanaojulikana kuwa walifaulu kuondoa fuwele za sukari kwenye maji ya miwa tangu mnamo mwaka 350 KK. Kupatikana kwa sukari ya fuwele kulirahisisha biashara yake kwa sababu sukari katika umbo kavu haiozi na inawezekana kuibeba safarini.

Kutoka Uhindi sukari ilienea. Ilitengenezwa pia katika China na Mashariki ya Kati. Watu wa Mediteranea kama Waroma wa Kale walijua sukari kama dawa ghali sana iliyoigizwa kutoka Uhindi kwa njia ya meli.

Kilimo cha miwa pamoja na kutengenezwa kwa sukari kilizidi kuenea katika ustaarabu wa Uislamu hadi Afrika ya Kaskazini.

Ulaya, sukari na ukoloni hariri

Watu wa Ulaya walipaswa kununua sukari kutoka kwa Waarabu hadi mnamo mwaka 1500 kwa sababu hali ya hewa ya Ulaya hairuhusu kilimo cha miwa. Uenezi wa milki za Ulaya katika nchi tropiki za Amerika ya Kati tangu Kolumbus kufikia Amerika uliwapa nafasi ya kuanzisha kilimo cha miwa. Wahispania walianzisha mashamba ya miwa huko Kuba mwaka 1523, Wareno walifuata Brazil mwaka 1532.

Kwa njia hiyo hamu ya sukari ilikuwa sababu muhimu ya uenezaji wa ukoloni pamoja na biashara ya watumwa.

Hata kama makoloni ya Hispania, Ureno, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa na Denmark yalitengeneza sukari, ilikuwa bado ghali kwa watu wa kawaida katika nchi baridi, hasa zile zisizokuwa na koloni.

 
Bitiruti ya sukari.
 
Shamba la sukari nchini Kuba.

Sukari ya bitiruti hariri

Katika karne ya 18 wanakemia Wajerumani walianza kugundua sukari ndani ya mimea ya nyumbani. Andreas Sigismund Marggraf alitambua sukrosi sawasawa na sukari ya miwa katika mimea mbalimbali ya kienyeji. Mwanafunzi wake Franz Carl Achard aliendelea kufanya majaribio akagundua nafasi kubwa ya bitiruti iliyolimwa kama chakula cha wanyama. Mwaka 1802 aliuza sukari ya kwanza kutoka bitiruti. Kwa kuteua mimea yenye sukari nyingi zaidi alizalisha aina mpya ya bitiruti ya sukari yenye kiwango cha asilimia 16-18 za sukari katika maji yake. Kiwango hicho ni kidogo kulingana na miwa lakini kimetosha kutengeneza sukari kwa wingi.

Kwa njia hiyo nchi za kaskazini zisizokuwa na koloni zilipata chanzo cha sukari kwa bei nafuu. Leo hii takriban 1/4 ya sukari yote duniani hutengenezwa kwa njia ya bitiruti. Kiwango kiliwahi kuwa kikubwa katika miaka ya 1960 lakini kimepungua tena kutokana na mabadiliko ya bei.

Uzalishaji wa sukari duniani hariri

Nchi zilizozalisha sukari nyingi duniani mwaka 2003
 Nafasi  Nchi  Uzalishaji 
(t milioni)
 Nafasi  Nchi  Uzalishaji 
(t milioni)
   1 Brazil    24,8    9 Ujerumani    4,2
   2 Uhindi    22,1    10 Pakistan    4
   3 China    11,1    11 Kuba    3,8
   4 Marekani    8    12 Afrika Kusini    2,6
   5 Uthai    7,3    13 Kolumbia    2,6
   6 Australia    5,4    14 Ufilipino    2,1
   7 Mexiko    4,9    15 Indonesia    2,1
   8 Ufaransa    4,4    16 Poland    2

Aina za sukari hariri

Tanbihi hariri

Viungo vya Nje hariri

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: