Roma (pia: Rumi) ndio mji mkuu ("Roma Capitale") wa Jamhuri ya Italia.

Mji wa Roma

Bendera

Nembo
Nchi Italia
Mkoa Lazio
Idadi ya wakazi (2018)
 - 2.860.009
Tovuti: www.comune.roma.it
Vilima saba vya Roma asili na vilima saba vya kandokando yake.

Uko katika makutano ya mito ya Tiber na Aniene karibu na Bahari ya Mediteranea.

Roma una wakazi milioni 2,860,009[1] katika eneo la km² 1,285.

Ndani ya mji wa Roma lipo eneo la mji wa Vatikano ambao ni nchi ya kujitawala chini ya Papa wa Kanisa Katoliki.

Sehemu ya mji imo katika orodha ya urithi wa dunia wa UNESCO.

Eneo la RomaEdit

 
Kiini cha Roma kutoka angani.

Roma uko katikati ya Italia ikiwa mita 20 juu ya UB ndani ya tambarare ya bonde la mto Tiber linalopakana na milima ya Abruzzi, milima ya Sabini na milima ya Albani.

Wilaya za jirani ni Viterbo, Rieti, L'Aquila, Frosinone na Latina.

Mwanzo wa Roma ulikuwa kwenye vilima saba vilivyo katikati ya mji wa leo vinavyoitwa: Palatino, Aventino, Campidoglio, Quirinale, Viminale, Esquilino na Celio.

Hali ya hewaEdit

Hali ya hewa hutawaliwa na bahari iliyo karibu. Wastani wa halijoto kwa mwaka ni sentigredi 15,4. Mvua hunyesha wastani wa mm 758 kwa mwaka.

Miezi yenye joto ni Juni hadi Agosti ikiwa na wastani wa sentigredi 21 hadi 23,8; ni miezi ya mvua kidogo.

Mwezi baridi zaidi ni Januari ikiwa na wastani wa sentigredi 7,9.

HistoriaEdit

Historia ya mji inasemekana imeanza rasmi tarehe 21 Aprili 753 KK, lakini majengo ya kwanza ni ya karne ya 10 KK.

Katika karne za KK ulikuwa mji mkuu wa ufalme wa Roma, halafu wa Jamhuri ya Roma, hatimaye wa Dola la Roma.

Katika miaka 100 KK - 400 BK hivi ulikuwa na wakazi wengi kuliko miji yote duniani.

Uenezi wa Ukristo kuanzia mwaka 30 na hasa ujio wa Mtume Petro na Mtume Paulo waliofia dini yao (64-68) huko viliathiri mji huo moja kwa moja.

Kuanzia karne ya 7 BK ukawa mji mkuu wa Dola la Papa, halafu wa Ufalme wa Italia na sasa wa Jamhuri ya Italia. Huitwa mara nyingi "Mji wa Milele".

WakaziEdit

Roma ilianza kama muungano wa vijiji vidogo vyenye wakazi mia kadhaa.

Katika karne ya 1 BK ilikuwa tayari na wakazi milioni moja.

Tangu kuondoka kwa makao makuu ya Kaisari na kupungua kwa nguvu ya Dola la Roma Magharibi idadi ya wakazi ilipungua hadi kuwa na takriban 100,000 mnamo mwaka 530.

Katika karne zilizofuata Italia pamoja na Ulaya iliona vita na mashambulio ya makabila yasiyostaarabika. Mnamo mwaka 1000 Roma ilikuwa mji mdogo wenye wakazi 20,000 pekee walioishi ndani ya maghofu ya mji mkubwa wa kale.

Tangu kuimarika kwa utawala wa mapapa mji ulianza kukua tena; mnamo mwaka 1900 ukawa na wakazi 400,000. Katika karne ya 20 mji ulipanuka sana hadi kufikia idadi ya wakazi wa zamani hata kuipita. Siku hizi asilimia 7.4 ni wageni.

Orodha inayofuata inaonyesha makadirio hadi 1858, baadaye ni namba za sensa.

Mwaka BK Wakazi
330 1.000.000
410 400.000
530 100.000
650 20.000
1000 20.000
1750 156.000
1800 163.000
1820 139.900
1850 175.000
1853 175.800
1858 182.600
31. 12. 1861 194.500
31. 12. 1871 212.432
Mwaka BK Wakazi
31. 12. 1881 273.952
10. 02. 1901 422.411
10. 06. 1911 518.917
01. 12. 1921 660.235
21. 04. 1931 930.926
21. 04. 1936 1.150.589
4. 11. 1951 1.651.754
15. 10. 1961 2.188.160
24. 10. 1971 2.781.993
25. 10. 1981 2.840.259
20. 10. 1991 2.775.250
21. 10. 2001 2.546.804
31. 12. 2011 2.617.175
Mandhari ya Roma kutoka kuba ya Basilika la Mt. Petro

UchumiEdit

Roma ndiyo kitovu kimojawapo cha sekta ya viwanda na sekta ya huduma ya Italia. Utalii ni pia muhimu sana kiuchumi, kutokana na watalii 26,100,000 wanaoutembelea kila mwaka: 6.5% za Jumla ya Pato la Taifa zinapatikana ndani ya Roma ambazo ni kushinda miji mingine yote ya Italia.

Roma ina makao makuu ya F.A.O. (Food and Agriculture Organisation - Shirika la Chakula na Kilimo) ya Umoja wa Mataifa pamoja na ofisi zote za serikali ya Italia.

TanbihiEdit

  1. "I numeri di Roma Capitale" (PDF). Comune di Roma. 31 December 2018. Archived (PDF) from the original on 4 May 2020. Retrieved 4 May 2020.

Viungo vya njeEdit

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu maeneo ya Italia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Roma kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.