Patasi (kundinyota)

Patasi (kwa Kilatini na Kiingereza Caelum[1]) ni jina la kundinyota ndogo kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu. Jina linataja zana ya patasi.

Nyota za kundinyota Patasi (Caelum) katika sehemu yao ya angani

Mahali pakeEdit

Patasi lipo jirani na kundinyota za Panji (Dorado [2]) na Mchoraji (Pictor) upande wa kusini, Saa (Horologium) na Nahari (Eridanus, kwa maana ya mto) upande wa mashariki, Arinabu (Lepus, kwa maana Sungura) upande wa kaskazini halafu Njiwa (Columba) upande wa magharibi.

JinaEdit

Patasi ni kati ya kundinyota zilizobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kutoka nusutufe ya kusini pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Kundinyota hii ilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “ Caela Sculptoris“ lililomaanisha “ Patasi za mchongaji“. Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za anga ya kusini ambazo zilianza tu kujulikana na wanaastronomia wa Ulaya wakati ule. Hapo alipima nyota 10,000 akazipanga kwa kundinyota na kutunga majina kwa kundinyota mpya 14[3]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Caelum"[4] (Patasi). Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale.

Patasi ipo kati ya kundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [5] kwa jina la Caelum. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Cae'.[6]

NyotaEdit

Nyota za Patasi ni chache na dhaifu; angavu zaidi ni Alpha Caeli ambayo ni nyota maradufu yenye mwangaza unaoonekana wa mag 4.45 ikiwa na umbali wa miakanuru 65.8 kutoka Dunia. [7][8]

TanbihiEdit

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Caelum " katika lugha ya Kilatini ni "Caeli" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Caeli, nk. „Caelum“ kwa maana hii ni tofauti na neno „coelum“ inayoandikwa pia „caelum“ yenye maana ya „anga, mbingu“
  2. inamaanisha samaki ya aina Coryphaena
  3. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  4. caelum ni umoja wa uwingi „caela“
  5. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  6. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. https://archive.org/details/sim_popular-astronomy_1922-10_30_8/page/469.
  7. * Alpha Caeli – Star in double system. SIMBAD. Iliwekwa mnamo 13 January 2013.
  8. GJ 174.1 B – Flare star. SIMBAD. Iliwekwa mnamo 13 January 2013.

Viungo vya NjeEdit

  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Patasi (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Mradi wa Astronomia Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano