Yahya Sinwar (Khan Younis, Ukanda wa Gaza, 29 Oktoba 1962 - Rafa, Ukanda wa Gaza, 16 Oktoba 2024) alikuwa kiongozi wa Hamas aliyeuwawa na jeshi la Israeli akiwa anapambana nao ana kwa ana.[1]

Yahya Sinwar, mfia taifa la Palestina

Kwa nini kauwawa

hariri

Yahya Sinwar si tu alionekana kuwa ndiye kiongozi mkuu wa kundi la kijeshi na upande wa siasa wa Hamas kwa sasa kufuatia kuuwawa kwa aliyekuwa kiongozi wao, Ismael Haniyeh, bali pia Israeli ilikuwa ikimtuhumu kuwa ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa shambulio la Hamas dhidi ya Israeli la Oktoba 7, 2023, lililosababisha vifo vya zaidi ya Waisraeli 1200 na kutekwa kwa zaidi ya raia 200 wa nchi hiyo.[2]

Israeli na washirika wake wakiongozwa na Marekani, waliamini kuwa endapo bwana Sinwar angekamatwa ama kuuwawa, basi suluhu ya vita vya Gaza ingekuwa rahisi kuipata. Hata hivyo, Sinwar alikuwa jemedari jasiri mno na mwingi wa ujanja wa porini na mbinu za kivita: wasingeweza kumkamata. Naye Yahya alikuwa akijua sana kuwa alikuwa akisakwa kwa udi na uvumba ili akamatwe au auwawe. Akawa daima yupo mstari wa mbele kwenye uwanja wa mapambano, akipigana na kuwaongoza wapiganaji wake hadi mauti yalipomfika na kufa kishahidi.[3]

Ilivyotokea

hariri

Mnamo tarehe 17 Oktoba, 2024, Jeshi la Ulinzi la Israeli, "IDF" lilitangaza kuwa kiongozi na kamanda mkuu wa Hamas Yahya Sinwar, ameuwawa siku moja iliyotangulia katika mapambano dhidi ya Brigedi ya 828 ya Bislamach mjini Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa taarifa za IDF na Shin Bet.[4] Mizinga ya kifaru ilitumika kulilipua jengo lililokuwa likilindwa na vilipuzi vingi na droni yenye kamera ilitumika kuhakikisha kuwa hakuna mpiganaji wa Hamas aliyebakia.

Redio ya Jeshi la Israeli ikatangaza kuwa vipimo vya DNA vilikuwa vikifanyika kupata hakika kuwa Sinwar ndiye aliyeuwawa.[5] Polisi wa Israeli walisema katika taarifa yao kuwa taarifa za marehemu zimeshabihiana na kumbukumbu za Sinwar za meno na alama za vidole. Sinwar, ambaye alikuwemo kwenye orodha ya watu waliokuwa wakisakwa sana na Israeli kufuatia shambulio la Hamas la Oktoba 7, alikuwa kwenye jengo hilo na wenzake wawili (Maelezo ambayo yanapingwa vikali na Hamas na umma wa Wapalestina wakisema Israel imebuni maelezo hayo ya jinsi alivyokutwa na kuuwawa ili kuibomoa haiba yake ya kamanda hodari, shupavu, jasiri na mwamasishaji wa kupigiwa mfano. Wanasema: Sinwar aliuwawa akiwa [[mstari wa mbele] akipigana bega kwa bega na wapambanaji wa Hamas. Kituo cha runinga cha Al Jazeera kilitangaza maoni hayo ya watu pamoja na kuyaandika[6]).

Shambulio la kijeshi lililomuua lilielezwa kuwa halikuwa la kupangwa na lilimnasa kibahati. Wachunguzi wa mambo ambao waliwahi kumhoji Sinwar kipindi alipokuwa kizuizini kadhalika daktari wa meno, waliitwa kwenye mchakato wa utambuzi wa mwili wa marehemu, ambao ulikuwa umesafirishwa hadi Israeli.

Mwitikio wa Hamas

hariri
 
Khalil al-Hayya (katikati)

Hamas ilikaa kimya kwa saa takriban 40 licha ya taarifa zilizokuwa zikisambaa kwa kasi mitandaoni na kwenye vyombo vikubwa vya habari duniani. Ni mpaka kufikia jioni ya Ijumaa ya tarehe 18 Oktoba, ndipo tamko lao rasmi la kuthibitisha kuuwawa kwa kiongozi huyo lilitolewa. Khalil al-Hayya, ambaye alikuwa makamu wa Sinwar huko Qatar pia akiiwakilisha Hamas kwenye awamu mbalimbali za mazungumzo ya kumaliza mapigano na kuleta upatanisho, alisema kiongozi huyo mwenda zake " alikuwa akipambana ana kwa ana na jeshi la walowezi hadi pumzi yake ya mwisho." Hamas haitomrudisha mateka yeyote, aliongeza, "hadi Israeli ikomeshe operesheni ya kinyama huko Gaza na kuondoka kwake Gaza.”[7]

Mwitiko wa Iran, Hezbollah

hariri

Iran na Hezbollah ndio pande kuu ziiteteayo Hamas. Iran imetoa kauli kufuatia kifo cha Yahya kwa kusema ameifia Palestina yake. Ni kifo cha heshima. Ikaongeza kwa kusema kifo hicho kitachochea mapambano zaidi dhidi ya Wazayuni. Nao Hezbollah, waungaji mkono wa hali na mali wa Hamas, wametoa tamko zito linalosadifu hasira yao kali inayotokana na kuuliwa kwake. Hezbollah imesema, israeli itarajie mashambulizi makali kutoka kwao ikiwa ni malipizi ya kuuwawa kwake.[8]

Mwitikio wa washirika wa Israeli

hariri

Wakati mataifa mengi yanayoihurumia Palestina hayajatoa kauli za wazi juu mtazamo wao kuhusu kifo hicho, washirika wa karibu wa Israeli na Israeli yenyewe, wameonesha kufurahishwa sana na kifo cha Sinwar. Rais Joe Biden ambaye Israeli ilimtumia taarifa rasmi juu ya kifo hicho mapema kabisa, alionekana kwenye runinga alipongeza ' mafanikio ' hayo huku akisema, "ilikuwa siku njema" na kuonesha kuamini kuwa kufa kwa Sinwar ni mwanzo wa kumalizika kwa vita vya Gaza.[9]

Hali kadhalika, makamu wa rais wa Marekani na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Kidemokrasia cha nchi hiyo, Kamala Harris, ameipongeza Israel Kwa hatua hiyo na kusema kuwa kifo cha Sinwar ni fursa ya kumaliza vita vya Gaza na kufungua njia za misaada ya kibinadamu kwenye ukanda huo.[10]

Pamoja na kauli hizo za viongozi wa Marekani, kauli aliyoitoa Benjamin Netanyahu imefifisha matumaini ya wengi juu ya kumaliza vita hivyo kwani alitamka kuwa, ujumbe wake kwa watu wa Gaza ni kwamba kuuwawa kwa Sinwar kutakuwa ni kumalizika kwa vita kama Hamas wataweka silaha chini na kuwarejesha raia wa Israeli wanaowashikilia mateka[11]. Kafifisha matumaini, na Hamas wameshamjibu kuwa hawatorudi nyuma na hawatowaachia mateka wao hadi Israel iwaachilie maelfu ya Wapalestina inaowaweka kizuizini sambamba na kuondoka Ukanda wa Gaza.[12]

Tanbihi

hariri
  1. https://www.npr.org/2024/10/17/nx-s1-5155887/hamas-yahya-sinwar-israel-gaza
  2. https://edition.cnn.com/world/live-news/israel-iran-gaza-lebanon-10-17-24-intl-hnk/index.html
  3. https://www.aljazeera.com/news/2024/10/17/israel-claims-hamas-leader-yahya-sinwar-has-been-killed
  4. "Officials to 'Post': Hamas leader Yahya Sinwar killed in Rafah, Gaza Strip". The Jerusalem Post. 17 Oktoba 2024.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. "Israel says Hamas leader Yahya Sinwar slain in southern Gaza Strip". CBC. 17 Oktoba 2024. Iliwekwa mnamo 17 Oktoba 2024.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. https://www.aljazeera.com/news/liveblog/2024/10/18/live-israel-says-hamas-chief-yahya-sinwar-killed-war-on-gaza-to-continue?update=3256029
  7. https://abcnews.go.com/International/wireStory/hezbollah-vows-new-phase-war-israel-killed-hamas-114920852
  8. https://www.timesofisrael.com/hezbollah-vows-escalation-after-sinwars-death-iran-says-resistance-will-endure/
  9. https://www.politico.com/news/2024/10/18/biden-israel-sinwar-death-cease-fire-talks-00184344
  10. https://www.theguardian.com/world/2024/oct/17/kamala-harris-yahya-sinwar-death-reactions
  11. https://edition.cnn.com/world/live-news/israel-hamas-lebanon-sinwar-gaza-iran-10-18-24-intl-hnk/index.html
  12. https://www.france24.com/en/middle-east/20241018-live-netanyahu-says-killing-of-hamas-chief-beginning-of-the-end-of-gaza-war