Pyrrhus au Pyrrhos (kwa Kigiriki: Πύρρος της Ηπείρου, Pyrrhos tes Epeiru; 319272 KK) alikuwa mfalme wa Epirus katika Ugiriki ya Kale wa enzi ya Uheleni.

Sanamu ya Pyrrhus. Makumbusho ya Kitaifa ya Akiolojia, Napoli, Italia

Alizaliwa baada ya kifo cha Aleksander Mkuu, kwa hiyo alikuwa mtoto wakati wa mvurugo wa mapambano baina ya majenerali wa Aleksander Mkuu. Kwa msaada wa Ptolemaio I wa Misri aliweza kushika urithi wa baba yake na kuwa mfalme[1].

Mnamo mwaka 280 KK aliitikia ombi la mji wa Kigiriki Taranto kusini mwa Italia uliotafuta msaada dhidi ya upanuzi wa Jamhuri ya Roma.[2]

Kwa msaada wa wafalme wengine wa Ugiriki alikusanya jeshi la askari wa miguu 20.000, askari farasi 3.000, wapiga mishale 2.000, wapiga manati 500 na tembo wa vita 20. Baada ya kufika Italia alishinda jeshi la Roma katika mapigano mawili. Hata hivyo, alipoteza askari wengi hadi kusema "ushindi mmoja tena wa namna hii na tutakuwa tumekwisha"[3]. Kwa hiyo ushindi unaoleta hasara kubwa kwa mshindi huitwa "ushindi wa Pyrrhus" (kwa Kiing. Pyrhic victory).

Baada ya mapigano mengine alishindwa na Waroma huko Benevento kwenye mwaka 275 KK na hapo alirudi Ugiriki. Alikuta nchi katika hali ya vita kati ya milki ndogo. Wakati wa kuvamia mji Argos aliuawa katika mapigano.

Marejeo hariri

Kujisomea hariri

Viungo vya Nje hariri