Shirikisho la Ujerumani

Shirikisho la Ujerumani (Kijer.: Deutscher Bund") ilikuwa ushirikiano wa nchi za Ulaya ya Kati hasa za shemu za Ujerumani baada ya Mkutano wa Vienna 1815 hadi vita ya Prussia na Austria ya 1866.

Shirikisho la Ujerumani katika Ulaya.
Sehemu za nchi mbili kubwa ndani yake Austria na Prussia zilikuwa nje ya shirikisho

Nchi hizi ziliwahi kuwa sehemu za Dola Takatifu la Kiroma hadi 1806 iliyokwisha kutokana na vita za Napoleoni.

Nchi na maeneo ya kujitawala 38 zilijiunga ndani yake. Hizi zilikuwa nchi 34 zenye utaratibu wa kifalme (ufalme, utemi) na miji huru minne yenye katiba ya kijamhuri. Kila nchi ilijitawala na kujitegemea hata kimataifa.

Nchi mbili kubwa kati ya wanachama zilikuwa Dola la Austria na Ufalme wa Prussia. Zote mbili zilikuwa na maeneo makubwa ambayo yalihesabiwa kuwa nje ya eneo la shirikisho kwa sababu hazikuwahi kuwa sehemu za Dola Takatifu kabla ya 1806.

Shirikisho lilikuwa na nguvu wakati ambako Austria na Prussia zilishirikiana vizuri. Tangu 1860 na hasa tangu vita ya Schleswig ya 1864 uhusiano ulikuwa mbaya na kusababisha Vita ya Kijerumani ya 1866 iliyomaliza shirikisho.

Tokeo la vita lilkuwa ya kwamba Austria ilibaki nje ya siasa ya Kijerumani; sehemu kubwa ya Ujerumani iliunganishwa katika Shirikisho la Ujerumani ya Kaskazini chini ya uongozi wa Prussia na madola ya Ujerumani kusini kama Bavaria yalibaki pekee.

Katika vita ya Ujerumani na Ufaransa nchi za Ujerumani kusini zilishikamana na Prussia. Tokeo lake likuwa kuundwa kwa Dola la Ujerumani tar. 18 Januari 1871 mjini Versailles (Ufaransa).