Kaa (pia: Saratani au lat.&ing. Cancer[1] kwa Kilatini/Kiingereza) ni kundinyota la zodiaki. Ni moja ya makundinyota yanayotambuliwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2]

Nyota za kundinyota Kaa (pia Saratani, lat. Cancer) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Kaa - Cancer jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini
Kaa - Saratani jinsi ilivyowazwa na msanii Hall

Nyota za Kaa huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Kaa" linaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Dunia.

Jina

Mabaharia Waswahili walijua nyota hizi tangu miaka mingi kwa jina la Saratani wakizitumia kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[3]

Jina la Saratani linatokana na Kiarabu سرطان saraṭaan linalomaanisha kaa[4]. Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Wagiriki wa Kale waliosema Καρκίνος karkinos kwa maana hiyohiyo na hao walipokea kundinyota hili tayari kutoka Babeli lakini Wababeli waliiona kama alama ya kobe maji.

Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Saratani" limesahauliwa ikiwa kundinyota linaitwa kwa tafsiri tu "Kaa".

Katika vitabu kadhaa vya shule jina la Saratani limetumiwa kutaja sayari ya Zohali kwa kulichanganya na matamshi ya jina la Kiingereza "Saturn".

Jina la zamani, pia jina la Kilatini, ni sawa na ugonjwa wa saratani unaoitwa pia "kansa". Sababu yake ni ya kwamba matibabu wa kale walifananisha uvimbe wa ugonjwa na mnyama kaa na hili ni pia maana ya neno saratani.

Mahali pake

Kaa iko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Mapacha (zamani Jauza, lat. Gemini) upande wa magharibi na Simba (zamani Asadi, lat. Leo) upande wa mashariki.

Magimba ya angani

Kaa haina nyota angavu sana si rahisi kuiona. Nyota angavu zaidi ni Beta Cancri yenye mwangaza unaoonekana wa 3.8 mag. Umbali wake na dunia ni miakanuru 230. Kuna fungunyota moja inayoonekana kwa macho matupu hii ni M 44 inayoitwa pia Praesepe yenye mwangaza unaoonekana wa 3.7 ikionekana kama doa dogo angavu.

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
β 17 Acubens 3,53m 230 K4 III
δ 47 Asellus Australis 3,94m 150 K0 III
ι 48 3,9 m 300 G6 + A3
α 65 Acubens 4,26m 180 A3
γ 43 Asellus Borealis 4,66m 160 A1 V
ζ 16 Tegmine 4,7 ca. 82 F7 V + F9 V + G0 V + M

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Cancer" katika lugha ya Kilatini ni "Cancris" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Cancris, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. ling. Knappert 1993
  4. Ugonjwa wa saratani au kansa ulipokea jina lake kwa sababu matibabu wa Ugiriki ya Kale waliona uvimbe wake unafanana na miguu ya mnyama kaa.

Viungo vya Nje


Marejeo

  • Ian Ridpath and Wil Tirion (2007). Stars and Planets Guide, Collins, London. ISBN 978-0007251209. Princeton University Press, Princeton. ISBN 978-0-691-13556-4.
  • Dictionary of Symbols, by Carl G. Liungman, W. W. Norton & Company. ISBN 978-0-393-31236-2
  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 107 ff (online kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331


 
WikiMedia Commons


  Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)
 

Kaa (Saratani – Cancer  )Kondoo (Hamali – Aries  )Mapacha (Jauza – Gemini  )Mashuke (Nadhifa – Virgo  )Mbuzi (Jadi – Capricornus  )MizaniLibra  )Mshale (Kausi – Sagittarius  )Ndoo (Dalu – Aquarius  )Nge (Akarabu – Scorpius  )Ng'ombe (Tauri – Taurus  )Samaki (Hutu – Pisces  )Simba (Asadi – Leo  )