Bahari kuu
Bahari Kuu (ing. w:ocean) ni jina linalotumika kutaja jumla ya maeneo makubwa ya maji ya chumvi duniani yanayopakana na kufuatana kama gimba moja. Kwa maana hii bahari kuu inafunika zaidi ya theluthi mbili za uso wa dunia.
Bahari Kuu imegawiwa na ardhi ya mabara kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia lakini sehemu zake zinaungana kwenye nusutufe ya kusini.
Ugawaji wa Bahari Kuu ya Dunia
haririEneo hili kubwa huhesabiwa mara nyingi kama bahari kuu tatu yaani:
- Bahari Atlantiki kati ya Amerika upande mmoja na Ulaya - Afrika upande mwingine
- Bahari Pasifiki kati ya Amerika na Asia
- Bahari Hindi kati ya Afrika na Asia.
Hizi sehemu tatu hutajwa pia kama "bahari kuu" kwa kuzitofautisha na maeneo madogo zaidi ya maji ya chumvi au sehemu zinazoitwa bahari ya kando. [1]
Wakati mwingine Bahari ya Aktiki na Bahari ya Antaktiki hutajwa kama bahari kuu ("oceans") za pekee.
Tabia za Bahari Kuu
haririBahari kuu hushika asilimia 97% ya maji yote duniani. Hadi sasa ni asilimia 5 pekee zilizofanyiwa utafiti kamili. [2] Kiasi cha maji yote kwenye bahari kuu ni takriban kilomita za mjazo bilioni 1.3.
Kiasi cha maji baharini kinajulikana kuwa kilicheza na kubadilika katika historia ya dunia. Wakati wa vipindi vya baridi duniani, kama vile enzi ya barafu, sehemu kubwa ya maji yalipatikana kwa umbo la barafu na maji kiowevu yalikuwa kidogo. [3]. Kuongezeka kwa halijoto duniani kunasababisha kupanda kwa uwiano wa bahari kote duniani. Nchi mbalimbali hasa kwenye pwani au nchi za visiwa zitapungua kieneo.
Halijoto ya bahari na mikondo yake ni athira muhimu mno kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Marejeo
hariri- ↑ Kwa Kiingereza na lugha nyingine kuna tofauti kati ya "ocean" (=bahari kuu) na "sea" (=bahari)
- ↑ http://www.noaa.gov/ocean.html Archived 24 Aprili 2013 at the Wayback Machine. Tovuti ya mamlaka ya bahari na angahewa ya Marekani
- ↑ Mfano: Wakati wa enzi ya barafu Uingereza haikuwa kisiwa bali sehemu ya Ulaya bara maana usawa wa bahari ulikuwa chini ya uwiano wa leo.