Afrika ya Kusini-Magharibi
Afrika ya Kusini-Magharibi (au kwa Kiingereza South-West Africa) ilikuwa jina la eneo la Namibia ya leo kuanzia mwaka 1922 hadi uhuru wa nchi ya Namibia mwaka 1990.
Maeneo yake yaliunganishwa mara ya kwanza ilipokuwa koloni la Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani kwenye mwaka 1884. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilivamiwa na Uingereza na Afrika Kusini. Pamoja na makoloni mengine ya Ujerumani iliwekwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa.
Hivyo tangu 1922 ilikuwa eneo la kudhaminiwa na kukabidhiwa kwa Afrika Kusini.
Wakati wa kuvunjwa kwa Shirikisho la Mataifa mwaka 1946, Umoja wa Mataifa ulichukua wajibu wa kuratibu maeneo ya kudhaminiwa[1].
Afrika Kusini haikutambua badiliko hili ikitangaza ya kwamba hali ya udhamini ilikuwa ya Afrika ya Kusini-Magharibi tangu kuvunjwa kwa Shirikisho la Mataifa.
Mwaka 1949 bunge la Afrika Kusini lilitangaza sheria ya kufanya eneo jimbo la tano la Afrika Kusini na kueneza siasa yake apartheid (ubaguzi wa rangi) hadi huko.
Baadaye mfumo wa bantustan sawa na Afrika Kusini ulianzishwa pia huko ambako maeneo makubwa yenye rutuba yalitengwa kwa ajili ya Wazungu ilhali Waafrika walitakiwa kuwa na maeneo kadhaa tu kama "homeland" walipokuwa na haki ya kukaa lakini katika maeneo mengine waliruhusiwa kukaa kama wafanyakazi kwa muda tu. Mfumo huo haukutekelezwa kwa ukali, tofauti na Afrika Kusini yenyewe.
Hii haikukubaliwa na Umoja wa Mataifa ulioendelea kudai ya kwamba Afrika Kusini ilipaswa kuandaa eneo kwa uhuru.
Mwaka 1966 Mkutano Mkuu wa UM uliamua kuondoa mamlaka ya Afrika Kusini na kuweka eneo moja kwa moja chini ya Umoja wa Mataifa. Azimio hilO halikuweza kutekelezwa kwa sababu Afrika Kusini ilikataa.
Hapo wanamgambo wa chama cha SWAPO walichukua silaha wakajaribu kupigania uhuru.[2].
Azimio la Mkutano Mkuu wa UM la mwaka 1968 lilibadilisha jina la eneo kuwa Namibia.
Mwaka 1971 Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikaamua ya kwamba utawala wa Afrika Kusini si wa haki. Hapo serikali ya Afrika Kusini ikaanza kuchukua hatua za kuandaa uhuru wa eneo hili, lakini vita kati ya jeshi lake, SWAPO na wanajeshi wa Angola na Kuba iliendelea.
Baada ya mapatano ya kumpumzisha silaha mwaka 1988, majadiliano kati ya pande mbalimbali yalianzishwa rasmi na mwaka 1990 nchi ilipata uhuru wake kwa jina la Namibia.
Marejeo
hariri- ↑ Katiba ya UM, kifungu cha 77b
- ↑ Namibian War of Independence 1966-1988 Ilihifadhiwa 5 Machi 2016 kwenye Wayback Machine. Armed Conflict Events Database. Iliangaliwa 2-10-2015.