Injili Ndugu (zinaitwa pia Injili sinoptiki) ni Injili 3 za kwanza katika Agano Jipya ya Biblia ya Kikristo ambazo ni:

Injili hizo tatu zinafanana katika lugha na yaliyomo zikitofautishwa na Injili ya Yohane inayoonekana kutumia lugha kiasi tofauti na kufuata muundo tofauti katika taarifa yake juu ya Yesu kuliko zile za sinoptiki.

Historia

hariri

Kwa muda wa miaka 30 na zaidi Mitume wa Yesu na Wakristo wa kwanza kwa jumla walitangaza habari za Yesu Kristo hasa kwa midomo, halafu kwa barua na maandishi mengineyo.

Lakini wakati huohuo (miaka ya 50 BK?) baadhi yao walianza kukusanya kwa maandishi ushuhuda wa mitume na wengineo kuhusu mafundisho na maisha ya Yesu, kama vile mifano aliyoitoa, mabishano yake na Mafarisayo, na hasa mateso yake.

Kati yao tunaambiwa Mathayo aliandika kwa Kiaramu, ingawa hatuna hata kipande cha kitabu chake asilia na cha vinginevyo.

Ila Wainjili wetu walivisoma na kuvitumia kwa kutunga vya kwao.

Baada ya Injili zao nne kupatikana, Kanisa likaacha vitabu vya kwanzakwanza hata vikapotea.

Wataalamu wengi wanakubaliana kusema Marko ndiye aliyetangulia kuandika kitabu kamili juu ya maisha na mafundisho ya Yesu kuanzia utume wa Yohane Mbatizaji hadi ufufuko wake.

Ndiye aliyekiita kitabu cha namna hiyo Injili, hata neno hilo, lililokuwa na maana ya ujumbe kuhusu Yesu, likaja kuwa na maana mpya ya kitabu cha habari za Yesu.

Marko aliandika akiwa Roma miaka 65-70 hivi, mara baada ya serikali kuanza kuwatesa Wakristo, na akiwa na nia ya kuwaimarisha katika dhuluma.

Baada ya Marko, watu wawili tena waliandika vitabu kama cha kwake, wakikitegemea kwa kiasi kikubwa na kukipanua kwa habari za utoto wa Yesu, mafundisho mengi zaidi n.k.

Wataalamu wanaona Injili hizo za Mathayo na Luka ziliandikwa kati ya miaka 80 na 90, hata hatujui ipi imetangulia.

Mazingira ni yaleyale ya Mashariki ya Kati, labda Antiokia, ila walengwa ni tofauti.

Injili ya Mathayo iliandikwa kwa ajili ya Wakristo wa Kiyahudi wakati mabishano kati ya Kanisa na Israeli yalipozidi, na ina lengo la kuwaimarisha katika imani yao kuwa Yesu ndiye Masiya, ndiye Musa mpya.

Kumbe Luka ambaye alikuwa Mpagani kwanza aliwaandikia hasa Wakristo wa mataifa akisisitiza upendo wa Yesu kwa wote, na kwa namna ya pekee kwa maskini, wakosefu na wengine waliodharauliwa.

Injili hizo tatu zinaitwa “ndugu” kwa jinsi zinavyofanana katika mpangilio, katika habari na pengine katika maneno yenyewe; kwa Kigiriki zinaitwa “sunoptiki”, yaani zinazotazamika kwa pamoja.

Luka aliiongezea Injili yake kitabu cha pili, yaani Matendo ya Mitume, kama mwendelezo wake, kwa kuwa aliona kazi ya Kristo inakamilishwa na Roho Mtakatifu katika ile ya Kanisa.

  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Injili Ndugu kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.