Tafsiri
(Elekezwa kutoka Translation)
Tafsiri (Asili ya neno hili ni Kiarabu; kisawe cha neno hili ni Tarjuma) ni kazi ya kutoa maana ya maneno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Mtu anayefanya kazi hii huitwa mfasiri au mkalimani.
Kutafsiri kuna maana mbili kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK):
- Ni kutoa andiko au maelezo fulani katika lugha nyingine kwa maana ilele.
- Toa maelezo ya lugha fulani kwa lugha nyingine kwa maana ileile kwa kutumia maandishi. Katika maana ya pili, maana yake ni kitenzi elekezi, ni kitenzi ambacho kinapokea Yambwa, yaani nomino ya mtendwa.
Katika misingi ya kielimu dhana ya tafsiri imeweza kujadiliwa na wataalamu mbalimbali.
- Newmark (1982): Tafsiri ni jaribio la kuwasilisha ujumbe uleule ulioandikwa katika lugha moja kwa lugha nyingine.
- Mwansoko na wenzake (2006): Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji (Transferring) wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.
- Uhawilishaji ni kuhamisha mawazo au ujumbe kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine.
- Mfasiri ni mtu mwenye ujuzi mzuri wa lugha zaidi ya moja anayefanyakazi ya kutafsiri matini kutoka lugha moja kwenda nyingine. Mara nyingi mtu anayefanya kazi ya kutafsiri huwa anahawilisha matini kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Hasa katika maandishi.
- Matini ni maandishi yaliyomo katika andiko linalohusu jambo fulani. Matini inaweza kuwa riwaya, tamthiliya au ushairi. Kimsingi chochote kilichoandikwa ili kiweze kutolewa tafsiri huitwa matini.
Aina za matini
haririKuna aina kuu mbili za matini, ambazo ni:
- Matini chanzi/ Chasili (Source text): Ni matini ambayo iko katika lugha yake ya awali au lugha yake iliyoandikiwa kabla ya mchakato wa kutafsiri.
- Matini lengwa/ Tafsiri (Target text): Ni matini iliyotafsiriwa kutoka lugha yake iliyoandikiwa.
Kumbuka:
- Lugha Chanzi/Chasili (LC) ni lugha iliyotumika kuandikia matini chanzi (Source language)
- Lugha Lengwa (LL) (Target language) ni lugha iliyotumika kutafsiria matini chanzi au lugha unayoitumia kufanyia tafsiri.
Ugumu wa kutafsiri
haririHakuna tafsiri kamili kabisa. Kila mfasiri hana budi kuchagua kati ya mawili:
- Akikaa karibu zaidi kwa matini ya lugha ya asili, tafsiri yake inaweza kukosa uzuri katika lugha ya kutafsiriwa. Pia anaweza kukosa maana ya maneno ya asili hasa kama yalitumia methali au lugha ya mifano na lugha ya picha.
- Akielekea kutoa maana ya maneno asilia kwa umbo zuri katika lugha ya kutafsiriwa kuna hatari ya kwenda mbali kiasi na yale yaliyosemwa awali na kuingiza rai za mfasiri mwenyewe.
Viungo vya nje
haririWikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Tafsiri kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |