Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani

Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani (kwa Kijerumani Deutsch-Südwestafrika) ilikuwa koloni la Ujerumani katika Afrika kuanzia mwaka 1884 hadi 1915. Leo hii ni nchi ya Namibia.

Ramani ya Kijerumani ya Afrika ya Kusini-Magharibi (Namibia)

Tangu mwaka 1891 Windhuk ilikuwa mji mkuu wa koloni. Sawa na Namibia ya leo, koloni lilikuwa na eneo la kilomita za mraba 835,100. Eneo la hori ya Walfish Bay ilikuwa chini ya Uingereza, baadaye kama eneo la Afrika Kusini.

Kutokana na tabia yabisi ya nchi, maeneo makubwa yalikuwa na wakazi wachache tu. Hata hivyo Wajerumani walikuta upinzani mkali wa wenyeji, hasa Waherero na Wanama, walioshindwa katika vita vya miaka 1904-1908; takriban Waherero 80,000, Wanama 10,000 na Wajerumani 1,749 walikufa kutokana na mapigano hayo.

Mwaka 1915 nchi ilivamiwa na jeshi la Uingereza na Muungano wa Afrika Kusini na utawala wa Kijerumani ukaisha.

Mwaka 1922 eneo likawa eneo la kudhaminiwa kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa kwa jina la Afrika ya Kusini-Magharibi (South-West Africa). Hatua hiyo ilikuwa msingi kwa uhuru wa Namibia kama nchi ya pekee nje ya Afrika Kusini.