Kuhusu mtaalamu mashuhuri wa karne ya 2 BK angalia Klaudio Ptolemaio

Sanamu ya kichwa cha Ptolemaio I; Jumba la makumbusho la Louvre, Paris
Sarafu ya Ptolemaio I

Ptolemaio I Soter (kwa Kigiriki: Ptolemaîos Sōtḗr, yaani "Ptolemaio Mwokozi "; mnamo 367 KK - Januari 282 KK) alikuwa rafiki wa Aleksander Mashuhuri na jenerali katika jeshi lake. Baada ya kifo cha Aleksander mwaka 323 KK aliendelea kuwa mtawala wa Misri akajitangaza farao (mfalme).

Alitawala hadi 305/304 KK[1] akaunda nasaba ya Waptolemaio iliyoendelea karne 3 hadi Kleopatra.

Asili yake

hariri

Ptolemaio I alizaliwa Masedonia, kaskazini mwa Ugiriki akiwa mwana wa Arsinoe wa Makedonia na mumewe Lagus, lakini kuna pia uwezekano kwamba ni mfalme Filipo II wa Makedonia, baba wa Aleksander, aliyemzaa. Ptolemaio alikuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Aleksander.

Jenerali wa Aleksander

hariri

Wakati wa vita katika Uajemi Ptolemaio alikuwa mmoja wa viongozi wakuu chini ya Aleksander akamkamata Bessos mfalme wa mwisho wa Waajemi. Kwenye mapigano ya Sogdia (Asia ya Kati) aliongoza kitengo kikubwa cha jeshi; kwenye mapigano ya Uhindi alisemekana aliokoa uhai wa Aleksander na ndiyo asili ya jina lake "soter" (mwokozi, mwokoaji).

Kati ya waandamizi

hariri

Baada ya kifo cha Aleksander mjini Babeli mnamo 323 KK, majenerali wake waligawana himaya yake kubwa, mwanzoni kwa nia ya kuitunza kwa ajili ya mtoto wa marehemu. Ptolemaio alipewa mamlaka juu ya Misri. Lakini umoja wa waandamizi wa Aleksander uliporomoka haraka na kipindi cha vita kati yao kilifuata kilichokwisha mwaka 301 KK na tangu mwaka huo himaya ya Aleksander ilikwisha ikigawiwa katika himaya za waandamizi wake. Wakati maiti ya Aleksander ilihamishwa kutoka Babeli kwenda kuzikwa nyumbani kwake Masedonia, Ptolemaio aliichukua kwa nguvu na kuiweka huko Memphis, baadaye ilihamishiwa Aleksandria kwenye kaburi jipya.

Alishambuliwa na mwandamizi mwingine, Perdikkas lakini shambulio hilo lilishindikana. Ptolemaio aliweza kuimarisha utawala wake juu ya Misri.

Mtawala wa Misri

hariri

Katika mfululizo wa vita baina ya waandamizi wa Aleksander, Ptolemaio aliweza kupanua eneo lake juu ya Yudea akachukua pia udhibiti wa Kupro na Kirenaika. Katika vita zilizofuata kati ya waandamizi, Antigonos (wakati ule mtawala wa Anatolia au Uturuki wa leo) alichukua cheo cha mfalme akidai kuwa mrithi pekee wa Aleksander. Hatua hiyo ilisababisha pia waandamizi wengine kujiita wafalme, pamoja na Ptolemaio aliyetumia cheo cha kale cha wafalme wa Misri akijiita farao.

Ptolemaio alioa wake mbalimbali; mke wake wa mwisho alikuwa Berenike kutoka Masedonia, na mwana wao akawa mrithi wake, Ptolemaio II.

Ptolemaio I alifariki mwaka 282 KK. Kabla ya kifo chake alianzisha Maktaba mashuhuri ya Aleksandria.

Marejeo

hariri
  1. Hölbl, Günther (2013). A History of the Ptolemaic Empire. Routledge. uk. 21. ISBN 9781135119836.

Kujisomea

hariri
  • Walter M. Ellis: Ptolemy wa Misri, London: Routledge. 1993. ISBN 9780415100205
  • Christian A. Caroli: Ptolemaios I. Soter - Herrscher zweier Kulturen, Konstanz: Badawi. 2007. ISBN 9783938828052
  • Waterfield, Robin (2011). Dividing the Spoils – The War for Alexander the Great's Empire (hardback). New York: Oxford University Press. ISBN 978-0-19-957392-9.978-0-19-957392-9
  • McKechnie, Paul na Jennifer A. Cromwell (eds). Ptolemy I na Mabadiliko ya Misri, 404-282 KWK . Leiden, NL; Boston, MA: Brill, 2018. ISBN 978-90-04-36696-1 .

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Ptolemaio I
Born: 367 KK Died: 282 KK
Alitanguliwa na
Aleksander Mkuu
Farao wa Misri
305/304–282 KK
Akafuatiwa na
Ptolemaio II