Dola Takatifu la Kiroma

Dola Takatifu la Kiroma si sawa na Dola la Roma la Kale.

Dola Takatifu la Kiroma (Kijerumani: Heiliges Römisches Reich, Kilatini: Sacrum Romanum Imperium) lilikuwa jina la Ujerumani kati ya takriban mwaka 1000 na 1806. Lakini dola hilo, licha ya Ujerumani, lilikuwa pia na maeneo makubwa, yakiwa ni pamoja na Austria, Italia ya Kaskazini, Ubelgiji, Uholanzi na Ucheki wa leo.

Ramani ya Dola Takatifu la Kiroma yaonyesha mikoa yake.
Maeneo ya Dola Takatifu la Kiroma pamoja na mipaka ya nchi za sasa.

Mipaka yake yalibadilika mara kadhaa katika karne nyingi za kuwako kwake.

Tabia za Dola

hariri

Maeneo hayo yote yaliunganishwa chini ya Kaisari aliyekuwa pia mfalme wa Wajerumani.

Maeneo hayo yalikuwa na kiwango kikubwa cha kujitegemea yakitawaliwa na makabaila wa ngazi mbalimbali na maaskofu wa Kanisa Katoliki au yakiwa miji huru.

Halikuwa dola la kisasa, kwa kuwa vyombo vya dola vilikuwa vichache. Kaisari alitegemea hasa mali yake binafsi pamoja na haki ya kuthibitisha watu waliopokea vyeo mbalimbali.

Tangu 1438 hadi 1806 cheo cha Kaisari kilibaki katika familia ya Habsburg waliotawala Austria.

Chanzo baada ya Karolo Mkuu

hariri

Asili ya dola lilikuwa milki ya Karolo Mkuu aliyefaulu kuunganisha Ujerumani, Ufaransa na Italia chini yake. Mwaka 800 alipokea cheo cha Kaisari wa Roma kutoka mikono ya Papa Leo III.

Hatua hii ilichukuliwa kama kuendelezwa kwa Dola la Roma la Kale katika magharibi ya Ulaya hata kama hali halisi ilikuwa kwamba milki ya Karolo ilikuwa milki ya Wafranki na Wagermanik wengine na taasisi zote za Roma ya Kale zilikuwa zimeshakwisha kabisa katika magharibi ya Ulaya.

Yaliyobaki ya Roma ya Kale yaliendelea Ulaya mashariki kwa umbo la Milki ya Bizanti.

Lakini makaisari walijenga hoja la "translatio imperii" (kwa Kilatini: ukabidhi wa mamlaka) la kuwa mamlaka ya Kaisari yaliyokuwa na Waroma wa Kale na sasa yalikabidhiwa kwa Wajerumani.

Karolo aligawa urithi wake kati ya wanae na hii ilikuwa chanzo cha Ufaransa upande wa magharibi na Ujerumani upande wa mashariki. Cheo cha Kaisari kiliendelea upande wa mashariki. Hivyo Ufaransa iliendelea kuwa ufalme wa nchi moja lakini upande wa mashariki Wajerumani waliunganishwa pamoja na watu jirani chini ya Kaisari aliyekuwa pia mkuu wa Italia ya Kaskazini, Bohemia (Ucheki) na sehemu mbalimbali ambazo leo hii ni ama Ufaransa au Ubelgiji na Uholanzi.

Mjerumani wa kwanza aliyepokea ukaisari kutoka kwa Papa wa Roma alikuwa Otto I mwaka 962.

Dola likaendelea hadi 1806 wakati Napoleon alipolifuta.

Jina la "Dola Takatifu la Kiroma" lilianza kutumiwa tangu 1100 likaitwa baadaye pia "Dola Takatifu la Kiroma la Wajerumani".

Matatizo ya Dola

hariri

Hadi karne ya 13 dola lilikuwa na nguvu. Baadaye maeneo ndani yake yalijiongezea kiwango cha kujitawala. Kila Kaisari alichaguliwa na kamati ya makabaila na watemi wakuu. Kabla ya uchaguzi Makaisari walipaswa kuahidi ya kwamba wataheshimu haki ya makabaila juu ya maeneo yao. Mwishoni maeneo yalikuwa kama nchi huru kabisa yaliyoendelea kujitawala, kuendesha vita dhidi ya majirani kufuata siasa zao.

Mwishoni dola lilikuwa za zaidi ya maeneo 300 ya kujitegemea; mengine makubwa kama Austria na Prussia, mengine madogo mno yenye eneo la mji mmoja tu.

Tangu karne ya 16 dola halikuwa na uwezo tena wa kufuata siasa ya nje kwa pamoja isipokuwa dhidi ya Waturuki Waosmani walioshambulia mara mbili Vienna, mji mkuu wa makaisari (1529 na 1683).

Lakini vita vya kuwasukuma Waturuki watoke katika maeneo ya Ulaya ya kusini-mashariki waliyowahi kuvamia viliendeshwa na Kaisari kama mkuu wa Austria bila ya msaada wa dola takatifu.

Dola lilifaulu kwa kiasi fulani kutunza amani au angalau kuepuka vita kati ya maeneo yake. Isipokuwa Vita ya Miaka 30 kati ya 1618 na 1648 ilionyesha uwezo mdogo wa dola na karibu theluthi moja ya wakazi wa Ujerumani walikufa.

Tangu karne ya 17 majirani kama Ufaransa na Sweden walijiingiza zaidi na zaidi katika siasa ya Ujerumani na maeneo makubwa kama Prussia hayakujali tena maazimio ya Kaisari. Dola Takatifu likaendelea kudhoofika.

Vita vya Napoleon vilimaliza mabaki yake.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dola Takatifu la Kiroma kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.