Wabunge wa kuteuliwa
Mbunge wa kuteuliwa ni mbunge ambaye hakuchaguliwa na wananchi lakini ameteuliwa bila uchaguzi.
Nchi mbalimbali huwa na wabunge wa kuteuliwa lakini katika nchi nyingi hawako.
Kwa kawaida idadi ya wabunge wa kuteuliwa ni ndogo ikilinganishwa na wabunge wa kuchaguliwa.
Mara nyingi haki ya kuteua wabunge imo mkononi mwa mkuu wa dola. Katika nchi kadhaa kuna kamati mbalimbali zinazoshughulika uteuzi.
Kusudi
haririKusudi la utaratibu huo unaelezwa kwa namna tofauti
- ni njia mojawapo ya kuingiza bungeni makundi ambayo yasingepatikana kwa njia ya kisiasa, kwa mfano wataalamu, wasanii, wawakilishi wa jumuiya ndogo
- katika nchi zenye mfumo wa Uingereza (Westminster) mawaziri wanateuliwa kutoka kwa wabunge; mfumo wa wabunge wa kuteuliwa unampa rais au mkuu wa serikali nafasi ya kumpa mteule uwaziri hata kama mtu huyu hakuchaguliwa au hakupatikana kwa mfumo wa siasa wa kawaida
- kwa vyovyote, uteuzi kama mbunge ni namna ya kumzawadisha mfuasi mwaminifu au kuendelea na mwanasiasa aliyefeli kwenye uchaguzi
Tanzania
haririNchini Tanzania ibara 66, 1e ya katiba inampa rais haki ya kuteua wabunge wasiozidi 10; angalau 5 kati yao ni wanawake.
Kenya
haririBunge la Kenya huwa na wabunge wa kuteuliwa 12 pamoja na 237 wanaochaguliwa. Wabunge hao wanateuliwa na vyama vya kisiasa kufuatana na idadi ya wabunge waliochaguliwa kwa vyama hivyo[1].
Singapur
haririNchini Singapur kuna wabunge wa kuteuliwa 9 pamoja na wabunge 95 waliochaguliwa. Majina yanapendekezwa na kamati ya bunge na kuteuliwa na rais kwa kipindi cha miaka 2 na nusu. Kusudi la kuteua ni kuongeza mawazo ya raia wenye utaalamu fulani au michango maalum katika jamii; wabunge wa kuteuliwa hawana haki ya kupiga kura katika maazimio ya bunge lakini wana haki ya kuchangia maoni.
Uhindi
haririKatika bunge la wananchi la Uhindi Lok Sabha kuna wabunge 2 wa kuteuliwa na rais, katika bunge la majimbo Rajya Sabha kuna wabunge 12 wa kuteuliwa katika jumla ya 250. Utaratibu unaelezwa katika ibara 4 na 80 za katiba. Rais anateua raia 12 wenye michango maalumu katika sanaa, sayansi, fasihi au huduma za kijamii.
Zambia
haririBunge la Zambia lina wabunge wa kuteuliwa 8, pamoja na wabunge wanaochaguliwa 156. Uteuzi umo mikononi mwa rais.
Marejeo
hariri- ↑ http://www.parliament.go.ke/the-national-assembly/about About National Assembly, Tovuti ya Bunge la Kenya, iliangaliwa Aprili 2022