Fani (fasihi)
Kwa matumizi tofauti ya neno hili angalia makala fani
Fani ni mbinu anayoitumia mwandishi ili kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia/hadhira.
Vipengele vya fani
Vipengele vya fani ni pamoja na Jina wahusika, mandhari, lugha, muundo na mtindo.
Wahusika
Wahusika; ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa wahusika katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni mwa kitabu.
Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika katika makundi yafuatayo:
- Mhusikamviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
- Mhusikabapa ni mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano; kama ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.
- Mhusikashinda yuko katikikati ya mhusika papa na mviringo. Huongozwa na matendo ya hao wahusika wawili. Hajitokezi na msimamo wake imara.
Mandhari
Mandhari ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza kuwa halisi kama vile baharini, njiani, msituni, kijijini, mijini au ya kufikirika kama vile kuzimu, mbinguni, peponi n.k.
Lugha
Lugha ndio wenzo mkubwa wa msanii katika kazi za fasihi, miongoni mwa vipengele vya lugha ni tamathali za semi pamoja na semi.
Muundo
Muundo ni mpangilio wa visa katika kazi ya fasihi anayotumia mwandishi katika kupangilia kazi yake.mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na mtukio.
Kuna aina mbili za kupangilia matukio kama vile:
- Msago: ni namna ya moja kwa moja ya kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna yalivyotukia. Huu ni muundo wa moja kwa moja.
- Urejeshi: ni usimuliaji wa kurukaruka hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo.
Mtindo
Mtindo ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii mmoja na mwingine. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua msamiati, namna anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi ya kwanza, ya pili au ya tatu). Kwa mfano katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” iliyoandikwa na Mariama Ba ametumia mtindo wa barua ya kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho, hii pia inaonesha mtindo wake wa kipekee.
Tanakali za sauti
Tanakali za Sauti: ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
- Tashbiha: ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano.
- Tashihisi: ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano, "Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi".
- Takriri: ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.
- Ukinzani: ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
- Sitiari: ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, juma ni mwamba.#Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
- Taashira: ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
- Jazanda: ni kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.
- Majazi: ni pale tabia za wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
- Lakabu: ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake.
- Chuku: ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu.
Semi
Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:
- Nahau – ni usemi unaotumia maneno ya kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Nahu huwa na vitenzi.
- Misemo – ni semi fupifupi ambazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.
Tazama pia
Viungo vya nje
- Fani (fasihi) Archived 23 Machi 2016 at the Wayback Machine. katika Shule Direct
Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Fani (fasihi) kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |