Oskar Baumann

(Elekezwa kutoka Oscar Baumann)

Oskar Baumann (pia Oscar Baumann, *25 Juni 1864 Vienna, Austria - +12 Oktoba 1899 Vienna) alikuwa mwanajiografia na mchunguzi wa Afrika kutoka Austria. Anakumbukwa kwa ramani na vitabu ambako alieleza kwa umakini maeneo mbalimbali ya Afrika, hasa katika Tanzania na Rwanda ya leo, aliyowahi kupita kwenye safari zake pamoja.

Oskar Baumann akiwa balozi wa Austria huko Zanzibar
Ramani ya mji wa Zanzibar iliyochorwa na Baumann mnamo 1892
Ramani ya Usambara iliyopimwa na kuchorwa na Baumann mnamo 1888

Familia na elimu

hariri

Oskar Baumann alizaliwa mjini Vienna iliyokuwa wakati ule mji mkuu wa milki ya Austria-Hungaria. Babake alifanya kazi ya benki. Oskar alipita shule za msingi na sekondari akaanza masomo ya jiografia kwenye Chuo Kikuu cha Vienna akaendelea kusoma uchoraji wa ramani kwenye taasisi ya jiografia ya jeshi. Alipokuwa na miaka 19 alisafiri katika Montenegro akachora ramani za milima yake.

Safari za uchunguzi

hariri

Matokeo mazuri yalimpatia nafasi katika safari ya upelelezi wa beseni ya Kongo iliyotumwa na shirika la jiografia la Austria mwaka 1885 alipofaulu kuchora ramani halisi za kwanza za mto Kongo.

1886 Baumann alitembelea kisiwa cha Fernando Poo na kuchunguza jiografia na utamaduni wa wakazi wake. Baada ya kurudi Ulaya alitumia uchunguzi wake kwa kuandika tasnifu iliyompatia shahada ya uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Leipzig (Ujerumani).

Mwake uleule alikaribishwa na Hans Meyer [1] kuja Afrika ya Mashariki ambako koloni ya Kijerumani ilianzishwa. Baumann aliyeelekea Kilimanjaro alianza kazi za kupima maeneo ya Usambara. Hapo alikamatwa na askari wenyeji waliopinga ukoloni katika Vita ya Abushiri akawa mfungwa wa Abushiri mwenyewe. Alifaulu kumwomba kuhifadhi karatasi zake zote zenye vipimo vya maandalizi ya ramani halafu Meyer na Baumann waliachishwa kwa ahadi ya kulipa fidia.

1899 alienda tena Montenegro akiendelea kuchora ramani za milima yake.

Katika Januari 1890 alirudi Afrika ya Mashariki akapita maeneo yote ya Usambara akaendelea kupima Upare hadi kilimanjaro halafu Useguha. Hapo alikagua nafasi za kujenga reli iliyopangwa Tanga-Korogwe. Taarifa ya safari hii inapatikana katika kitabu chake kuhusu Usambara na maeneo jirani[2] kinachotunza habari nyingi kuhusu vijiji, uchumi, utamaduni na historia ya wenyeji.

Baada ya kurudi Ujerumani alitumwa tena Afrika ya Mashariki kwa mara ya tatu kuanzia 1891 hadi 1893, sasa kwa shabaha ya kupeleleza maeneo upande wa kusini ya Ziwa Viktoria Nyanza kwa niaba ya Kamati ya Kijerumani ya Kupambana na Utumwa. Baumann alipewa pesa ya kutosha ya kuajiri wapagazi na askari 200 pamoja na vifaa vya lazima kwa kundi kubwa hivi akaondoka nao kutoka Bagamoyo akiwa mzungu wa pekee katika safari hii. Alipita katika Umasaini wakati wa njaa kubwa na baada ya kufika Viktoria Nyanza aliamua kutafuta chanzo cha mto Naili. Hivyo alipita Burundi akawa Mzungu wa kwanza aliyefika Rwanda.

1895 alirudi tena akipeleleza na kuchora funguvisiwa ya Unguja na pia bonde la mto Pangani.

Mwaka uliofuata alipewa nafasi ya balozi wa Austria-Hungaria katika Zanzibar. Lakini miaka ya nyumba aliteswa tena na tena na homa ya malaria; wakati wa kutembelea Austria alifariki mjini Vienna mnamo 12 Oktoba 1899.

Maandiko yake

hariri

Sehemu kubwa ya vitabu vyake inapatikana kwa Kijerumani tu.

  • Beiträge zur Ethnologie des Congo, 1887 (kuhusu watu na makabila wa Kongo).
  • Versuch einer Monographie von Fernando Póo, 1888 ("Jaribio la maelezo kuhusu Fernando Poo; tasnifu yake).[3]
  • Fernando Po and the Bube. Vienna (1888).
  • In Deutsch-Ostafrika während des Aufstandes (Katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumano wakati wa uasi - masimulizi ya safari na kukamatwa kwake wakati wa vita ya Abushiri), Vienna (1890) (online hapa).
  • Usambara und seine Nachbargebiete. Allgemeine Darstellung des nordöstlichen Deutsch - Ostafrika und seiner Bewohner, Berlin 1891 (Usambara ma maeneo jirani. Maelezo ya kaskazini-mashariki ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na wakazi wake) online hapa.
  • Karte des nordöstlichen Deutsch-Ostafrika (Ramani ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani), Berlin (1893).
  • Durch Massailand zur Nilquelle (Kupitia Umasaini hadi chanzo cha Naili), Berlin (1894).
  • Die kartographischen Ergebnisse der Massai-Expedition (Matokeo ya safari ya Umasaini kwa uchoraji wa ramani), In: Petermann's Geographische Mitteilungen, Ergebnisheft 111, Gotha (1894).
  • The Sansibar archipelago. 3 booklets. Leipzig (1896–99).
  • Afrikanische Skizzen (Picha kutoka Afrika), Berlin (1900).[4]

Tanbihi

hariri
  1. Meyer alikuwa mmoja wa kundi la kwanza lililopanda baadaye mlima Kilimanjaro
  2. Usambara und seine Nachbargebiete, (18912)
  3. OCLC WorldCat List of published works
  4. HathiTrust Digital Library published works

Viungo vya Nje

hariri