Wiper Democratic Movement

Wiper Democratic Movement ni chama cha kisiasa nchini Kenya. Chama hicho kilianzishwa mwaka 2006 katika maandalizi ya uchaguzi wa bunge la Kenya wa mwaka 2007 ikijulikana kama Orange Democratic Movement-Kenya.

Katika Agosti 2007 chama hicho kilifarakana kati ya wafuasi wa Kalonzo Musyoka aliyeendelea kwa ODM-Kenya na maungano ya viongozi wengi zaidi pamoja na Raila Odinga walioendelea kama Orange Democratic Movement. Sababu ya farakano ilikuwa suala la nani atakuwa mgombea wa urais upande wa ODM[1].

Basi, kilitoka katika Orange Democratic Movement Party of Kenya (ODM) na kinaongozwa na Kalonzo Musyoka, ambaye aligombea urais mwaka wa 2007.

Chanzo cha ODM katika kura ya katiba mpya hariri

Chanzo cha ODM kilikuwa kura maalumu ya wananchi ya 2005 kuhusu katiba mpya. Katiba ilipendekezwa na rais Mwai Kibaki na wafuasi wake. Wabunge wa LDP walipinga pendekezo la katiba pamoja na chama cha upinzani cha KANU chini ya Uhuru Kenyatta. Pande mbili katika kura hii zilipewa alama za ndizi (kambi ya "ndiyo") na chungwa (kambi ya "hapana").

LDP na KANU zilishirikiana pamoja katika kambi ya machungwa. Baada ya katiba kukataliwa na wananchi katika kura maalumu Kibaki aliondoa wafuasi waote wa kambi la machungwa katika serikali yake.

Kuunda chama na farakano hariri

Hapa waliamua kuandaa chama kipya pamoja na KANU kwa ajili ya uchaguzi wa 2007.

KANU ilijiondoa kabla ya uchaguzi lakini viongozi kadhaa kama vile Musalia Mudavadi na William Ruto walibaki upande wa ODM.

Swali la kumteua mgombea wa urais iligawa ODM kwa sababu viongozi mbalimbali walitaka kushika nafasi hii. Hii ilileta farakano kati ya ODM chini ya Raila Odinga na ODM-Kenya chini ya Kalonzo Musyoka.

Uchaguzi wa 2007 hariri

Kundi la Raila, ambalo pia lilijumuisha Musalia Mudavadi, William Ruto, Joseph Nyagah na Najib Balala, lilinunua chama cha ODM halisia kutoka kwa Mugambi Imanyara, wakati kundi la Kalonzo, likijumuisha mwenyewe na Julia Ojiambo, lilibakia katika ODM-Kenya.

Makundi hayo mawili yalifanya uchaguzi wa kumchagua mgombea wao wa urais siku kadhaa mfululizo katika jumba la michezo la Kasarani mjini Nairobi. Tarehe 31 Agosti 2007, Kalonzo Musyoka alimshinda Julia Ojiambo kwa tiketi ya ODM-Kenya. Tarehe 1 Septemba, Raila Odinga alichaguliwa mgombea urais wa ODM. Raila na Kalonzo walikabiliana na rais Kibaki katika uchaguzi mkuu. Kalonzo aliibuka wa tatu, lakini mnamo Januari 2008, akawa makamu wa rais wa Kenya chini ya Kibaki, ambaye ushindi wake ulikataliwa na Raila Odinga na ODM.

Kufuatia mgogoro wa Kenya wa 2007-2008, uliosababisha vifo vya watu wengi, serikali ya umoja wa kitaifa iliundwa kati ya PNU ya Kibaki na ODM ya Odinga, pamoja na Musyoka kubakiza nafasi yake kama makamu wa rais. Hadi wa sasa, Musyoka ni mmoja wa wafuasi wawili wa ODM-K walio katika baraza la mawaziri, pamoja na Mutula Kilonzo kama Waziri wa Ustawi wa Jiji la Nairobi, kwani kundi lake lilipata kura kidogo sana katika uchaguzi wa bunge.

Katika uchaguzi wa 2007 ODM-Kenya haikutokea kama chama cha kitaifa. Kilikuwa na nguvu katika Ukambani ilipochukua majimbo ya uchaguzi 13 kati ya 17 za Ukambani. Ikaongeza majimbo mawili ya Bura na Saku nje ya Ukambani, jumla la wabunge 15.

Kalonzo Musyoka alipata asilimia 9.5 za kura katika uchaguzi wa rais akamaliza nafasi ya tatu. Alitangaza atakuwa tayari kuingia katika ushirikiano na rais atakayechaguliwa. Baada ya uchaguzi ODM-K iliingia katika serikali ya mseto na PNU ya Mwai Kibaki. Kiongozi wake Musyoka alipewa nafasi ya makamu wa rais na mwenyekiti wa chama Samuel Poghisio akawa waziri wa mawasiliano na habari kati ya mawaziri 15 wa kwanza walioteuliwa na Kibaki baada ya uchaguzi wake uliopingwa na ODM.

Sheria ya Vyama vya Kisiasa hariri

Mnamo Desemba 2008, chama cha ODM-Kenya kilifanya uchaguzi kwa kuzingatia sheria iliyopitishwa hivi karibuni ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa [2]

Mwaka 2011 jina la chama lilibadilishwa kuwa Wiper Democratic Movement, ili kuwezesha wafuasi wake kuitofautisha na chama cha ODM.

Tanbihi hariri

  1. "upinzani nchini Kenya wagawanyika mara mbili",BBC News, 15 Agosti 2007
  2. Ni vyama vinane tu ambavyo vimekubaliwa http://www.eastandard.net/InsidePage.php?id=1144002455&cid=4 Archived 9 Januari 2015 at the Wayback Machine.

Viungo vya nje hariri