Kiyama ni neno linalotokana na Kiarabu يوم القيامة, Yawm al-Qiyāma yaani "Siku ya ufufuko" ambayo inaitwa pia يوم الدين , Yawm al-Dīn, yaani "Siku ya dini".

"Hukumu ya Mwisho" ilivyochorwa na Michelangelo kwenye ukuta wa Cappella Sistina huko Vatikano.
Mchoro wa Hans Memling kuhusu "Hukumu ya Mwisho" 1467-1471.
Mchoro wa karne ya 17 kutoka Lipie (kwenye Historic Museum in Sanok, Poland).
Mchoro wa ukutani kuhusu "Hukumu ya mwisho" huko Voroneţ Monastery, Romania.
Mchoro wa William Blake Mwono wa Hukumu ya Mwisho (1808)

Kadiri ya imani ya dini mbalimbali, hususan Uyahudi, Ukristo na Uislamu, kutakuwa na siku ambapo Mungu ataleta ufufuko wa wafu wote pamoja na hukumu ya matendo yao.

Katika Ukristo

hariri

Kadiri ya Mtume Paulo, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa, lakini katika hali tofauti: “hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika” (1Kor 15:42). Siku ya ufufuo “ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Lk 21:27). “Saa yaja ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuko wa uzima, na waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yoh 5:28-29). “Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Math 25:46).

Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu kwa kudhihirisha misimamo ya watu wote ambao, kwa kupokea au kukataa upendo wa Mungu moyoni mwao, wametenda mema au la. “Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyopenda, kwamba ni mema au mabaya” (2Kor 5:10). “Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu” (1Kor 4:5). “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake. Na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, ‘Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia… Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi’” (Math 25:31-36,40). “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Math 5:7).

Baada ya hukumu ya mwisho, waadilifu watatukuzwa mwili na roho pamoja na Yesu, na ulimwengu pia utageuzwa. “Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake” (2Pet 3:13). “Na Roho na Bibi arusi wasema, ‘Njoo!’ naye asikiaye na aseme, ‘Njoo!’… Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, ‘Naam, naja upesi’. Amina. Na uje, Bwana Yesu! Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina” (Ufu 22:17,20-21).

Mada hiyo imetumiwa na muziki, uchoraji n.k., hasa Wakristo, kufuatana na Injili (Math 25:31-46).

  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.