Jina la Bayer (kwa Kiingereza Bayer designation) ni utaratibu wa kutaja nyota ulioanzishwa na mwanaastronomia Mjerumani Johann Bayer katika karne ya 17 na kutumiwa hadi leo kwa kutaja nyota angavu.

Muundo wa majina ya Bayer

Jina la Bayer huwa na sehemu mbili:

Mpangilio

Kwa kawaida nyota angavu zaidi huitwa "Alfa", nyota angavu ya pili "Beta" na kadhalika, kufuatana na utaratibu wa alfabeti ya Kigiriki na mwangaza unaoonekana wa nyota ndani ya kundinyota.

Lakini kuna mifano ambapo si nyota angavu zaidi iliyopokea "Alfa", ama kwa sababu Bayer alishindwa kuitambua sawasawa kwa vifaa alivyokuwanavyo wakati ule, au kwa sababu wakati mwingine alifuata tu ufuatano wa nyota jinsi unavyoonekana angani.

Kati ya kundinyota 88 zinazotambuliwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kuna 30 ambako nyota ya "Alpha" si angavu zaidi katika kundi lake. Kundinyota 4 zinakosa "Alfa" kabisa kwa sababu hapo mipaka kati ya kundinyota zilibadilishwa baadaye, lakini majina yalijulikana tayari kwa nyota zilizobaki.

 
Kundinyota Jabari (Orion) na nyota zake

Mfano wa majina ya Bayer katika kundinyota Jabari (Orion)

Katika kundinyota ya Jabari Bayer alitumia madaraja sita ya mwangaza yaliyokuwa kawaida wakati wake bila kutofautisha mwangaza ndani ya kila daraja. Kuna nyota mbili za daraja la kwanza yaani Ibuti la Jauza (Betelgeuse) na Rijili Jabari (Rigel), alizozipanga kuanzia kaskazini kwenda kusini, hivyo Ibuti la Jauza ilipokea "α" na Rijili Kantori ilipokea "β" ingawa ni angavu zaidi.

Halafu Bayer aliendelea kupanga nyota za daraja la pili vilevile kuanzia kaskazini kwenda kusini bila kutofautisha mwangaza ndani ya daraja hili.

Jina la
Bayer
Mwangaza
unaoonekana
Jina
α Ori 0.45 Ibuti la Jauza (Betelgeuse)
β Ori 0.18 Rijili Jabari (Rigel)
γ Ori 1.64 Najida (Bellatrix)
δ Ori 2.23 Mintaka
ε Ori 1.69 Nidhamu (Alnilam)
ζ Ori 1.70 Alnitak

Kasoro na mifumo mbadala

Utaratibu ulikuwa na matatizo katika kundinyota kubwa ambako idadi ya nyota zinazoonekana inazidi ile ya herufi za Kigiriki. Hapo Bayer aliongeza herufi za Kilatini na namba.

Kasoro hizo zilikuwa sababu mojawapo kwa Mwingereza John Flamsteed kuanzisha mfumo wake wa namba za Flamsteed. Hata hivyo kwa nyota angavu nyingi majina ya Bayer yanaendelea kutumiwa. Siku hizi namba za Flamsteed hutumiwa pamoja na majina ya Bayer hasa pale ambapo zinahusu nyota ambazo Bayer hakutolea majina, kwa mfano kwa sababu Bayer aliorodhesha 1,564 nyota pekee zinazoonekana kwa macho matupu ilhali Flamsteed alitumia darubini na hivyo aliorodhesha nyota 2,554. Mara nyingi namba za Flamstee zimekuwa kawaida pia pale ambapo Bayer alilazimishwa kuongeza herufi za Kilatini au namba kwa zile za Kigiriki kutokana na idadi ya nyota katika kundinyota fulani. Kwa mfano namba ya Flamsteed "55 Cancri" hupendelewa kuliko jina la Bayer "Rho-1 Cancri".

Leo hii idadi ya nyota zinazojulikana imeongezeka sana: kuna nyota bilioni kadhaa zinazoweza kutambuliwa kwa vifaa vya kisasa kama darubini zinazopima mawimbi ya spektra mbalimbali nje ya nuru inayoonekana pamoja na darubini kwenye anga-nje kama Hubble, Hipparcos na Gaia. Hapo kuna orodha mbalimbali ambamo nyota zinaorodheshwa kwa namba tu. Mifano inayotajwa sana ni orodha ya Henry Draper Catalogue (kifupi: HD), ya Bright Star Catalog (kifupi HR), ya Hipparcos catalogue (Kifupi HIP) na ya Gaia Catalogue inayoendelea kupanuka ilhali kazi ya chomboanga hiki kinaendelea.

Marejeo

  1. Jina la kundinyota linaandikwa kwa umbo la uhusika milikishi (en:genitive) mfano "Orionis" badala ya "Orion" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Orionis, n.k.