Geji sanifu
Geji sanifu (kwa Kiingereza: standard gauge [1]) ni geji (yaani kipimo cha umbali kati ya pau mbili za njia ya reli) inayotumika zaidi duniani. Takriban asilimia 55 za njia zote za reli duniani zinatumia geji hii yenye upana wa milimita 1,435.[2]
Hasa njia zote za reli ya mkasi mkubwa (isipokuwa Urusi, Uzbekistan na Ufini) hutumia geji sanifu.
Geji sanifu katika Afrika ya Mashariki
haririReli za Afrika ya Mashariki zilianzishwa wakati wa ukoloni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na wakati ule geji nyembamba ya mita 1 ilichaguliwa kwa kusudi la kupunguza gharama za ujenzi. Njia ya TAZARA pekee kati ya Dar es Salaam na Zambia ina upana wa milimita 1067 ambayo ni kawaida ya mtandao wa Afrika ya Kusini.
Tangu miaka ya 2000 hivi ilionekana ya kwamba hali ya miundombinu ya reli hizi ilichakaa mno na kuanzia mwaka 2004 mipango ilianza ya kutengeneza upya reli katika Afrika ya Mashariki. Mpango Mkuu wa Usafiri wa Reli katika Afrika ya Mashariki (East African Railway Master Plan) ulikuwa tayari mwaka 2009 ukipendekeza njia mpya za geji sanifu (zilizokuwa maarufu kwa kifupi chake "SGR", yaani standard gauge rail) za kuunganisha Kenya na Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini, halafu Tanzania na Burundi na Rwanda hadi Uganda.
Reli ya SGR itaruhusu treni za mkasi mkubwa zaidi jinsi ilivyo sasa. Inaruhusu pia mabehewa kubeba mizigo mizito zaidi na hivyo kuongeza kiasi cha mzigo kwa kila behewa.
Reli ya SGR Kenya
haririReli ya SGR ya Kenya ilianza kujengwa Kenya mwana 2011 ambako njia ya SGR kati ya Mombasa na Nairobi ilifunguliwa mwezi Juni 2017. Njia hii inatarajiwa kuendelea hadi Kisumu kupitia Naivasha na hatimaye hadi Malaba kwenye mpaka wa Uganda[3].
Reli ya SGR Tanzania
haririTazama makala kuu Reli ya SGR Tanzania
Mwaka 2017 ulianza ujenzi wa awamu ya kwanza ya njia ya SGR nchini Tanzania inayolenga kuunganisha Dar es Salaam na Morogoro[4]. Njia hii inatarajiwa kuendelea hadi Mwanza na hatimaye hadi Burundi.
Tarehe 14 Juni 2024 treni ya kwanza ilisafiri toka Dar es Salaam hadi Morogoro, tangu saa 12:01 asubuhi hadi 1:55 asubuhi. Ilikuwa na mabehewa 14 na abiria 600-700 hivi.
Marejeo
hariri- ↑ Pia Stephenson gauge kutokana na mhandisi George Stephenson, international gauge au normal gauge
- ↑ Marekani pekee haikubali bado vipimo vya milimita, inaeleza geji sanifu kuwa na futi 4 na inchi 8 na nusu, ambayo ni sawa na milimita 1,435
- ↑ Standard Gauge Railway Development in Kenya Archived 21 Mei 2017 at the Wayback Machine., tovuti ya Kenya Railways Company, iliangaliwa Mei 2017
- ↑ Turkish, Portuguese firms win bid to construct Tanzania’s SGR , tovuti ya theeastafrican.co.ke ya 6 Februari 2017, iliangaliwa Mei 2017