Milki ya Gupta
Milki ya Gupta (kwa Kisanskrit: गुप्तसाम्राज्य, gupta sāmrājya) ilikuwa dola la kihistoria nchini Uhindi uliotawala sehemu kubwa ya Bara Hindi kati ya 320 - 550 BK na kutawaliwa na nasaba ya Gupta.
Kipindi cha Gupta kilikuwa kipindi cha amani na maendeleo katika sayansi na sanaa. Wahindi wengi wanakitazama kuwa "enzi ya dhahabu" katika historia yao. Ustaarabu wa Uhindi uliweza kuongeza elimu na wezo wake katika fani nyingi kama vile sayansi, tekinolijia, uhandisi, sanaa, falsafa, hisabati, astronomia na dini zilizoendelea kuwa msingi wa utamaduni wa Kihindi.
Milki hii kubwa iliporomoka polepole kutokana na mafarakano ya ndani na uvamizi wa makabila ya Wahunni kutoka Asia ya Kati.
Chanzo
haririWafalme wa Gupta kiasili walikuwa watawala wadogo katika kazkazini ya Uhindi katika eneo lililopo leo kati ya Bengali ya Magharibi na Bihar.
Si rahisi kutofautisha watawala wa kwanza; majina kama Sri Gupta, Gupta na Chandragupta yanazajwa kifupifupi tu katika vyanzo vya kihistoria.
Uenezi wa eneo
haririChandragupta I (mnamo 320–335 BK) alimwoa Kumaradevi binti wa mfalme jirani akarithi ufalme wake wa Magadha (katika Bihar) na hivyo kupanusha eneo lake. Katika sarafu alijiita "Maharajadhiraja" yaani "mfalme mkubwa juu ya wafalme".
Mwanawe Samudragupta (mnamo 335–375) alivamia falme ndogo za jirani. Alitoa sarafu za dhahabu alipoonyeshwa kama mwanamuziki.
Kilele cha milki chini ya Chandragupta II
haririAlifuatwa na Chandragupta II (375–413/15) aliyefanya milki dola kubwa kabisa katika Bara Hindi. Alijiunga na majirani wakubwa kwa njia ya ndoa. Alipomwoa binti wa mfalme katika kusini ya Uhindi alipata uhuru kwa kushambulia majirani madogo zaidi katika kaskazini na magharibi.
Uchumi ulistawi vizuri katika ufalme huu mubwa. Mfalme aliwaachia wafanyabiashara na mafundi katika miji uhuru wa kujitawala. Wafanyabiashara walisafiri hadi China, Afrika ya Kazkazini na Bahari ya Mediteranea.
Mtawa Mbuddha Faxian kutoka China alitembelea Uhindi mnamo 399–412 akaandika: "Wananchi ni matajiri. Hawatozwi kodi za binafsi na hawabanwi katika shughuli zao. Wale pekee wanaolima ardhi ya mfalme walipa kodi ya mashamba. Wanaweza kubaki au kuondoka. Mfalme anatawala nchi bila kutumia adhabu ya mauti. Hata wasaliti wanakatwa mkono tu."
Kuporomoka kwa milki ya Gupta
haririKatika karne ya 5 uwezo wa Gupta ilipungua. Kwanza wakubwa waliopewa majimbo ya milki walianza kujiona kama watawala wenyewe na kodi hazikurudishwa ipasavyo hadi mji mkuu.
Kutoka kazkazini makabila ya Wahunni ya Asia ya Kati yalianza kusogea dhidi ya mipaka ya milki. Skandagupa alifaulu kuwapiga na kurudisha katika mapigano makubwa mnamo mwaka 458.
Kuanzia mwaka 500 kuna majina ya wafalme watano katika muda mfupi. Haijulikani kama walikufa mapema au kama walipinduliwa lakini badiliko la mara kwa mara lilidhoofisha milki. Mashambulio ya Wahunni yalianza tena na sasa walifaulu kuvamia Kashmir na kuwarudisha watawala wa Gupta zaidi kuelekea mashariki.
Mnamo mwaka 550 BK milki kubwa ilikwisha. Watawala wadogo wa kieneo walijitegemea na kupigana kati yao.
Watawala wa nasaba ya Gupta
hariri- Gupta (mnamo 275-300)
- Ghatotkacha (mn. 300-320)
- Chandragupta I. (320-335)
- Samudragupta (335-375)
- Ramagupta mn. 375 (?)
- Chandragupta II. (375-413/5)
- Kumaragupta I. (415-455)
- Skandagupta (455-467)
- Purugupta (mn. 467-472)
- Narasimhagupta Baladitya (mn. 472/73)
- Kumaragupta II. (mn. 473-476)
- Budhagupta (mn. 476-495)
- watawala mbalimbali mnamo mwaka 500, ufuatano wao haueleweki vizuri:
- Chandragupta III.
- Vainyagupta mn. 507 (huko Bengali?)
- Bhanugupta mn. 510 (huko Malwa?)
- Narasimhagupta Baladitya II. mn. 500-530
- Kumaragupta III. Kramaditya (mn 532)
- Vishnugupta Chandraditya (ca. 550)
Dini
haririWafalme wa Gupta walifuata Uhindu wakajenga mahekalu mazuri. Uhindu uliona matengenezo na upata nguvu upya. Mfumo wa kupanga wananchi katika varna yaani tabaka za kurithiwa za askari, wafanyabiashara na wakulima uliimarishwa tena. Walivumulia pia dini za Ubuddha na Ujain na kujenga mahekalu yao.
Elimu
haririKati ya wataalamu wakuu wa enzi hili alikuwa Aryabhata aliyebuni nafasiy a sifuri katika hisabati na kufundisha ya kwamba dunia inazunguka jua. Aliangalia pia kupatwa mwezi na jua na kufanya makadirio ya kanuni zake. Hisabati ya mfuno wa desimali ilibuniwa. Alitambua ya kwamba nuru ya mwezi na sayari ina asili yake katika kuakisi nuru ya jua.
Fasihi ya Kisanskrit ilifikia kilele chake. Kitabu mashuhuri cha Sushruta Samhita kinachoeleza elimu ya tiba ya Ayurveda pamoja na maelezo juu ya upasuaji wa mwili wa kibinadamu kilitungwa pia wakati wa Gupta.
Jeshi na Vita
haririHatuna taarifa nyingi za kihistoria za undani lakini uenezaji wa milki na habari chache zinaonyesha kuwa Wagupta walikuwa mfumo wa kijeshi uliowawezesha kushinda maadui.Taarifa kadhaa zimehifadhiwa kutoka kwa wageni Wachina na kutoka magharibi waliotembelea milki ya Gupta.
Kama falme nyingine za Uhindi jeshi la Gupta lilitumia tembo wa kijeshi na pia askari farasi wazito waliokingwa kwa nguo za chuma pamoja na farasi zao. Andiko moja la zamani ile ambalo linaitwa Siva-Dhanur-veda linatoa maelezo mengi hasa juu ya matumizi ya upinde[1].
Mapigano kwa pinde yalitazamiwa njia bora ya vita. Wagupta walitumia pinde za feleji au mianzi. Mishale ilikuwa pia ya mwanzi mwenye ncha ya metali. Upinde mrefu wa Kihindi ulikuwa silaha kali iliyofika mbali ikaweza kutoboa hata kingo la askari farasi. Askari upinde walitumia pia mishale za chuma dhidi ya tembo walioshambulia na mishale ya moto iliyowaka.
Askari upinde walilindwa na askari wengine waliotumia mkuki, ngao na upanga. Wagupta walitumia pia mashine za kivita kama vile mashine ya fyata.
Wakati wa utawala wa Chandragupta II milki yake ilikuwa na jeshi lenye askari wa miguu 500,000, askari farasi 50,000, askari wa magari ya farasi 20,000 na tembo 10,000. Alikuwa pia na jeshi la maji lenye manowari zaidi ya 1,200.
Sanaa
haririKipindi cha Gupta hutazamiwa kama kilele cha maendeleo ya sanaa katika kaskazini ya Bara Hindi. Kuna dalili ya kwamba uchoraji ulitumiwa sana lakini kuna mabaki machache tu. Kazi zilizodumu katika hali hewa ya Uhindini ni hasa uchongaji wa kidini katika jiwe.
Sanamu za miungu ya Kihindu zilichongwa kwa mtindo unaorudiwa hadi leo, vilevile sanamu za Buddha na Thirtankara wa Ujain. Kulkuwa na mahali pawili palipokuwa vitovu vya sanaa hii ambapo ni Mathura and Gandhara. Gandhara walichonga kwa mtindo wa Kigiriki (sehemu za magharibi kabisa za Uhindi ziliathiriwa na sanaa ya Kigiriki tangu kuingiliwa na Aleksanda Mkuu katika karne ya 3 KK). Wasanii walipeleka sanamu zao kutoka hapa kwendamaeneo mengine au walisafiri weyewe kwa kazi za sanamu kubwa sana.
Kipindi hiki hakina mifano ya sanamu za watawala.
Ajanta ina mifano bora za uchoraji uliohifahiwa kwenye kuta ndani ya pango. Uzuri wake ni dalili ya kwamba wasanii walikuwa na uzoefu mkubwa wa kuchora ukutani, labda kwenye kasri na majumba ya kifalme. Hekalu ya Dashavatara ilikuwa hekalu kubwa pale Deogarh inaonyesha mifano ya uchongaji mzuri.
Picha
hariri-
Vishnu, enzi za Gupta, Makumbusho ya Taifa mjini New Delhi
-
Buddha kutoka Sarnath, kare ya 5–6 BK
-
Trimurti (nyuso 3 za Mungu) kwenye Mapango ya Elephanta
-
Uchoraji wa Padmapani kwengo pango la Ajanta
Marejeo
hariri- ↑ Maelezo ya Dhanurveda
- ↑ "Hindu Art;Vishnu". Encyclopædia Britannica. Iliwekwa mnamo 2010-03-25.
- ↑ "Wonderful Indonesia - Borobudur: A Wonder of Indonesia History". Indonesia.travel. 26 Septemba 2012. Iliwekwa mnamo 2013-01-26.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link)
- Harle, J.C., The Art and Architecture of the Indian Subcontinent, 2nd edn. 1994, Yale University Press Pelican History of Art, ISBN 0300062176
- Majumdar, R.C. (1977). Ancient India, New Delhi:Motilal Banarsidass, ISBN 81-208-0436-8
- Raychaudhuri, H.C. (1972). Political History of Ancient India, Calcutta: University of Calcutta ISBN 1-4400-5272-7
- Shiv Chhatrapati 14 February 2013 @ 5:43 pm
- Tej Ram Sharma (1978). Personal and geographical names in the Gupta inscriptions. Concept Publishing Co., Delhi.
Viungo vya Nje
hariri- Frontline Article on Gupta Period Art Ilihifadhiwa 4 Desemba 2008 kwenye Wayback Machine.
- Regents Prep:Global History:Golden Ages:Gupta Empire Ilihifadhiwa 17 Desemba 2008 kwenye Wayback Machine.
- Inscriptions of the Guptas and their contemporaries Ilihifadhiwa 24 Septemba 2015 kwenye Wayback Machine.
- Coins of Gupta Empire
- Photo Feature on Gupta Period Art
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Milki ya Gupta kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |